ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 26, 2015

Wagombea urais CCM wagonga 40

Kada wa CCM, Helena Elinawinga akionyesha begi lenye fomu za kuomba kugombea kiti cha Urais kupitia chama cha CCM, baada ya kukabidhiwa jana katika makao makuu ya chama hicho, mjini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi

Dodoma/Dar. Mtafiti binafsi na kada wa CCM, Helena Elinawinga (41), amejitokeza kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama chake kuwania urais na kusema amefikia uamuzi huo ili kupunguza kujirudiarudia kwa adhabu za vifo kwa viongozi.
Helena anakuwa kada wa 40 wa CCM kuomba ridhaa ya chama hicho kuteuliwa kupeperusha bendera yake katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Kada huyo ni mwanamke wa sita kuchukua fomu za kuomba kuwania nafasi hiyo katika chama hicho akitanguliwa na Balozi Amina Salum Ali, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk Mwele Malecela, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro, Monica Mbega na Ritta Ngowi.
Helena alifika katika ofisi za Makao Makuu ya CCM saa saba mchana akiwa ndani ya bajaji lakini tofauti na wenzake, akiwa amevalia shati la rangi ya zambarau, suruali nyeusi na kofia yenye rangi za Taifa.
Akiwa na Katibu wa Oganaizesheni, Muhammed Seif Khatib, kada huyo ambaye pia hakuwa na wapambe kama ilivyo kwa wagombea wengine, alikataa ombi la wapigapicha kuvua kofia. “...nitawaambia kitu kizuri baadaye kwa nini sitaki kuvua hii kofia,” alisema huku Khatib akiwasihi waandishi kutoendelea kumtaka avue au asogeze kofia hadi atakapomaliza kuchukua fomu.
Aidha, wakati akichukua fomu hiyo, kada huyo ambaye mkononi alikuwa amebeba begi lililotengenezwa kwa kitambaa cha nguo aina ya batiki, alilazimisha kupigwa picha pamoja na bango lake huku akisisitiza umuhimu wa picha hiyo kupigwa hata kabla ya kumaliza shughuli ya kukabidhiwa fomu.
Bango hilo, licha ya kuwa na maneno ambayo yalikuwa hayaeleweki vizuri na michoro ya watu waliovalia mavazi ya kifalme, moja lilionyesha akiwa amebeba mizani inayotumiwa na mahakama kuonyesha usawa wa sheria na mkono mwingine akiwa amebeba jambia. Bango hilo pia lilikuwa na gari aina ya shangingi, picha za marais wa zamani wa Liberia, Charles Taylor, Mohammed Morsi wa Misri na wanawake wengine wawili ambao hawakufahamika.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu hiyo, huku akicheka, Helena alisema: “Nilikataa kuvua kofia kwa sababu sikuchana nywele.”
Kuhusu kutovaa sare za CCM, Helena alisema aliwaambia viongozi wa chama chake kuwa wanatakiwa kufanya mafunzo ya pamoja ya wagombea wote ili kuelewa hadhi ya sare. Alipoulizwa kama siku saba zitamtosha kukusanya wadhamini katika mikoa 15 alisema; “Huwezi kujua nini kitatokea kama utakuwa hai au utakufa.”

Helena ni nani?
Alizaliwa Desemba 31 mwaka 1974, Dar es Salaam na kusoma shule tatu za msingi tofauti mkoani Arusha na Kilimanjaro. Alijiunga na Shule ya Sekondari Weruweru ya Kilimanjaro na baadaye Chuo Kikuu cha Marekani katika Shule ya Masomo ya Kimataifa na kutunukiwa Shahada ya Siasa ya Mazingira na Uchumi.
Hivi sasa anafanya utafiti wa jinsi vijana wanavyoweza kujiajiri wakimaliza vyuo akishirikiana na Chuo cha Mwalimu Nyerere Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Sokoine Morogoro.

Lowassa avunja rekodi ya Mbeya
Zaidi ya wana CCM 120,000 walijitokeza juzi kumdhamini Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jijini Arusha na kuvunja rekodi ya Mkoa wa Mbeya alikodhaminiwa na zaidi ya wanachama 58,000.
Shughuli ya kumdhamini Lowassa zilizofanyika katika Viwanja vya Msikiti Mkuu wa Ijumaa (zamani bustani ya Mashujaa), ilimalizika saa 10.47 jioni, licha ya maandalizi yake kuanza tangu saa nne asubuhi kwa burudani za nyimbo za hamasa za CCM. Lowassa aliwasili uwanjani hapo Saa 10.07 jioni.

Muhongo, Mulenda wamaliza kazi
Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amerejesha fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania urais na kutaka wanaomhusisha na sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, kuhojiwa kama tatizo ni urais.
Akizungumza jana baada ya kurejesha fomu, Profesa Muhongo alisema hana haja ya kuzisemea tuhuma hizo kwa kuwa hakuna chombo ambacho kimemtaja kuhusika.
“Waliokuwa wamelisuka waende walitolee maelezo. Ripoti ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) jina langu halipo,” alisema Profesa Muhongo.
Aliwataka Watanzania kusoma taarifa za mabenki ambazo zinaonyesha watu waliogawana fedha hizo na kwamba jina lake halipo. “Sikuitwa na Kamati ya Maadili ya Viongozi wa Umma, sasa nizungumzie nini? Takukuru sikuitwa nieleze nini?” alihoji.
Katika makabidhiano hayo, Profesa Muhongo pia alimkabidhi Khatib CD 15 zenye orodha ya wadhamini, picha na maoni ya kila mdhamini katika mikoa yote.
Pia, alikabidhi ramani ya maeneo aliyozunguka kusaka wadhamini.
Alisema Watanzania hawatafuti mtu wa kujaza nafasi ya urais ila ambaye anaweza kufanya mapinduzi yatakayowatoa katika umaskini na kwamba mtu sahihi ni yeye.
Aidha, Mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali la Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Jamii (EGSOF), Leonce Mulenda, amerudisha fomu na kusema amepokewa vyema katika mikoa yote aliyokwenda kutafuta wadhamini.

Makongoro amkubali Profesa Lipumba
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere ameunga mkono kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akisema baadhi ya wagombea wenzake hawapaswi kuwa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa vile siyo wasafi na wangetupwa jela kutumikia vifungo.
Juni 14 mwaka huu, Profesa Lipumba, wakati akichukua fomu kuwania urais kupitia CUF ili apendekezwe na Ukawa, alionyesha kushangazwa na utitiri wa wagombea ndani ya CCM akisema baadhi yao walipaswa kuwa gerezani wakitumikia kifungo kutokana na kuhusika katika kashfa mbalimbali za ufisadi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana baada ya kumaliza kazi ya kukusanya wadhamini, Makongoro alisema kuwa kamwe hawezi kuwa rafiki na mafisadi.
Alisema walarushwa na mafisadi katika CCM ndio wanaofanya baadhi ya wanachama wa chama hicho wenye sifa, kukosa nafasi za uongozi.
“Mimi siyo mnafiki, naungana na kauli hii aliyoitoa kaka yangu Ibra... si mnamjua Ibra...?” alisema Makongoro.


Dk Mwele azoa wanawake
Wanawake jijini Dar es Salaam wamejitokeza kwa wingi kumdhamini Dk Mwele Malecela, anayeomba kuteuliwa na CCM kuwania urais.
Katibu wa CCM Wilaya ya Temeke, Robert Kerenge alisema mgombea huyo ni wa 11 kuomba udhamini katika ofisi yake, lakini alishangaa kuona idadi kubwa ya wanachama waliojitokeza kumdhamini tofauti na ilivyokuwa kwa wagombea wengine.
Mwananchi

No comments: