ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 26, 2015

CCM wamkataa Maalim Seif barazani, Ni kulipiza CUF kususia Baraza.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Mgogoro wa kisiasa Zanzibar umeingia katika hatua nyingine baada ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukataa hoja ya Spika wa baraza hilo ya kumwalika Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, kuhudhuria kuvunjwa kwa baraza hilo leo.

Hali hiyo inaashiria kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaiaf (SUK) iliyoundwa na Chama cha Wananchi (CUF) na CCM baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 imepata majaribu.

Awali akitoa taarifa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi jana, Spika wa baraza hilo, Pandu Ameri Kificho, aliwataarifu wajumbe hao kuwa wakati wa kuvunjwa kwa baraza hilo wageni watatu wanatarajiwa kuhudhuria akiwamo Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif na mlinzi wa rais.

Hata hivyo, Kificho alisema wajumbe wa baraza hilo ndiyo wenye mamlaka ya kukubali au kukataa wageni hao kuhudhuria na kutaka idhini yao.

Spika huyo alipowauliza wajumbe hao kama wanakubaliana na ujio wa wageni hao, wajumbe hao kwa kauli moja walimjibu kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na mlinzi wa Rais wa Zanzibar wanamruhusu kuingia lakini walikataa Makamu wa Kwanza wa Rais (Maalim Seif) asiingie katika kikao hicho.

SPIKA: Ndugu wajumbe wageni wetu wakuu kesho (leo) ni watatu na tayari nimeshawapelekea barua ya kuwaalika kuhudhuria katika ufungaji wa kikao hiki, nataka kauli zenu vipi bodigadi wa rais mnamruhusu?.

WAJUMBE: Ndiyooo
SPIKA: Je?, Jaji Mkuu wa Zanzibar mnamruhusu?
WAJUMBE: ndiyoooo
SPIKA: Mgeni wetu mwengine ni Makamu wa Kwanza wa Rais vipi mnamruhusu?
WAJUMBE: Hatumtaki.
Spika Kificho alirudia kuuliza mara tatu swali hilo lakini majibu ya wajumbe mara zote yalikuwa ni hayohayo ya kumkataa Maalim Seif kuhudhuria.

Kufuatia hali hiyo, Kificho aliwaambia wajumbe hao kama hawataki Makamu wa Kwanza wa Rais kuhudhuria kikao hicho kwa kuwa alishamwandikia barua ya mwaliko itabidi amwandikie tena barua ya kumtaarifu kongozi huyo kuwa asihudhurie kikao hicho kutokana na wajumbe wa baraza hilo kukataa ujio wake.

Baadhi ya wajumbe wa CCM wakizungumza na NIPASHE, walieleza sababu za kukataa Maalim Seif kuhudhuria shughuli hiyo.

Kaimu Mnadhimu wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka CCM, Ali Salum Haji, alisema wana sababu za msingi kukataa Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF kuhudhuria kikao hicho, ikiwamo kuwa yeye ni kiongozi wa upinzani lakini wajumbe wake na mawaziri wa chama chake wamesusia baraza hilo.

“Kama baba una watoto na watoto wakakukataa utakuwa peke yako, kwa hiyo tumeamua na yeye aendelee na msimamo wa wajumbe wa chama chake ambao wamegoma,” alisema Salum ambaye pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Kwahani (CCM).

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Muhammed Aboud, alisema uamuzi wa wajumbe wa baraza hilo kukataa Makamu wa Kwanza wa Rais kuhudhuria kikao hicho unatokana na hatua ya wajumbe wa CUF kugoma kuwamo katika baraza hilo kujenga nchi.

“Kauli ya wajumbe wa CCM kukataa Maalim Seif asihudhurie huo ni ujumbe kuwa walichokifanya wajumbe wa CUF siyo sahihi na hatma yake italeta mpasuko mkubwa katika nchi yetu” alisema Aboud.

Alishauri kuwa ni vyema viongozi wa CUF wanapoamua kuigomea serikali kufikiria kwanza kabla ya kutenda, kwani kitendo walichokifanya siyo kizuri na hawapaswi kukifanya tena kwani kinaweza kusababisha mpasuko mkubwa katika nchi.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alisema hatua hiyo ya wajumbe wa CUF imesababisha mpasuko kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoundwa na CCM na CUF, hasa kitendo walichofanya mawaziri wa chama hicho cha upinzani ambao nao ni miongoni mwa viongozi katika serikali hiyo.

Alisema kitendo walichokifanya wajumbe wa CCM kukataa Maalim Seif kuhudhuria kikao hicho kimefuata kanuni za baraza hilo.
“Wajumbe wameona kukubali Makamu wa Kwanza wa Rais kuhudhuria kikao hicho wakati hakuna waziri hata mmoja kutoka katika chama chake atakaa kwa misingi ipi,” alisema na kuongeza:

“Kitendo walichokifanya wajumbe wa CUF hasa mawaziri ni kibaya sana na wamevunja kanuni na sheria za baraza na sheria za nchi na mawaziri hao walipaswa kujiuzulu kutokana na kitendo hicho,” alisema Balozi Iddi.

Alisema tangu waliposusia muswada wa sheria wa kuidhinisha matumizi ya fedha za bajeti ya serikali, mawaziri hao walipaswa kuandika barua ya kujiuzulu kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi, lakini ameshangazwa hadi sasa hawajapeleka barua hizo kwa Rais wa Zanzibar.

Alisema mwenye uamuzi wa kuwachukulia hatua mawaziri hao waliogomea kikao cha baraza hilo ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa mujibu wa sheria na kanuni za nchi zinazompa mamlaka hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji, alisema bado wanaendelea na msimamo wao wa kutohudhuria kikao hicho kutokana na wenzao wa CCM na mawaziri wa chama hicho kuvunja sheria na kanuni za nchi ikiwamo kuwaandikisha watu wasiokuwa na sifa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.

“Sisi tumeapa kulinda katiba na sheria za nchi na kitendo cha kutoka katika baraza hatujavunja sheria wala katiba na wala hatuna mpango wa kujiuzulu,” alisema Duni ambaye pia ni Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano.

Alisema kitendo cha wajumbe wa CCM kumkatalia Makamu wa Kwanza wa Rais kuhudhuria kikao hicho kinaonyesha hawataki maridhiano katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa hasa ikizingatiwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais ni mshauri wa Rais wa Zanzibar,” alisema Duni.

Msaidizi wa Maalim Seif, Masoud Said na Katibu wake, Issa Heri, walipotafutwa kuzungumzia suala hilo, simu zao zilikuwa zinaita bila kupokelewa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: