Ben Pol kutoka Tanzania (wa pili kushoto), Wangechi kutoka Kenya (wa tano kushoto) na Silva Stone kutoka Ghana (wa pili kulia) wakiwa pamoja na vijana kutoka Tanzania waliokwenda kushuhudia tamasha la Coke Studio Afrika nchini Kenya baada ya kushinda kupitia shindano lililoedeshwa kupitia akaunti ya instagramu ya Millard Ayo.
Vijana watano wapata fursa ‘Coke Studio Afrika’ Kenya.
Coke studio Afrika ni moja ya matamasha makubwa ambayo huandaliwa na kampuni ya Coca-Cola ambayo hufanyika kila mwaka katika mataifa tofauti tofauti ya Afrika. Pia wasanii kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika hushiriki katika tamasha hilo.
Kuna Wasanii mbalimbali ambao wameshawahi kutumbuiza katika tamasha hilo. Wasanii hao ni kama vile Diamond Platinumz, Joh Makini (Tanzania), Yemi Alade (Nigeria) na wengine wengi.
Tangu Coke Studio Afrika ianze, huu ni msimu wa tatu ambapo imeshuhudiwa ukienda bega kwa bega na kampeni mpya ya ‘Sababu Bilioni za Kuamini’ yenye lengo la kuwahamasisha vijana kuamini katika kufikia ndoto zao ambazo wamekuwa wakiamini kila siku katika maisha yao.
Katika kuhakikisha kampeni hii inaenda kwa vitendo, Coca-Cola wameamua kupeleka moja kwa moja vijana watano watano kutoka hapa nchini nchini baada ya kufuzu kupitia shindano kupitia ukurasa wa Instagramu wa Millard Ayo na kupata tiketi ya moja kwa moja kwenda nchini Kenya kushuhudia tamasha la Coke Studio na kujifunza masuala mbalimbali ambayo yatawafanya wajiamini na katika kukamilisha ndoto zao.
Vijana hao ni Minaeli Benedict, Stanley Meshack , Hassani Singizi, Shabani Swaibu (wote kutoka Dar es Salaam) na Jackson Kassian (Morogoro).
Wakiwa nchini Kenya vijana hao walitembelea maeneo mbalimbali maarufu nchini humo, ikiwemo jengo maaarufu la biashara ambalo mwaka jana lilpata tafrani kutoka kwa wapiganaji wa Al Shabaab, Westgate na kujifunza masuala mbalimbali ambayo kwa namna moja ama nyingine yaliwapa mafunzo mengi sana.
Si hivyo tu, bali pia walipata fursa ya kutembelea kituo maarufu cha runinga nchini humo, Citizen TV ambapo walipata wasaa wa kufanya mahojiano mafupi na kuelezea ndoto na malengo yao ya baadaye ambayo wangependa siku moja yatimie.
Fursa nyingine waliyopita ni kutembelea studio yenyewe ambapo shughuli zote za Coke Studio hufanyika na kuoneshwa vifaa mbalimbali vilivyomo ndani ya Studio hiyo.
Tukio ambalo liliwasisimua ni pale walipokutana na msanii kutoka hapa nchini ambaye ni mkali wa miondoko ya R&B Ben Pol, bila kusahau mwanamuziki wa kike machachari wa Hiphop wa Kenya Wangech,i pamoja na mkali mwingine kutoka Ghana anayejulikana kwa jina la Silva Stone.
Walipata fursa ya kuwashuhudia wasanii hao wakitumbiza katika jukwaa la Coke Studiona kuamsha ari zao kutokana na namna wasanii hao walivyokuwa wakitoa burudani ya nguvu licha ya kuwa na umri mdogo kabisa.
Baada ya kumalizika kwa burudani kutoka kwa wasanii hao, vijana hao walipata fulana za Coke Studio na baadaye kupata nasaha kutoka kwa wasanii hao, ambapo, kwa upande wa Ben Pol aliwaambia kwamba, mpaka kufikia mafanikio aliyonayo sasa, amepitia changamoto nyingi sana ikiwemo kunyimwa nafasi ya kurekodi nyimbo zake na waandaaji mbalimbali wakiamini kuwa hakuwa na uwezo wa kuimba lakini licha ya kufanyiwa hivyo aliendelea kupambana mpaka kufanikiwa kufika alipo sasa.
“Ninachotaka kuwaambia ni kwamba, mfano, kwa wale wenye vipaji vya kuimba, kitu kikubwa unachotakiwa kufanya ni kuwa na nyimbo nyingi ambazo, hata ukirekodi moja isipofanya vizuri, unatoa nyingine ili kuhakikisha unaendelea kusikia masikioni kwa watu”, alisema
“Kitu kingine ni kwamba unaposimama mbele ya watu, waone ni wa kawaida tu na wala usiwagope, bila ya kujali nyadhifa zao isipokuwa kikubwa ni kutowaonesha dharau”, aliwasisitiza.
Wangechi kwa upande wake alisema : “ Vijana wa jinsia zote ni muhimu kujiamini na kuondokana na dhana kwamba jinsia fulani ndio wanaweza kitu fulani, kwa mfano mimi naweza kufanya ‘hiphop’ na R&B, sasa wasichana wengi hata kama wanaweza, huogopa kufanya Hiphop wakiamini kwamba ni mziki wa kiume lakini kumbe yeyote anaweza kuimba”.
Kwa upande wake, mmoja wa vijana katika kundi hilo anayejulikana kwa jina la Jackson Kassian alisema kwamba “Mimi kama muhitimu wa chuo kikuu ninapenda sana siku moja niwe meneja wa wasanii kama Babu Tale ili niweze kusimamia maslahi ya wasanii na naamini siku moja itakuwa hivyo, ila kwa sasa najishughulisha kwanza na biashara za viatu ambazo nafanya kupitia mtandao wa Instagramu, mambo yakikaa sawa basi mimi nazama moja kwa moja”, alisema.
Lengo kuu la Coke Studio Afrika ni kuwakutanisha kwa pamoja wasanii mbalimbali wa Afrika na kuimba nyimbo ambazo zina vionjo tofauti hivyo kuongeza msisimuko. Lakini vilevile kutoa fursa kwa wasanii wachanga kushirikiana na wakubwa ili kuwapa changamoto ya kuongeza ujuzi katika kazi zao na kuzidi kukuza vipaji vyao
Katika msimu huu wa Coke Studio Afrika, ni wasanii kutoka mataifa matano tu tu ndio wamechaguliwa kutumbuiza. Mataifa hayo ni Nigeria, Msumbiji, Kenya, Uganda na Tanzania
No comments:
Post a Comment