Waandamanaji wakionesha msimamo wao wa kumtaka Rais Pierre Nkurunziza kutogombea tena nafasi hiyo muhula ujao.
Bujumbura, Burundi
Polisi mjini Bujumbura leo wamefyatua za moto hewani katika kukabiliana na maandamano mapya ambayo yameanza maeneo kadhaa ya mji huo.
Makundi mbalimbali ya vijana yaliweka vizuizi barabarani huku wakiimba nyimbo za kumtaka Rais Pierre Nkurunziza abadili msimamo wake wa kutaka kugombea awamu ya tatu ya Urais nchini humo.
Maandamano hayo yameanza siku chache baada ya kushindwa kwa jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali ya Nkurunzinza.
Wanahabari walishuhudia wanajeshi wakifyatua risasi za moto kwa waandamanaji walioonekana wakikimbia na kusambaa barabarani.
Biashara kadhaa zilifungwa na shughuli za kawaida kukwama katika maeneo ya Nyakabiga, Musaga na Mutakura mjini Bujumbura.
Mpaka sasa hakuna habari zo zote zilitolewa kuhusiana na waliouawa au kujeruhiwa kutokana na vurugu hizo za maandamano.
Hata hivyo maeneo anakoungwa mkono Rais Nkurunzunza na katikati ya mji shughuli ziliendelea kama kawaida.
Waandamanaji waliviambia vyombo vya habari kuwa wanapinga uamuzi wa Rais Nkurunziza kukugombea awamu ya tatu uongozini.
Jana kiongozi huyo wa Burundi alijitokeza hadharani kwa mara ya kwanza mbele ya vyombo vya habari vya kimataifa lakini hakusema lo lote kuhusiana na hali ya wasiwasi inayokumba taifa lake.
Rais Nkurunzinza aliyerudi nchini Burundi Alhamisi jioni aliwambia waandishi wa habari kuwa Burundi inakabiliwa na vitisho kutoka kwa kundi la magaidi walioko nchini Somalia la Al Shaabab.
Wakati huo huo ubalozi wa Marekani nchini Burundi umefungwa na taarifa zilitolewa zikiwaomba wafanyakazi wake ambao hawashughulikii maswala ya dharura na familia zao waondoke nchini kwa sababu ya kuendelea kuzorota kwa uchumi.
BBC
No comments:
Post a Comment