ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 19, 2015

VURUGU KUBWA ZAZUKA TUNDUMA


Wakazi wa Mji wa Tunduma, Wilaya ya Momba, Mbeya wakiangalia moto uliowashwa katikati ya Barabara ya Tunduma-Sumbawanga jjana baada ya kutokea vurugu baina ya wananchi na askari wa kikosi cha Kutuliza Ghasia.

Tumepata habari za kusikitisha kutoka Tunduma mkoani Mbeya kwamba, kwa siku tatu mfululizo, mji huo, ambao ni lango la biashara kusini mwa Tanzania, uligeuka uwanja wa mapambano kati ya Askari wa Kutuliza Ghasia (FFU) na makundi ya vijana.
Taarifa ya Jeshi la Polisi ilisema kwamba vurugu hizo zilitokana na makundi mawili yaliyokuwa yakivutana kuhusu matumizi ya kiwanja; moja likidai ni mali ya CCM na jingine likidai ni kwa ajili ya ujenzi wa zahanati.
Baada ya ugomvi huo kuibuka, hakuna uongozi wa Serikali uliotumia busara ya kuyakalisha makundi hayo yanayotofautiana kwa misimamo ya vyama, kuzungumza na kuupatia ufumbuzi mgogoro huo; badala yake askari wa FFU walifika na kuanza kuwapiga kwa virungu na mabomu ya kutoa machozi kwa lengo la kuwatawanya na kurejesha amani.
Siku ya kwanza; Jumatatu, askari hao walidai walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya vijana waliokuwa wanapinga CCM kutwaa kiwanja hicho ikidai ni wahuni. Watu kadhaa akiwamo Diwani wa Kata ya Tunduma (Chadema), walikamatwa na kuwekwa mahabusu.
Siku ya pili; Jumanne polisi walidai walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kutawanya vijana waliodaiwa kujikusanya kutaka kuwatoa, kwa nguvu, diwani huyo na wenzao waliokuwa wamekamatwa na kuwekwa mahabusu. Polisi walidai kwamba walipata taarifa za kuwapo maandamano ya kushinikiza diwani huyo aachiwe huru.
Siku ya tatu; Jumatano polisi walipambana tena na vijana kwa mabomu ya kutoa machozi ili kujihami walipokuwa wakishambuliwa na wananchi waliokuwa wanawashtumu kwamba ndiyo wanaharibu nyumba, vibanda vya biashara na kupora mali.
Kutokana na vurugu hizo ofisi za Serikali, watu binafsi, biashara mbalimbali na maduka katika eneo hilo zilifungwa hali iliyoathiri shughuli za uchumi na usalama wa raia na mali zao.
Inasikitisha kuona kwamba licha ya kutoa ushauri mara kadhaa, busara itumike katika mazingira kama haya ili kuepusha vurugu, bado polisi wamekimbilia kupiga watu, kuwamwagia maji ya washawasha na kuwapiga kwa mabomu ya machozi, kujeruhi na kukamata wengine na kuwatia mahabusu.
Hata katika matukio mengi, kama si yote, Polisi, ambao kwa viapo vyao wanatakiwa kulinda usalama wa watu na mali zao, wamekuwa wakituhumiwa kuwa ndiyo wa kwanza kuzusha vurugu. Katika maeneo mengi nchini, wananchi na hasa vyama vya siasa walipokusanyika na kujilinda wao wenyewe, wamekuwa wakiondoka salama, lakini pale polisi walipoingilia kati ndipo tumeshuhudia vurugu.
Hivi kabla ya kurusha mabomu, polisi walijiuliza na kuwa na uhakika waliokuwa wanataka kiwanja kwa ajili ya zahanati hawakuwa na haki?
Hivi kabla ya kutumia nguvu, kupima vijana hao na kumtia ndani diwani, walijihakikishia pasi na shaka kuwa huo ulikuwa uchochezi?
Tunashauri kwamba wakati umefika sasa, katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, Jeshi la Polisi lijitathmini ili kuzuia madhara. Raia wakijikusanya, kwa vyovyote huwa lipo jambo zito, muhimu na wakati mwingine la dharura hivyo, kuwatawanya bila kuwasikiliza au kutatua tatizo, ni kutowatendea haki.
Jeshi la Polisi litajijengea heshima katika jamii ikiwa litaacha kutumika kisiasa; lifanye kazi zake kwa weledi litende haki na kila upande uone kwamba haki imetendeka. Huo ndiyo utawala bora, wa sheria na unaozingatia haki.
Ndiyo maana tunaiomba Serikali kuingilia kati kumaliza tatizo hili kwa amani.
MWANANCHI

No comments: