Mkuu wa Wilaya wa Wanging’ombe, mkoani Njombe Frederick Mwakalebela akifungua warsha ya kujifunza kwa pamoja juu ya utekelezaji wa mpango wa usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimaliza maji (UMURAME) iliyoandaliwa na Bodi ya Maji Bonde la Rufiji kwa kushirikiana na Shirika la WWF Tanzania iliyofanyika mkoani Njombe jana. (PICHA NA FRIDAY SIMBAYA)
Mkuu wa Wilaya wa Wanging’ombe, mkoani Njombe Frederick Mwakalebela (wa tatu kushoto walioketi) akiwa katika picha ya pamoja muda mfupi baada ya kufungua warsha ya kujifunza kwa pamoja juu ya utekelezaji wa mpango wa usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimaliza maji (UMURAME) iliyoandaliwa na Bodi ya Maji Bonde la Rufiji kwa kushirikiana na Shirika la WWF Tanzania iliyofanyika mkoani Njombe jana.
Mkuu wa Wilaya wa Wanging’ombe, Frederick Mwakalebela ametoa wito kwa wanasiasa kutoingilia kazi ya wataalam katika mipango yao ya ugawaji vibali vya matumizi ya rasilimali za maji katika wilaya zao.
Mkuu huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika warsha ya kujifunza kwa pamoja juu ya utekelezaji wa mpango wa usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimaliza maji (UMURAME) iliyoandaliwa na Bodi ya Maji Bonde la Rufiji kwa kushirikiana na Shirika la WWF Tanzania iliyofanyika mkoani Njombe jana.
Alisema kuwa wapo baadhi ya wanasiasa wanaokwamisha shughuli za waatalamu kwa kutumia nyadhifa zao kuvuruga mipango yao ya ugawaji vibali vya rasilimali za maji.
Alisema kuwa wanasiasa mara nyingi wanakuwa wanaingilia kazi ya waatalamu kwa kuwalazimisha kugawa vibali vya maji kwa kutumia ushawishi wao ambapo kunapelekea kuvuruga mipango ya usimamazi endelevu wa rasilimali za maji katika bonde.
“Ili Mto Ruaha Mkuu uwezekutiririsha maji kwa miezi kumi na mbili kwa mwaka mzima tunahitaji kupanga mipango yetu kwa kushirikiana na kila mdau kuainisha viwango vya matumizi ya maji katika bonde ambamo jamii inaishi kwa mahusiano mazuri kwa manufaa ya kiuchumi na kijamii,” alisema.
Warsha hiyo ilishirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya ya Iringa, Mbarali, Wanging’ombe, Makete na Mufindi, afisa wa maji wa Bonde la Rufiji, wawakilishi wa taasisi za serikali, maafisa mipango wa halmashauri za wilaya pamoja na timu za wawezeshaji wa wilaya (DFTs).
Wadau wengine walioshiriki warsha hiyo ni wawakilishi wa jumuiya za watumia maji (WUA) na wadau wa maendeleo toka WWF UK.
Hata hivyo, lengo la warsha hiyo ilikuwa ni kutekeleza dhana ya ushirikishwaji wa wadau katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji, ambao ni msingi wa pili miongoni mwa kanuni nne za usimamizi wa pamoja wa rasilimali za maji.
Aidha, Shirika la WWF Tanzania kupitia program ya maji Ruaha (WWF-RWP) na ofisi ya maji bonde la Rufiji (RBWO) kwa kipindi cha miaka miwili zimetekeleza mpango wa usimamizi, matumizi na uendelazaji endelevu wa rasilimali za maji katika maeneo ya mabonde madogo ya mito ya Ndembela na Mbarali.
Katika kipindi cha utekelezaji wa mpango huu wadau mbalimbali walikuwa wakishirikishwa katika kuibua shughuli za usimamizi wa rasilimali za maji chini ya usimamizi wa ofisi ya maji bonde la Rufiji na Shirika la WWF.
Mratibu wa Program ya Maji wa WWF, Kelvin Robert alisema kuwa katika kipindi cha mradi katika maeneo waliweza kutambua changamoto zinazokabili usimamizi shirikishi wa rasilimali za maji na kusababisha kukauka kwa Mto Ruaha Mkuu kwamba ni matumizi makubwa ya maji katika maeneo ya bonde, matumizi ya maji katika mashamba makubwa na madogo yasiodhibitiwa, mifugo na ongezeko la mahitaji ya maji.
Changamoto zingine ni pamoja na matumizi yasioendelevu ya ardhi, ukataji wa misitu, kilimo pamoja na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Afisa wa Maji wa Bonde la Rufiji, Idris Msuya alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa changamoto hizo zinasababisha kukauka kwa Mto Ruaha Mkuu ambao maji yake yanachangiwa na mito Ndembera na Mbarali mpango huu umeweza kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto kama vile kuzingatia viwango vya ugawaji maji kama inavyoelezwa katika vibali vya matumizi ya maji.
Utii wa sheria ya rasilimali za maji, uimarishaji wa usimamizi wa rasilimali za maji na ardhi, ushirikishaji wa wadau na uhamasishaji ushirikiano wa kisekta nje ya sekta za wadau.
No comments:
Post a Comment