Miaka kadhaa nyuma aliibuka msanii mchanga na nyimbo kali na zilizogusa mioyo ya wengi, hisia kali, mashairi yenye mpangilio na hata vina vilivyosimama kwa unadhifu, walilia wenye kulia kwa tungo hizo, wakafurahi wenye kufurahishwa na utunzi huo, vijana wakasema dah!, mshikaji ni noumaa!, ndio, hayo ndo maneno yetu vijana tukimkubali mtu, ila wazee nao wakasema Mungu amzidishie na kumbariki kijana huyu. Ndio, maneno ya wakubwa dawa bwana, na Mungu kweli akatenda, kijana akabarikiwa.
Kwa mara ya kwanza nlimskia na wimbo wake ‘nenda kamwambie’, hatukukaa sawa akaruka hewani tena na wimbo mzuri wa ‘Mbagala’, baada ya hapo akafululiza na vibao kadhaa matata, ikiwemo ‘Nitarejea’, ‘Moyo wangu’ na ‘mawazo’, vyote vi kanigusa, si mimi peke yangu, ila wengi wetu tuliguswa na tungo zake, ndio maana nikasema alipata baraka za vijana na wazee.
Akalivuka lile daraja reefu la hofu linaloogopwa na wengi, ‘kufeli’, na sasa akawa ni mmoja wa waliomaarufu nchini, waliombeza wakamkubali, waliompuuza wakamuona anafaa, hakuwa na baiskeli sasa akamiliki magari ya kifahari, na mengine akayatoa zawadi kwa walioichezea bahati, bado wazee wakambariki.
Niliwahi kusikia anataka kujenga nyumba ya ibada, ili wenye mioyo safi wapate sehemu safi na salama ya kumlilia Mola wao, ilinipa faraja na wengi wakazidisha maombi kwake, lilikuwa ni wazo zuri ingawa sikujua wapi liliishia, na bado maombi na baraka za wengi zikazidi kwake.
Ikawa huwezi kufanya onyesho na lijae kama hayupo kijana huyu, itakula kwako nzima nzima huku ukibaki na viti vitupu na hakuna hata atakae ingia, ili matangazo yako yakae vyema basi huna budi kuliweka jina lake. Zote hizo ni baraka kwake.
Akakua na akahitaji mwenza, ni jambo zuri na wala si baya, akachagua, mara ya kwanza, Mrembo wa Tanzania, anaefanya vizuri kwenye tasnia ya filamu na ujasiriamali, Wema Abraham Sepetu, wengi tukapenda chaguo lake, tukapenda hadithi zao na tukapenda kujua hata hatma yao, pakaharibika. Si mbaya, kwani kosa si kosa bali kosa kurudia kosa. Ingawa hatukujua nini kilitokea.
Akafunga virago, akahama, sasa akahamia kwa mwingine, nae ni mrembo tu, na ni binti mtaratibu mwenye maadili, mwenye nyota na mafanikio kimuziki, kuitangazaji, urembo na hata ujasiriamali pia yumo, mrembo matata anayesemekana alikuwa wa mkali wa mpira wa mikono, Braza Hashimu, hii ni kutoka kwenye majarida kadhaa ya kibongo, huko nako hakukaa, akafungasha tena virago na kurudi kule kule kwa mwanzo alikokuacha, mara hii alirudi kwa pete na matangazo ya majukwaani, kwa mtoto wa Abraham. Ingawa tulishtuka ila tukasema si mbaya, kwani kujaribu ndo kubahatisha.
Aliporudia hakukaa, akahamia tena kwengine, na mara nyingi huwa haendi mbali, sasa akaenda kwengine, mtangazaji na mtu maarufu wa luninga mwenye umbo zuri, ambae mie binafsi sijui alimnyang’anya nani, tukasema wee tukanyamaza, na udaku wakaandika wee wakachoka. Bwana mkubwa hakujali, ila uko nako akahama.
Tulipouliza kwasasa yuko wapi, tukaambiwa karudi kulee kwa mwanzo, tena mara hii ikasemekana hataki tena ujinga, dhamira yake ni kuoa na kuweka ndani, yaani Mke na mume, na magazeti pia yakamnukuu kwa nukuu mbali mbali, nasi tukasema kaka kakua, ingawa wazee waliokuwa wakimbariki kipindi kile, sasa wakakaa kimyaa.
Kwa Yule tena keshafungasha na amehama tena, na sasa kavuka boda kabisa, kaenda kwa majirani zetu Uganda, kwa Binti wa watu mwenye chenji za kutosha, ambae inasemekana aliwahi kuolewa na bwana mmoja maarufu nchini humo na kubarikiwa watoto watatu, ila kwa sasa ameamua kutulia na bwana huyu wa kibongo, tayari buraza anatarajia kupata mtoto na shemeji yetu huyo.
Yote heri na yote ni maamuzi binafsi, ila imani yangu inaniambia mapenzi na yote yafanyikayo mapenzini ni siri ya wawili, sasa inakuaje mitandao yote inatapakaa picha zake za kudendeka laivu laivu na watoto wa watu? ambao wengine aidha ni watoto wa wazazi wenye kuheshimiwa katika jamii, au wengine ni mama za watoto wanaotarajiwa kukua na kuwa watu fulani katika jamii hii.
Sikatai kwamba kaka ni maarufu na kuandikwa kwake ni kawaida, sawa, ila inakuaje picha za siri ambazo naamini wakati wa kufanya haya wanakuwa wawili tu, halafu leo hi zinapamba magazeti na mitandao ya kijamii kwa fujo kiasi hiki! Ni makusudi au wanamnyatia? na kama ni hivyo basi ana bahati kweli ya kubambwa.
Je hii ni kweli haya yanatokea kwa kupangwa au ni kwa bahati mbaya tu?, kama haya hutokea kwa kupangwa basi kuna haja ya kufikiria mara mbili, ila kama kwa dhumuni maalumu pia inabidi tuliangalie kwa jicho la pili, kwani nachelea usije kuwapotosha wale woote wanaokuona wewe kama kioo cha jamii.
Hebu awafikirie wazazi wa watoto hawa wa kike, hebu awafikirie watoto wa mabinti hao, watoto ambao watakua na kukuta picha hizi za wazazi wao kwenye mitandao, hebu pia awafikirie wale ambao mwanzo nilisema kwamba walimkukubali na kusema “Mungu akuzidishie”, na nnahofia wasije badili dua zao zikawa mwiba. Awafikirie pia na washkaji wanaoumkubali kimuziki na kumuona yeye ndio kioo chao
Ila kaka pongezi kwa kazi nzuri iliyotoka hivi karibuni ambao sisi wote tumeikubali, iko tait kinyama, na tunaamini itabamba kitaani kwa muda mrefu kama kawaida yako, siku zote kaka hutoa vilivyo bora, big up! Na naamini itabamba chati zoote mama bongo
No comments:
Post a Comment