ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 12, 2015

Siro Atoa Ushahidi Kesi ya Profesa Lipumba


MKUU wa Operesheni Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Simon Siro (54) ametoa ushahidi katika kesi inayowakabili Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na wafuasi wake 30 na kudai mkutano huo ulipigwa marufuku kutokana na taarifa za intelijensia za kuwapo kwa tishio la ugaidi.
Siro aliyaeleza hayo juzi mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Cyprian Mkeha, akiwa shahidi wa upande wa mashtaka.


Alidai Januari 23 mwaka huu walipokea barua ya CUF ikiiarifu polisi kuwa Januari 27 mwaka huu wangefanya mkutano na maandamano yenye lengo la kukumbuka watu waliouawa Pemba na kulaani mauaji hayo.


Siro alisema barua hiyo ya CUF ilidai kuwa chama hicho kimekuwa na tabia ya kuwakumbuka watu waliouawa na kuyalaani mauaji hayo kila mwaka, Januari 27.


“Tuliipokea barua hiyo ya CUF Januari 23, 2015 na Januari 24 na 25, timu ya intelejensia ilifanya kazi kuona kama yanaweza kufanyika na kumalizika kwa usalama,” alisema Siro.


Alidai kuwa taarifa hizo za intelejensia zilieleza kuwa lilikuwapo tukio la ugaidi lililokuwa limelenga maandamano hayo.

Siro alidai pia kuwa kwa kipindi kile yalikuwapo matukio ya unyang’anyi wa silaha katika vituo mbalimbali vya polisi na kwa sababu hiyo jeshi la polisi liliyazuia maandamano na mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika, kwa mujibu wa sheria inayoruhusu kufanya hivyo.


Alidai polisi hawakuyaruhusu maandamano hayo ya Januari 27, 2001 na yalikuwa haramu na hata waliouawa hawakuwa wanachama wa CUF pekee bali hata polisi walikuwamo.


Alidai jeshi hilo liliandika barua ya kuyapinga yasifanyike na kumkabidhi Abdul Kambaya kwa niaba ya Katibu wa CUF na walikubaliana kuwa maandamano na mkutano hautakuwapo.


“Niliamini kuwa makubalino tuliyofanya Januari 26 yangetekelezwa lakini Januari 27 majira ya saa 8.00 nilipigiwa simu na Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Kamishna Zakaria ambaye aliniambia kuwa walikuwapo watu wengi wenye mabango katika ofisi ya CUF wilaya ya Temeke.


“Nilimwambia awaite viongozi waliopo azungumze nao kwa sababu tayari walikuwa na barua ya katazo lakini baada ya dakika 20 alinipigia simu kuwa wamekaidi na nilimjibu kuwa sheria ichukue mkondo wake,”alieleza Siro.

Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea Julai 9 na kusikilizwa kwa siku tatu mfululizo, Julai 29,30 na 31 ambako upande wa mashtaka umeahidi kuwasilisha mashahidi wengine sita katika siku hizo.


Tukio la viongozi hao kukamatwa lilitokea Januri 27 mwaka huu wakati Profesa Lipumba na viongozi wenzake walipokamatwa kwa kuitisha mkutano wa hadhara kuadhimisha miaka 14 tangu wafuasi wa chama hicho kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati wakiandamana kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais wa Zanzibar mwaka 2001.

Maandamano hayo ya Januari 27, mwaka huu yalianzia katika ofisi za CUF Temeke yakiongozwa na Lipumba kuelekea viwanja vya Zakhem kwa ajili ya mkutano wa hadhara.

1 comment:

Anonymous said...

Mbona TZ haibadiliki...kila 7chaguzi huyu Lipumba lazima awe na Kesi ya kufanya ashindwe kuwin au ndiyo njama