Thursday, December 31, 2015

Kampuni 5 za simu zatozwa faini ya milioni 125/

Kampuni 5 za simu zatozwa faini ya milioni 125/
MAMLAKA ya Mawasiliano nchini (TCRA) imezitoza faini kampuni tano za simu za mkononi nchini, kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kuhakikisha uwepo wa usalama wa kiufundi na kisheria kwenye masuala ya taarifa zinazopitia kwenye mitandao yao. Kampuni hizo kila moja imetozwa faini ya Sh milioni 25.

Kampuni hizo ni Benson Informatics Limited yenye mtandao wa Smart, Mic Tanzania Limited (Tigo), Airtel Tanzania Ltd, Viettel Tanzania Ltd (Halotel) na Zanzibar Telecom Ltd (Zantel). Mkurugenzi Mtendaji wa TCRA, Dk Ally Simba alisema kampuni hizo zinatakiwa kutoa faini hiyo kabla ya Januari 29, mwaka 2016 na kwamba kila kampuni imetakiwa kujenga mazingira wezeshi yatakayoweza kuziba mianya ya uharibifu wa mawasiliano kwenye mitandao yao.

Alisema ni vema kampuni hizo zikakumbuka kwamba zinapaswa kufuata Sheria ya Mawasiliano ya mwaka 2011 na kushindwa kutimiza matakwa ya sheria ni kutoa mianya ya wahalifu kujipenyeza, kuingilia mawasiliano ya watu, hivyo kuleta matatizo kwa watumia huduma za mawasiliano.

“Tumepokea malalamiko kutoka kwa wateja kuhusu usalama wa mawasiliano ya simu, ambayo mitandao hiyo inaruhusu wahalifu kuweza kuingilia mitandao hiyo na kutuma ujumbe mfupi wa simu unaopotosha umma”, alisema Dk Simba. Alisema mamlaka hiyo na Polisi wamepokea malalamiko 42 katika kipindi cha miezi miwili iliyopita na kwamba katika matukio hayo, kila moja linaweza kusababisha hasara ya Sh milioni 25.

Alisema kampuni hizo, zinatambua wajibu wao wa kulinda usalama wa mawasiliano ya wateja na kwamba TCRA iliwakumbusha jambo hilo Oktoba mwaka huu, na kwamba hadi Desemba 2015 hakuna kampuni hata moja kati ya hizo iliyochukua hatua kutekeleza jambo hilo.

Alisema adhabu hiyo, imechukuliwa kutokana na matakwa ya sheria inayosimamia kampuni za mawasiliano na kwamba kama wakishindwa kutekeleza wajibu na mambo yaliyoambiwa kuyafanyia kazi, hatua zaidi zitachukuliwa dhidi yao, zikiwemo za kusitisha leseni zao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa TCRA, Elizabeth Nzagi, aliwaonya watumiaji wa mawasiliano kwamba teknolojia ni nzuri kwa upande mmoja na upande wa pili ni mbaya iwapo itatumika ndivyo sivyo.

Alisema ni vyema watumiaji wa mitandao, wakaitumia kwa ajili ya maendeleo na kuchukua tahadhari, kwani wapo pia wahujumu ambao huingilia mitandao na kuwataka watu watume fedha kwa ajili ya kupewa huduma fulani.

Nzagi alisema kwa wateja na watumia mitandao ni vyema kujiridhisha na ujumbe inaoupokea ili kuepuka kutuma fedha kwa matapeli ambao wakati mwingine hutuma ujumbe kwamba ndugu au wazazi wa mteja ni wagonjwa, wanahitaji fedha haraka kwa ajili ya matibabu.

“Sasa unapopokea ujumbe wa namna hiyo unaweza ukachanganyikiwa na ukajikuta unatuma fedha bila kuhakikisha namba iliyokutumia ujumbe kama unaifahamu au la, ni vyema kutulia na kuhakikisha kwanza namba hiyo ili ujiridhishe kabla ya kutuma”, alisisitiza Nzagi.

Wakati huo huo, Serikali imepiga marufuku kampuni zote zinazofanya malipo ya ujira kwa saa kwa wafanyakazi wake, kwa kuwa jambo hilo ni kinyume cha taratibu na sheria za kazi.

Onyo hilo limetolewa na Naibu Waziri, Ofisi wa Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde wakati alipobaini kuwepo kwa madudu katika kampuni ya Erolink, inayotoa huduma kwa kampuni ya simu ya Vodacom.

Aidha, ameagizwa kufutwa kwa vibali vya kazi vya muda (CTA) ambavyo vimetolewa baada ya tangazo la Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama la kuwataka waajiri kuzingatia sheria za kazi na vibali vya ajira za wageni.

Kampuni hiyo ambayo inatoa huduma ya watumishi wa Idara ya huduma kwa Mteja, ilibainika kuwalipa wafanyakazi wake Sh 2,050 kwa saa, huku likiwakata fedha wafanyakazi wanaochelewa au kupata matatizo na kushindwa kufika kazini.

“Ni marufuku kufanya malipo kwa saa, kwa sababu kwanza ni kinyume cha sheria na hairuhusiwi...kama kuna kampuni zinazofanya hivi ziache mara moja,” alisema Mavunde.

Aidha, alionya wote wanaobeza kuwa kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano ni ‘Moto wa Mabua’, wafute dhana hiyo, kwani kasi waliyoanza nayo ndiyo hiyo hiyo hadi mwisho.

Mavunde aliwataka waajiri waendelee kuzingatia kulipa mishahara kwa mujibu wa sheria; huku akiagiza kampuni hiyo kulipa wafanyakazi wake mapunjo, yaliyofanywa ndani ya siku saba na kumpelekea ripoti.

Aliwataka maofisa kazi alioambatana nao kufuatilia kampuni hiyo kwa undani zaidi ili kubaini kama kuna ukiukwaji wa sheria, uliofanywa waweze kuchukua hatua haraka iwezekanavyo.

Aidha, aliiagiza kampuni ya Vodacom kuwasilisha orodha ya watoa huduma wao na hatua walizochukua kutokana na kukiuka mikataba waliyoingia. Mavunde alibaini kuwepo kwa mapungufu mbalimbali baada ya kufanya ziara ya ukaguzi katika ofisi hizo na kuzungumza na baadhi ya wafanyakazi, ambapo pia alibaini kampuni ya Erolink kuwa na mapungufu katika masuala ya usalama mahali pa kazi, ambapo aliwatoza faini ya Sh milioni 2.5.

“Katika masuala ya kazi naagiza kabla hatujaondoka hapa tuwe tumepata mikataba ya wale waliokuja kujifunza, nakala ya orodha na vibali vya wageni wote wanaofanya kazi hapa,” alisema.

Awali, akizungumzia suala hilo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya mahali pa Kazi (OSHA), Dk Akwilina Kayumba alisema mapungufu yaliyobainika hayatokani na Vodacom bali watoa huduma wake, ambapo alisema watazuia leseni ya kutimiza masharti ya Vodacom ya Afya na Usalama mahali pa kazi mpaka watakapowasaidia washirika wao kuwa vizuri.

Awali Mavunde akiwa katika kampuni ya simu ya Tigo alisema, kampuni hiyo ambayo watoa huduma wake ni Huawei na Infinity, zinatakiwa kuzingatia sheria za kazi ili kuondoa misuguano isiyo ya lazima baina yao na wafanyakazi.

Aidha, kampuni hiyo pia haikukidhi vigezo vya afya na usalama mahali pa kazi, ambapo walitozwa faini ya Sh milioni nne na kutaka mambo yote yalibainika kuwa na mapungufu yarekebishwe.

“Kazi za wafanyakazi zibandikwe katika kila eneo ambalo linaonekana lakini hapa sijaona hilo sasa naagiza zibandikwe sasa hivi...mtekeleze sheria za ajira na taratibu zilizopo,” alisema

HABARI LEO

No comments: