Jeshi la Polisi, Uwanja
wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNAI), linamshikilia, raia wa Kuwait,
Hussein Mansoor, kwa kukutwa na kobe hai 173 aliokuwa akiwasafirisha kueleka
nchini kwake.
Kaimu Mkurugenzi wa Uwanja wa JNIA, Clemence
Jingu alisema abiria huyo mwenye hati ya kusafiria yenye namba 003870237,
alikamatwa usiku wa kuamkia jana akijitayarisha kupanda ndege ya Emirates
iliyokuwa ikielekea Kuwait kupitia Dubai.
Jingu alisema raia huyo alikamatwa saa tano
usiku katika eneo la abiria wanaoondoka, baada ya polisi wa JNIA kwa
kushirikiana na maofisa wa Wizara ya Maliasili kufanya ukaguzi na kugundua kobe
hao wakiwa wamefichwa kwenye masanduku makubwa mawili.
“Hii ni moja ya kazi kubwa ambazo tunazifanya
kwa sasa hapa JNIA, ila tutahakikisha kuwa hakuna nyara za Serikali
zitakazotaifishwa na kupitishwa hapa kwa kuwa tumeimarisha ulinzi maradufu,”
alisema Jingu.
Jingu alisema kobe hao wenye thamani ya Sh 30
milioni ni miongoni mwa nyara muhimu za Serikali ambazo zimekuwa zikitaifishwa
kupitia mbinu mbalimbali.
“Pamoja na kuimarisha ulinzi, lakini
tutahakikisha JNIA inakuwa bora kuliko viwanja vingine vya Afrika Mashariki na
zaidi hasa kuhakikisha ulinzi unapewa kipaumbele” alisema.
Kamanda wa Polisi wa JNIA, Khamis Suleiman,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mtuhumiwa huyo anashikiliwa
na jeshi hilo kwa uchunguzi zaidi.
Tukio hilo lilithibitishwa pia na Kamishna wa
Interpol, Tawi la Tanzania, Gustav Babile ambaye alisema raia huyo alikamatwa
na wanyama hao huku akiwa na vibali halali.
Mmoja wa wafanyakazi wa JNIA (jina
linahifadhiwa) alisema kabla ya kukamatwa, ilionekana kuna mpango umefanywa ili
kumpitisha raia huyo bila kugundulika kwani taa za eneo la ukaguzi zilizimwa
kwa saa kadhaa uwanjani hapo.
“Si kawaida taa kuzimwa lakini wakati yeye
anapita taa zilizima jambo linaloonyesha kuwa ni njama zilizopangwa lakini hata
hivyo hazikufanikiwa,” kilisema chanzo hicho.
Kadhalika chanzo hicho kilisema raia huyo
aligunduliwa na askari wa maliasili akiwa tayari ameshapita katika vizuizi
vyote vya ukaguzi na ameshaingia katika eneo la abiria wanaoondoka.
Tukio hili linafanana kwa kiasi kikubwa na lile
lililotokea Januari 8, mwaka huu, ambapo raia mwingine wa Kuwait, Ahmed Ally
Mansour alikamatwa uwanja wa JNIA akiwatorosha kenge hai 149 wenye thamani ya
Sh 6.3 milioni.
Kama ilivyo kwa tukio la jana, hata tukio la
Januari lilitokea saa tano, likihusisha ndege ile ile huku watuhumiwa wakiwa na
ubini unaolandana.
Kadhalika, Julai 31 mwaka jana, raia wa
Vietnam, Dong Van (47) naye alikamatwa uwanjani hapo akiwa na meno 65 na kucha
447.
CHANZO: MWANANCHI
3 comments:
Hao kobe si tayari walikuwa wamenunuliwa kutoka serikalini; yaani, vitalu viliuzwa kwa watu binafsi. Sasa mnamlili nani na ninyi milishauza vitalu. Kwani kitalu ni jina au tembo na kobe waliomo ndani yake. Vitalu ni vyangu; tembo na kobe mimi nitawafanyia nini kam sio kuwauza nchi za nje?
Hao kobe si tayari walikuwa wamenunuliwa kutoka serikalini; yaani, vitalu viliuzwa kwa watu binafsi. Sasa mnamlili nani na ninyi milishauza vitalu. Kwani kitalu ni jina au tembo na kobe waliomo ndani yake. Vitalu ni vyangu; tembo na kobe mimi nitawafanyia nini kam sio kuwauza nchi za nje?
Who is this anonymous? saying stating about "vitalu" vilivyonunuliwa? na nani? hati ipo kuthibitisha? Muuzaji wa vitalu hivyo ni nani? Je ni Serikali? vithibitisho? Vitalu hivyo vilivyouzwa ni eneo gani ambalo linaweza kuwa na "Nyara za Serikali" bila ya Serikali yenyewe kujua ama UMMA wa Watanzania ? Hatua gani zitafuata baada ya huyo raia wa Kuwait kukamatwa? Je, atashtakiwa mahakamani?
Post a Comment