Mechi ya Yanga SC na Platnum FC iliyochezewa uwanja wa Taifa Dar
Yanga itaikabili Etoile baada ya miamba hao wa Tunisia kulazimisha sare ya 1-1 ugenini Angola dhidi ya Benfica jana na hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1 kufuatia ushindi wa 1-0 katika mechi yao ya kwanza.
Yanga watacheza dhidi ya Etoile katika wikiendi ya Aprili 17–19 hapa Tanzania na kurudiana ugenini kati ya Mei 1–3.
Kama Yanga itaing'oa Etoile, itaingia katika hatua ya 8-Bora, ambayo inafahamika pia kama "kapu" kwani timu 8 zilizotolewa katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika zitajumuika kwenye "kapu" hilo. Itachezeshwa droo na kila timu itapangiwa mpinzani wake mmoja, watacheza nyumbani na ugenini kwa ajili ya mtoano kusaka timu 8 za kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
Hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho inahusisha makundi mawili ya timu nne-nne, ambazo zitacheza nyumbani na ugenini kupata timu mbili kila kundi zitakazoingia nusu fainali na kisha timu mbili za fainali.
Yanga ilirejea nchini juzi usiku ikitokea Zimbabwe huku kocha wa timu hiyo, Mholanzi Hans van der Pluijm, akisema kwamba kikosi chake kinaahidi kufanya makubwa kwenye hatua ya 16-Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho wanayoshiriki.
Yanga imesonga mbele katika mashindano hayo ya kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-2, ikishinda 5-1 nyumbani Dar es Salaam kabla ya kulala 1-0 ugenini juzi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Pluijm alisema amefurahishwa na kitendo cha timu yake kusonga mbele na kiwango walichokionyesha kwenye mchezo wao wa juzi uliofanyika kwenye Uwanja wa Mandava uliopo Kilomita 200 kutoka mji wa Bulawayo licha ya kufungwa bao 1-0.
Pluijm alisema mechi za kimataifa ni dakika 180 lakini hakuna timu yenye uhakika wa kusonga mbele mpaka filimbi ya mwisho itakapopulizwa hata kama mechi ya kwanza ulipata ushindi mnono.
Alisema soka ni mchezo usiotabirika na wenye kutumia makosa ya mpinzani wao hunufaika, hivyo kila dakika ya mchezo ni muhimu kujipanga na kutotoa nafasi kwa timu nyingine kutawala.
"Ninafurahi kusonga mbele, kweli tumepoteza mchezo lakini timu yangu haikucheza hovyo, tulitengeneza nafasi ingawa hazikutumiwa vyema, tumeyaona makosa hivyo tutaendelea kuyafanyia kazi kwa ajili ya mechi zinazofuata, tuko tayari kucheza na yoyote itakayofuzu," alisema Pluijm.
Naye Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, alisema kuwa kikosi chao kinatarajia kuendelea na mazoezi leo jioni kwenye Uwanja wa Karume kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union ambayo itachezwa keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa.
Muro alisema baada ya timu kurejea nchini juzi saa saba usiku kwa ndege maalum ya serikali ambayo waliikodi, jana walipewa mapumziko na leo wataanza kujifua.
Alisema wachezaji wote 20 waliosafiri wamerejea jijini Dar es Salaam wakiwa wazima na wako tayari kuikaribisha Coastal Union.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment