Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu kutoka Kongo Brazzaville, Mkuu wa Msafara wa timu hiyo, Blassy Kiondo, alisema kuwa wachezaji walifanya mazoezi ya mwisho kujiandaa na mchezo huo jana asubuhi na wote wanaendelea vizuri.
Kiondo alisema kuwa mchezo huo unatarajiwa kufanyika kuanzia saa 11 jioni za Kongo Brazzaville sawa na saa moja usiku kwa Tanzania.
“Timu iko katika hali nzuri, na sasa (jana saa saba mchana) tumemaliza mazoezi kwa ajili ya mechi ya kesho (leo), vijana wanajiamini na wameahidi kufanya vizuri,” alisema Kiondo ambaye ni Mjumbe wa Kanati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Aliongeza kuwa hali ya hewa inafanana na ya jijini Dar es Salaam hivyo, haijawaathiri wachezaji kwa aina yoyote ile na kilichobakia ni kusubiri muda wa mchezo.
Baada ya mechi ya leo, Twiga Stars ambayo iko kundi A itashuka tena uwanjani keshokutwa Jumatano kucheza dhidi ya Nigeria na itamaliza hatua ya makundi Septemba 12 mwaka huu dhidi ya wenyeji Kongo Brazzavile.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment