Tumshukuru Mungu kwa kutupa uhai sisi Watanzania huku akitutia moyo wa kudumisha amani na utulivu katika taifa letu.Baada ya kusema hayo nianze mada yangu leo kwa kutahadharisha kuwa kwa hali ilivyo sasa hapa nchini, kunahitaji chombo cha kujenga umoja miongoni mwetu ili amani ambayo ni tunu ya taifa iendelee kudumu.
Kwangu naona chombo hicho ni muhimu hasa wakati huu tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Chombo hicho kisiwe chini ya vyama vya siasa, dini, ukanda wala ukabila kwani hakuna nchi inayoweza kusimama na kupata maendeleo ya haraka bila ya kuwa na umoja. Tanzania imesimama imara hadi leo hii kwa sababu ya umoja wa kitaifa uliojengwa na waasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
Hivi sasa nchi yetu inapata sifa kutokana na utulivu na amani kwa sababu ya umoja tulionao.
Enzi hizo tulikuwa na mfumo wa chama kimoja lakini walikuwepo watu wachache walioupinga mfumo huo lakini wote walilenga kujenga umoja wa kitaifa.
Wakati wa kujenga umoja huo, viongozi hawakulenga dini, jambo la kuabudu lilibakia kuwa la mtu binafsi. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, Watanzania walikuwa na dini, lakini Tanzania haikuwa na dini na hilo liliwekwa wazi kwenye Katiba ya Tanzania.
Ukabila ulipigwa vita na utawala wa machifu ulifutiliwa mbali. Lugha ya Kiswahili ilipewa kipaumbele na kuwa chombo cha kuwaunganisha Watanzania wote.
Nchi zinazotumia lugha za kigeni kama lugha zao za kitaifa hadi leo zinapata shida ya kujenga umoja wa kitaifa sina haja ya kuzitaja nchi hizo kwani nyingi ni majirani zetu.Hapa nchini katika kujenga umoja Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), lilianzishwa kwa lengo la kuwakutanisha vijana wasomi na wasio wasomi.
Kipindi chote cha mafunzo ya vijana hawa, uzalendo na umoja wa kitaifa ulisisitizwa hivyo kupunguza kasi ya ukabila, ukanda, majivuno na kiburi. Jeshi liliwatendea vijana wote haki sawa, bila ya kujali mtoto wa tajiri, kiongozi au mtoto wa mkulima.
Mfumo wa elimu ulikuwa mzuri, kijana wa Mwanza alikuwa anapelekwa kusoka Mtwara, wa Kigoma anapelekwa Tanga na wa Dodoma anapelekwa Mbeya nk. Hii ilisaidia kuwakutanisha vijana na kujenga umoja wa kitaifa.
Mwenge wa Uhuru ulibuniwa kwa lengo la kujenga na kuchochea umoja wa kitaifa.
Mwaka 1992, Tanzania ilijiingiza rasmi katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Wapinzani pamoja na chama tawala, wanaangalia zaidi umoja wa vyama vyao kuliko umoja wa kitaifa. Wanatanguliza mbele ari ya kuingia ikulu, ruzuku, mbwembwe za madaraka na ushindani wa chuki na utengano.
Wakati wanasiasa wa zamani walikuwa na sera ya uhuru na umoja, wanasiasa wetu wa leo ni vigumu sana kupambanua sera zao na kama zipo wanazipuuza.Baadhi ya vigogo wa CCM wakati tunalilia umoja wa kitaifa, wao wanalilia umoja wa chama chao na jambo la muhimu ni kutanguliza ‘uchama.’
Mfumo wa elimu umevurugika, shule nyingi za binafsi na sekondari za kata zimeanzishwa na kuchochea watoto wengi wasiweze kuivuka mikoa yao.
Watoto wa matajiri hawasomi tena na watoto wa maskini. Kiwango cha elimu kimeanza kutofautiana na kuleta hatari ya kuanza kuunda matabaka na kuvuruga umoja kitaifa. Tabaka ni adui mkubwa wa umoja na amani. Baadhi ya watoto wa wakubwa wanavuka mipaka ya nchi na kwenda kusoma nchi za nje. Hii ni hatari kwa umoja wa kitaifa!
Jambo lingine zito linaloonyesha dalili za kutishia uhai wa umoja wetu ni dini! Hasa hizi kubwa za Uislamu na Ukristo.
Kila tunapoingia kwenye mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Taifa, baadhi ya Waislamu wanamtaka rais Mwislamu na baadhi ya Wakristo wanamtaka rais Mkristo japokuwa Mwalimu Nyerere alikemea hili.
Watanzania wengi wamejiingiza kwenye udini na ni vigumu kuwaambia wazikimbie maana zinahatarisha umoja wa taifa letu.Wakati umefika wa kuzilazimisha dini hizi zikakubali utamaduni wetu wa umoja, utulivu na amani.
Wale wanaoiona hatari iliyo mbele yetu ni lazima waungane nami na wafikirie jinsi ya kuunda chombo cha kujenga umoja wa kitaifa ambacho hakitatawaliwa na wanasiasa, wa dini na ukanda kwani bila kufanya hivyo, taifa litaangamia!
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.
Credit:GPL
No comments:
Post a Comment