ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 15, 2015

Kugombea urais Chadema Sh1 milioni


Viongozi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba (Ukawa)

Dar es Salaam. Mwanachama atakayetaka kuwania urais kwa tiketi ya Chadema atatakiwa kulipia Sh1,000,000 za fomu, ambazo atarejeshewa iwapo hatapitishwa kuwa mgombea pekee wa vyama vinavyoundwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), chama hicho cha upinzani kilisema jana.
Sera hiyo ya kurejesha fedha pia itahusu watu wengine watakaotaka kuwania ubunge na udiwani baada ya Chadema na vyama vingine vitatu vya upinzani, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD, kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya urais hadi udiwani.
Chama hicho kikuu cha upinzani pia kimeweka utaratibu wa wagombea ubunge kujitathmini iwapo kutakuwa na mgombea zaidi ya mmoja kwa kuwapa nafasi ya kujipigia kura kabla ya vikao vya uamuzi kutumia kura hiyo kama maoni yatakayosaidia kumteua mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema kwamba wagombea wa urais watachukua fomu makao makuu kuanzia Julai 20 na kuzirudisha Julai 25.
Pia, katika uchaguzi wa rais mwaka 2010, mgombea wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 2,271,941, ambazo ni sawa na asilimia 26.34 akiwa nyuma ya Rais Jakaya Kikwete aliyepata kura 5,276,827 sawa na asilimia 61.17.
Hadi sasa Dk Slaa hajatangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya Chadema na hakuna mwanachama aliyeonyesha nia hiyo.
Kuhusu  fomu za nafasi ya ubunge wa jimbo na ubunge wa viti maalumu, Mwalimu alisema zitatolewa kwa gharama ya Sh250,000, huku fomu za udiwani wa kata na wa viti maalumu zitagharimu kiasi cha Sh50,000 na fomu hizo watazichukulia kwa makatibu wa majimbo  na makao makuu ya chama hicho.
“Huu ni uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema,” alisema Mwalimu bila ya kufafanua vigezo walivyotumia kuweka viwango hivyo.
Hadi sasa Chadema inaongoza upinzani kwa kuwa na wabunge 45, kati yao 23 ni wa viti maalumu.
Mwalimu alisema kuwa wagombea wa nafasi za ubunge wataanza kuchukua fomu kuanzia Mei 18 na kuzirudisha Juni 25, wakati kwenye sehemu ambazo zina wabunge, kazi hiyo itaanza Julai 6 na kumalizika Julai 10, kipindi ambacho Bunge la 10 litakuwa limevunjwa.
Pia, alisema kwamba wagombea udiwani wataanza kuchukua fomu kuanzia Mei 18 na kuzirejesha Juni 25 na watazipata kwenye ofisi za makatibu wao wa kata za jimbo pamoja na wilaya husika.
 Mwalimu alitoa wito kwa wananchi ambao ni wanachama wa Chadema wenye sifa wajitokeze kuwania nafasi hizo na kwamba vyombo husika vitazingatia matakwa ya katiba ya chama hicho kwa kuwa lengo ni kupata wagombea waadilifu wenye uwezo wa kuwatumikia watu na wanaokubalika kwa wapigakura.
Kuhusu kurejeshewa fedha za kuchukulia fomu, Mwalimu alisema uamuzi huo utahusu wanachama watakaokuwa wamepitishwa na Chadema, lakini wakakosa kuteuliwa na Ukawa.
“Chadema itabeba jukumu la kumrejeshea pesa zake alizochukulia fomu ikiwa kwa bahati mbaya Ukawa itampitisha mwingine, lakini ikiwa yeye mwenyewe atasema zibaki kwa ajili ya maendeleo ya chama basi zitatumika  kwenye maendeleo,” alisema Mwalimu ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari.
“Kila mgombea atapewa nafasi ya kujieleza mbele ya wapigakura, atajieleza kwa dakika tano na ataulizwa maswali yasiyozidi matatu kutoka kwa washiriki na kura zitakazopigwa baada ya wagombea wote kujieleza mbele ya mkutano maalumu,” alisema. Aliongeza kuwa kila mgombea atakuwa na haki ya kuweka wakala wa kuhesabu kura zake.
Akizungumzia utaratibu wa kuwapata wagombea, Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri  Kuu ya Chadema, John Mrema alisema wagombea wote watapewa fursa ndani ya mkutano maalumu kujipigia kura.

“Kila mgombea atatakiwa apige kura mara tatu iwapo kutakuwa na mgombea zaidi ya mmoja, moja itakuwa yake binafsi na kura nyingine atatakiwa kumpigia mgombea mwingine anayeona anafaa kati ya waliojitokeza,” alisema Mrema.
Mwananchi

No comments: