ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 4, 2015

Mgomo tena, Madereva wasema leo hakuna basi barabarani nchi nzima

Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta.

Takribani siku 22 zikiwa zimepita tangu madereva wagome kutoa huduma za usafiri nchi nzima, leo wametangaza mgomo mwingine kutokana na ukimya dhidi ya madai yao kwa serikali.

Madereva hao jana walitoa tamko la kuwapo kwa mgomo huo kupitia vyama vyao, huku wakikanusha kwamba watagoma sambamba na kuandamana.

Walisema leo watakuwa kwenye ofisi zao za muungano wao zilizopo Ubungo, jijini Dar es Salaam na hawatatoa huduma za usafiri.

Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu wa Umoja wa Madereva na Chama cha Malori, Rashid Salehe, alisema, mgomo upo pale pale kwa madai kuwa bado kuna mambo ambayo yameendelea kuwa kikwazo kwao.

Alisema iwapo serikali haitatoa majibu ya kuridhisha, leo hawataingia barabarani kutoa huduma za usafiri.

Alisema jana walifanya mkutano wa madereva jijini Dar es Salaam huku ajenda kubwa ikihusu mgomo huo.

Alitaja baadhi ya sababu zinazowafanya wagome kwa mara nyingine kuwa ni serikali kutotekeleza madai yao likiwamo la kupewa ajira rasmi na waajiri wao.

“Msimamo wetu upo palepale kwamba kesho (leo) hatutaendesha magari..madereva wanaambiwa wezi, tunataka mikataba iboreshwe…tutakaa hapa hata ndani ya siku saba hadi serikali ije na kutoa majibu yanayoridhisha. Tunataka tupatiwe mikataba inayoeleweka na waajiri wetu mbele ya serikali,” alisema na kuongeza:

“Tumekaa katika kikao cha leo (jana) kwa ajili ya kuangalia maazimio ya kikao tulichokaa Aprili 29, mwaka huu…katika kikao hicho zaidi ya madereva 40 walisema hawana hela.”

TABOA WAIPA
ANGALIZO SERIKALI
Katibu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Enea Mrutu, alisema walipata taarifa zote kuhusu mgomo huo na kueleza kwamba wanaotangaza mgomo huo siyo madereva walioajiriwa.

Kwa mujibu wa Mrutu, madereva hao ndiyo waliosababisha magari yao kutoingia barabarani Aprili 11, mwaka huu na kuitaka serikali kuingilia kati suala hilo, vinginevyo leo magari hayataweza kuingia barabarani.

DARCOBOA: MGOMO
UWE WA HIARI
Mwenyekiti wa Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), Sabri Mabrouk, alisema chama hicho kina taarifa kuhusu mgomo huo, lakini akaeleza kusikitishwa kwake kwa namna madereva wa vyombo vya usafiri wanavyowahusisha wao akisema hawahusiki.

Kutokana na hilo, Mabrouk aliomba mgomo huo usiwe wa lazima bali wa hiyari kwani si vyema kuwahusisha wao wanaohusika na daladala tena ndani ya mkoa na kupewa vitisho vya kupigwa mawe endapo gari lolote litakaidi agizo hilo.

“Serikali iangalie suala hili, kama kuna jambo lipo nyuma ya pazia basi liwekwe wazi….kama ni wa mikoani kwa nini wanatuhusisha sisi, tusitafute kuwasumubua wananchi,” alisema mwenyekiti huyo wa Tarcoboa.

SUMATRA: WANANCHI WATASUMBULIWA
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchikavu na Majini (Sumatra), Gilliard Ngewe, alisema, suala hilo lipo katika wizara husika na kwamba kufanyika kwa mgomo huo kutaathiri wananchi kutokana na kukosa huduma za usafiri.

Hata hivyo, gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta (pichani), bila mafanikio kutokana na simu yake kutopatikana, huku Naibu wake, Charles Tizeba, akisema: “Naomba mnitafute kesho..nipo msibani.”

NIPASHE pia lilimtafuta Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka na Naibu wake, Makongoro Mahanga, lakini simu zao hazikuwa hewani.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, alikaririwa na vyombo vya habari juzi akisema amepokea ujumbe mfupi wa simu kwamba leo kuna mgomo.

Tishio la mgomo wa leo ni mwendelezo wa mgomo mwingine mkubwa ambao ulidumu kwa takribani saa saba kwa mabasi kutokuruhusiwa kutoka katika kituo kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi cha Ubungo, Aprili 11, mwaka huu.

Madai ya mgomo huo ambao ulileta adha kubwa kwa wananchi yalikuwa ni kupinga ucheleweshwaji wa malori kwenye mipaka hususani ya Tunduma ambako hukaa kwa zaidi ya siku 26 licha ya kulipiwa kila kitu bandarini.

Mengine ni kupinga sheria namba G 31 ya mwaka 2015 ambayo inazungumzia faini ya Sh. 300,000 au kifungo cha miezi 21 kwa madereva wanapofanya makosa barabarani. Pia kupinga madereva kutakiwa kwenda Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kila baada ya miaka mitatu kwa ajili ya kujinoa.

Madai mengine yalikuwa ni wamiliki wa magari kutowashirikisha madereva katika mikataba yao ya kazi.
Hata hivyo, mgomo huo ulisitishwa baada ya serikali kupitia kwa Waziri Kabaka kufuta sharti la kwenda chuoni kila baada ya miaka mitatu.

Pia aliahidi kulipatia ufumbuzi suala la mikataba yao katika kikao kilichotarajiwa kufanyika wiki iliyofuata.
CHANZO: NIPASHE

No comments: