ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 4, 2015

MAALIM SEIF ADAHAMINIWA TENA KUGOMBEA URAIS

 Mwenyekiti wa CUF zoni ya Mjini Unguja Massoud Khamis, akimkabidhi fedha taslim Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, ili aweze kuchukua fomu ya kugombea urais wa Zanzibar wakati utakapofika.
  Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akionyesha fedha alizokabidhiwa kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea urais.
  Mwenyekiti wa CUF zoni ya Mjini Unguja Massoud Khamis, akimkabidhi Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, cheti cha heshima kutokana na uongozi wake.
Baadhi ya viongozi na wanachama wa CUF waliojitokeza katika hafla ya kumkabidhi fedha Maalim Seif iliyofanyika nyumbani kwake Mbweni. (Picha na Salmin Said, OMKR)

Na: Hassan Hamad (OMKR)

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amethibitisha nia yake ya kugombea tena nafasi ya Urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza katika hafla iliyoandaliwa na kamati maalum ya (CUF) Zoni ya Mjini iliyokwenda kumdhamini kugombea nafasi hiyo huko nyumbani kwake Mbweni, Maalim Seif amesema anatarajia kugombea tena nafasi hiyo ili aweze kutimiza ndoto yake ya kuwatumikia wananchi.

Kamati hiyo ya CUF Zoni ya Mjini imemdhamini Maalim Seif kwa fedha taslim shilingi milioni mbili na laki tano, ili iweze kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar wakati utakapofika.

Maalim Seif ameishukuru kamati hiyo kwa uamuzi wa busara waliochukua, hali inayoonyesha kuwa wananchi wa Zanzibar wanaendelea kuwa na imani naye kutokana na mwelekeo wake wa kutaka kuleta mabadiliko ya kweli kwa Zanzibar.

Amesema iwapo wananchi watakipa ridhaa Chama hicho kuongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu,  kitatandika misingi imara ya utawala bora, uchumi na kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi.

Ameyataja mambo mengine ya msingi kuwa ni pamoja na kurejesha heshima ya Zanzibar katika jamii ya Kimataifa, kuimarisha huduma za kijamii ziliwemo afya na elimu, pamoja kuandaa mazingira ya kuongeza ajira kwa vijana.

Amesema tofauti na chaguzi zilizopita, Chama hicho kimejiandaa vizuri kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao, na kuwaomba wananchi waendelee kukiunga mkono ili kiweze kupata ushindi mkubwa na kuweza kuongoza serikali.

Mapema akisoma risala ya kamati maalum ya (CUF) zoni ya mjini, mjumbe wa kamati hiyo Bw. Salim Abdallah Salim amesema wameamua kumdhamini Maalim Seif kutokana na utendaji wake ndani ya chama hicho pamoja na matumaini aliyonayo kwa Wazanzibari.

Aidha kamati hiyo imetoa tamko rasmi la kumuunga mkono Maalim Seif kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar wakati utakapofika, na kutoa wito kwa vijana kutafuta vitambulisho vya Mzanzibar Mkaazi (ZAN ID) na kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura, ili waweze kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao

1 comment:

Anonymous said...

Walu Pes ya Kununua Kahawa au Kigoda cha kukalia maana Mwezi october "He is Offically Retiring"