MAKAMBA
Na Saleh Ally
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), kiko katika harakati za mwisho kumpata mgombea wake wa urais na leo ndiyo tatu bora inajulikana.
Tayari tano bora imeishajulikana ambayo ni Benard Membe, Asha-Rose Migiro, Januari Makamba, John Magufuri na Amina Ally.
Mgombea mmoja atatangazwa kesho na kitendawili cha nani atakuwa mgombea wa urais wa chama hicho kikongwe nchini kitakuwa kimetenguliwa, huenda itakuwa wakati wa kupongezana na kufutana machozi.
Hayo tuwaachie wao wanasiasa, lakini si vibaya kuwagusa leo kwa kuwa wenyewe waliamua kuingia katika anga zetu.
Huenda nitakaowagusa wakiwemo waliopigwa chini kwenye tano bora, tatu bora na mwisho mgombea huyo mmoja.
Lakini nimeona si vibaya kuwakumbusha kuhusiana na walichosema baada ya kuwa wametangaza nia ya kugombea urais kupitia CCM.
PINDAAsilimia kubwa ya wagombea ukimtoa John Magufuli ndiyo sikuwasikia wakizungumzia masuala ya michezo. Waliobaki kwa asilimia kubwa, walizungumza, lakini mwisho waliigusa michezo.
Nilimsikia Januari Makamba akijisifia sasa Tanga ina timu tatu za Ligi Kuu Bara, yaani Coastal Union, Mgambo na wakongwe African Sports ambao wamerejea.
Edward Lowassa wakati akizindua kampeni zake, naye aliizungumzia michezo akidai akipata nafasi ya kuiwakilisha CCM, akagombea basi michezo itapewa kipaumbele na kuna mipango lukuki.
Hali kadhalika, Benard Membe, Sospeter Muhongo, Lazaro Nyalandu na wengine.
LOWASSA
Kweli wapo ambao nawajua walioonyesha angalau ushiriki wao michezoni kama Fredrick Sumaye, Samuel Sitta, Mwigulu Nchemba lakini bado ninaweza kusema hawakuwa ‘sirias’ katika suala hilo hadi unaweza kusema walikuwa na msaada mkubwa.
Makamu wa Rais, Dk Mohammed Ghalib Bilal na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambao wamekuwa madarakani kwa muda wote, ninaweza kusema michezo hawakuijali kabisa kwa kubwa ni nadra kweli kusikia hata wakizungumzia maendeleo yake.
MEMBEMembe alionyesha juhudi kidogo ambazo unaweza kusema kulikuwa na mwanga baada ya kuwaweka wachezaji wa Tanzania kambini nje ya nchi ili kujiandaa na Michezo ya Olimpiki kwa upande wa riadha na soka.
Kwa kundi lote hili, unaposikia mmojammoja anazungumzia michezo, hakuna ubishi nachukulia kama ni maneno ya ulaghai kwa kuwa si watu wenye mapenzi na michezo na hawaijali.
Huenda inakuwa ni wakati mwafaka kuiingiza katika hotuba zao wakitaka kuwakamata wanaopenda michezo kuwaona wapo pamoja nao.
Wanajaribu kuingiza maneno matamu kuhusiana na michezo kwa kuwa wanaijua ina nguvu kiasi gani. Hakuna ubishi hawaipendi michezo badala yake wanapenda nguvu zake ambazo wanajua zitakuwa msaada kwao.
NYALANDUKatika wagombea hao rundo wa nafasi ya urais kupitia CCM, wengi hawana sifa ya kuizungumzia michezo na kuwathibitishia wanamichezo kwamba wana nafasi ya kuikuza na kuiendeleza.
Lakini wakumbuke, michezo ina watu wengi wasikivu, waelevu na wang’amuzi wa mambo, hivyo haitakuwa rahisi kuwalaghai au kutaka kuwajaza maneno ya kijanja na kuwatumia. Halafu wakipata wanachokitaka, wawaache kwenye mataa kama ambavyo wamekuwa wakifanya miaka yote.
Pongezi kwa Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake. Kama alivyosema katika hotuba yake ya kuvunja bunge kuwa alijitahidi, yuko sahihi kabisa.
Wote tuliona namna alivyochangia, kweli aliidhinisha mishahara kwa makocha wa timu za taifa za soka, ngumi, kikapu na netiboli. Ingawa maendeleo hayakuwa makubwa sana, lakini angalau.
SITTA
Bado naweza kusema Kikwete alijitahidi, lakini serikali yake kwa kiasi kikubwa haikuwa mshiriki mzuri wa michezo na hata watu wengi walio katika wizara husika hawapo kwa ajili ya michezo kwa kuwa hawajasaidia lolote zaidi ya majungu kuliko utendaji bora zaidi.
Hivyo, mapema kabisa, taarifa hizi zimfikie atakayekuwa mgombea wa CCM, yaani yule atakayejulikana kesho kwamba yeye na wenzake, tumewasikia kuhusu michezo na akumbuke michezo ni ajira kubwa, ikifanyiwa mipangilio bora, itatengeneza ajira nyingi zenye mishahara mikubwa kuliko hata vitu vingine wanavyovitegemea.
Pia, kama amepata nafasi na atafanikiwa kushinda kuwa Rais wa Tanzania, aonyeshe kweli anaipenda michezo kama kauli walizozitoa, ana mipango nayo na si kuifanya ni sehemu ya kupita kwa ajili ya faida yake kwa ajili ya alichotaka kukipata. Kudanganywa kwa wanaspoti, imetosha.
CREDIT:SALEHJEMBE
No comments:
Post a Comment