ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 5, 2015

HISTORIA YAANDIKWA MJINI ADDIS ABABA- WHEN PRINCE OF SWAHILI BLUES MET THE LEGENDARY KING OF ETHIO JAZZ

 Hannival akipapasa zeze la Kihabeshi
 Timu kamili ya Ethio-Swahili  Fusion wakishambulia
 Juma Setumbi akipongezwa na mkongwe Dr Mulatu

Shabiki kutoka Brazil akimpongeza Dr Mulatu
 Leo Mkanyia akimkaribisha rasmi King of Ethio Jazz Dr Mulatu
 Dr Mulatu na Leo wakishambulia jukwaa
 Wadada wa Kihabeshi wakitwanga Swahili Blues kihabeshi habeshi


Dr Mulatu na Leo wakishambulia jukwaa
Mkongwe Dr Mulatu akimtoa kamasi Leo


Siku ya Jumamosi ya tarehe 4 April 2015 mjini Addis Ababa, historia iliandikwa pale Leo Mkanyia na Swahili Blues Band walipopiga jukwaa moja na gwiji la muziki la kimataifa na mfalme wa Ethio Jazz Dr Mulatu Astatke katika ukumbi maarufu wa African Jazz Village.


Shoo hiyo kali sana na ya kihistoria ilianza saa tatu kamili za jioni pale Swahili Blues Band walipofanya ufunguzi kwa kupiga nyimbo zao kwa takriban saa moja kabla ya kumkaribisha Dr Mulatu ukumbini. Nyimbo hizo zilizokuwa na mahadhi kamili ya Kitanzania ziliwabamba vilivyo wapenzi lukuki waliohudhuria na kubahatika kuwa miongoni mwa watu walioshuhudia historia ikitengenezwa. Wapenzi hao wa mataifa mbali mbali walibambika vilivyo na miziki hiyo iliyoundwa kutoka makabila mbalimbali ya Kitanzania yakiwemo ya Kimakua, Kizaramo, Kingoni na Kimakonde. Utamaduni halisi wa Kitanzania ulidhihirishwa pale wanamuziki walipocheza mirindimo ya ngoma kama vile Mtara ya kimakua, mdundiko, lizombe na sindimba.


Muziki huo wa Kitanzania ulihudhuriwa na wageni wengi wakiwemo wageni maalumu kama vile mabalozi kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Brazil, Argentina, Ufaransa, Lebanon, Israel, Marekani na wawakilishi kutoka mashirika kama vile UNHCR, UNICEF na Alliance Francaise.


Nyimbo za ufunguzi zilizopigwa na Swahili Blues Band zilikuwa pamoja na Dunia Hii, Mwanangu, Mdundiko, Binti Ally na Che Maria.


Saa nne kamili Leo Mkanyia alimkaribisha rasmi jukwaani Dr Mulatu kwa ajili ya kujiunga rasmi kupiga pamoja na Swahili Blues Band. Dr Mulatu alikuja na mwanamuziki mmoja kutoka Ethiopia anayepiga zeze la kiasili la ki Ethiopia pamoja na wanenguaji wawili wa kike wanaocheza mirindimo ya ki Ethiopia. Dr Mulatu alipiga vingoma vyake vidogo viwili pamoja na chombo chake mahsusi ambacho ni marimba ya umeme yaani Xylophone huku akitegemea mirindimo kutoka nyimbo za Swahili Blues.



Dhana nzima ya shoo hii ilikuwa ni kukutanisha tamaduni kutoka Afrika Mashariki na Ethiopia.Ilikuwa fursa mahsusi yakukutanisha Swahili Blues na Ethio Jazz.Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa gwiji huyu kupiga jukwaa moja na kwa pamoja na wanamuziki kutoka Afrika Mashariki huku gwiji akipiga muziki wa Kitanzania. Kwa mujibu wa Dr Mulatu, mirindimo hii ya Kitanzania inashabihiana sana na ngoma kutoka kaskazini mwa Ethiopia. Na hii ndiyo ilirahisisha kwake kufanya fusion hii mahsusi na maalumu kabisa.


Nyimbo sita za Swahili Blues zilipigwa kwa umahiri wa hali ya juu huku Dr Mulatu akijibishana kwenye ngoma na mpiga ngoma maarufu wa Swahili Blues Bwana Juma Setumbi. Mabishano hayo yaliendelea tena pale Juma alipohamia kwenye marimba ya kiswahili na mkongwe kuhamia kwenye Xylophone yake.Yalikuwa ni majibishano yaliyonoga kwa sana kabisa. Mamia ya wapenzi waliripuka kwa shangwe, nderemo, mbinja na vifijo pale majibishano hayo yalipokuwa yakiendelea. Kwa kweli ilikuwa ni shoo kabambe na ya kimataifa.


Nyimbo zilizopigwa katika fusion hiyo zilikuwa ni Seychelles, Afrika, Aichelelo, Wazazi Wangu, Sawa Saware na Bwana Mdogo.


Baadhi ya wapenzi waliohudhuria walihojiwa na waandishi wetu na kutoa maoni mbalimbali juu ya shoo hii kama ifuatavyo;


-Solomon Alemayehu kutoka Ethiopia- hii ni shoo kabambe ambaye haijawahi kutokea hapa Ethiopia kwenye miaka ya karibuni. Hakika hii bendi ni kali kweli kweli na miziki yake ni kitamaduni haswaa. Sijawahi kuona Dr Mulatu akipiga huku akitoka jasho namna ile.Hakika historia imeandikwa leo.

- Muna Tadese, Mmarekani mwenye asili ya ki Ethiopia anayeishi Atlanta Marekani- maingiliano ya kiutamaduni tuliyoyaona leo hakika yamedhihirisha kuwa Afrika ni nchi moja kubwa kiutamaduni. Kazi nzuri sana imefanyika jioni ya leo.


-Luiza Benicio kutoka Salvador Brazil- shoo ya leo imenikumbusha ngoma na dansi maalumu inayopigwa nchini kwetu maarufu kama Capoeira. Nitafanya juhudi kubwa kuhakikisha Bendi hii inakuja nchini Brazil kuendeleza mahusiano mazuri ya kiutamaduni miongoni mwetu. Nimefurahishwa sana

No comments: