Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la kuombea Amani Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 Alex Msama akifafanua jambo wakati wa mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania, Askofu David Mwasota.(Picha na Francis Dande)
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania, Askofu David Mwasota akifafanua jambo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Amani, Alex Msama akifafanua jambo.NA MWANDISHI WETU
NA MWANDISHI WETU
IDADI ya waimbaji wa muziki wa injili watakaopamba Tamasha la kuombea Amani Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, imezidi kuongezeka baada ya Sarah K kutoka Kenya naye kuthibitishwa na kamati ya maandalizi.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha hilo linalotarajiwa kuvuta hisia za wengi kutokana na umuhimu wake, Alex Msama alisema ni faraja kubwa kwa wadau wa injili na amani nchini.
Alisema mbali ya Sarah K anayetamba na nyimbo kadha wa kadha, pia Kwaya ya Kijitonyama Uinjilisti ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, nao watashiriki tukio hilo itakalotikisa mikoa 10 kuanzia Oktoba 4 hadi 18.
Msama alisema kampuni yake ya Msama Promotions imekuwa ikiwaleta waimbaji mahiri kuhakikisha tukio hilo linabeba hadhi ya heshima iliyostahili ya kuwaleta wengi pamoja.
“Tunashukuru kwamba, maandalizi yanakwenda vizuri kwani waimbaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, wamezidi kuthibitisha kushiriki tamaska hilo,” alisema Msama.
Alisema mbali ya Tamasha hilo kubeba ujumbe mahsusi wa kuombea na kuhimiza amani ya nchi, pia litatumika kuzindua albamu ya malkia wa muziki wa injili nchini, Rose Muhando.
Mbali ya Muhando, Msama alisema katika Tamasha hilo ambalo litapambwa pia na waimbaji kutoka Afrika Kusini, Rwanda, Zambia na Uingereza, Bonny Mwaitege naye atazindua albamu yake mpya.
“Mbali ya vionjo hivyo, pia tamasha hilo kutakuwa na wimbo wa pamoja kwa waimbaji wote wa kusisitiza umuhimu wa amani ya nchi wakati wote wa uchaguzi mkuu kwa mustakabali wa nchi,” alisema Msama.
Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania, Askofu David Mwasota akizungumzia tamasha hilo, amewasihi watanzania kujitokeza kwa wingi na kuliunga nmkono tukio hilo katika mikoa yote 10.
Alisema ujumbe na lengo la Tamasha hilo la kuombea amani nchi iweze kuvuka salama katika uchaguzi mkuu, ni jambo jema la kuungwa mkono na watanzania wote kutokana na thamani halisi ya amani kwa kila mmoja.
Baada ya tamasha hilo kuzinduliwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam ambalo pia litatumika kumuaga Rais Jakaya Kikwete, litaelekea katika mikoa mingine tisa ikiwemo Morogoro, Mwanza, Dodoma, Iringa, Mbeya na mingineyo.
No comments:
Post a Comment