KURUGENZI YA MAMBO YA NJE
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
SERIKALI YA TANZANIA ICHUKUE HATUA ZA
HARAKA
KUNUSURU WATANZANIA WAISHIO AFRIKA KUSINI
DHIDI YA GHASIA NCHINI HUMO
Kumekuwepo na hali ya raia wa Afrika
Kusini kushambulia , kujeruhi na kuua raia wa kigeni wa Kiafrika wanaoishi
nchini Afrika Kusini. Hali hii inadaiwa kuchochewa na
ukosefu mkubwa wa ajira kwa wananchi wa Afrika Kusini wanaodai ajira hizo
kuchukuliwa na Waafrika wa mataifa mengine na hivyo wao wenyeji kubakia kwenye
dimbwi kuu la umasikini.
Ni mtazamo wa kuimarika kwa kiwango
cha umasikini kwa wananchi wengi nchini humo dhidi ya kuimarika kwa kiwango cha
utajiri kwa wachache kunakopelekea ghasia hizi. Zaidi, mali za Waafrika wageni nchini
humo zimekuwa zikiharibiwa baada ya
wamiliki kukoswa katika mashambulizi hayo. Aidha, kama nchi nyingine za
Kiafrika, Tanzania ina idadi kubwa ya raia wake wanaoishi nakufanya kazi nchini
Afrika Kusini. Na mpaka sasa inadaiwa kuwa watanzania wawili (2) wameuwawa
katika ghasia hizo za wenyeji dhidi ya Waafrika wageni.
1. CHADEMA inalaani vikali hali ya raia
kudhuru na kutwaa uhai wa raia yoyote yule. CHADEMA kama muumini wa haki za
binadamu inayojumuisha haki kuu ya kuishi inasikitishwa na hali hiyo ya
machafuko inayoondoa usalama wa sio tu kwa raia wa kigeni wa Kiafrika walioko
Afrika Kusini bali pia kwa raia wengine wa Afrika Kusini ambao hawawezi kufanya
shughuli zao kwa ukosefu wa usalama nchini humo.
CHADEMA inawasii raia wa Afrika
Kusini kuwachukulia Waafrika wenzao kutoka mataifa mengine kama ndugu zao ambao
kwapamoja walishrikiana kupambana na ubaguzi wa rangi na hatimaye kuleta uhuru kwa taifa hilo. Ni muhimu raia wa
Afrika Kusini wakatatua matatizo yao ya ndani
hasa ya kiuchumi kwa kushirikina na wenzao wa mataifa ya Afrika waishio
nchini humo na si kuwaona kama maadui zao.
2. CHADEMA inaitaka serikali ya Tanzania
ishirikiane na serikali ya Afrika Kusini kuchukua hatua za haraka kunusuru
maisha ya watanzania waishio nchini Afrika Kusini dhidi ya ghasia hizi kwa
kuwahakikishia usalama wao ama kuwawekea utaratibu wa kuondoka ama nchini humo
na kurejea nyumbani ama kwenye miji yenye machafuko kama Durban na kuwapeleka
kwenye miji ya usalama zaidi mpaka hali itakapotengamaa kwenye miji hiyo kama
ilivyofanya kwa Watanzania waishio Yemen ambako nako machafuko yamekithiri. Ni
muhimu Serikali ikawa makini kwa jambo hili kwani teyari mataifa mengine ya
kiafrika ya Botswana, Malawi na Zimbabwe yaneshaanza kuwaondoa raia wake nchini
humo kwa kuhofia usalama wao.
3. CHADEMA inazikumbusha nchi za
Kiafrika ambazo zina utajiri mkubwa wa rasilimali kuhakikisha inatatua matatizo
ya kiuchumi yanayozikabili nchi hizo ikiwa ni pamoja na kupunguza tofauti ya
kipato kati ya wengi wasio nacho na wachache wenye nacho.
Ni muhimu serikali hizi kujikita
katika kupambana na umasikini kwa kutengeneza fursa za ajira kwa raia wake na
hivyo kupunguza kiwango cha umasikini na hatimaye kuondoa mazingira ya
machafuko yanayosababishwa na hasira za wananchi kutokana na hali yao ya
umasikini. Kwa mantiki hiyo, ni muhimu Jumuiya
za kikanda na Umoja wa Afrika wenyewe (AU) zikaweka msisitizo wa ukombozi wa
kiuchumi unawaweza kukidhi haja na matakwa ya raia wa bara hili.
4. Kipekee, CHADEMA inaikumbusha
serikali ya Tanzania kuichukilia hali ya Afrika Kusini kama taadhari kwake kwani hali ya umasikini na
ukosefu wa ajira hapa nchini imekuwa kubwa kiasi cha kuibuka kwa vikundi vya
kihalifu vya Komando Yoso na Panya Road vilivyofanya mashambulizi na uporaji
kwa raia wengine. Tofauti ndogo iliyopo kati ya Afrika Kusini na Tanzania ni
kwamba Afrika Kusini raia wazalendo wanashambulia waafrika wa mataifa mengine
wakati hapa Tanzania ilikuwa ni kushambuliana baina ya Watanzania.
Imetolewa leo tarehe 18.04.2015
Jijini Dar es salaam na;
Deogratias Munishi
Mkuu wa Mambo ya Nje – CHADEMA
+255715887712
No comments:
Post a Comment