Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. George Simbachawene amemuagiza
Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma kuwasimamisha kazi mara moja Kaimu Afisa
Biashara wa Manispaa ya Dodoma Bw. Elias N. Kamara na Bibi Donatila D.
Vedasto (Afisa Biashara) kuanzia leo tarehe 30/12/2015 kwa kosa la kusababisha
urasimu katika utoaji wa leseni za biashara.
Kutokana na hali hiyo Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI amemuagiza
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kumuondoa kwenye nafasi
yake Kaimu Afisa Biashara wa Manispaa na Msaidizi wake na nafasi zao
kukaimishwa kwa watu wengine ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizotolewa
dhidi yao.
Agizo hili limetolewa na Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI baada ya
kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wafanyabiashara ambayo yalionyesha
kuwepo kwa mazingira ya rushwa.
Katika uchunguzi ambao umefanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma
imegundulika kuwa kulikuwa na maombi ya leseni 750 ambayo yalikuwa
hayajashughulikiwa bila sababu za msingi na hali hiyo ilipelekea kuikosesha
Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kiasi cha shilingi Milioni 75.
Aidha, Mhe. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI ameagiza Mamlaka za
Serikali kote nchini kuhakikisha wanatoa leseni za biashara bila urasimu wowote na
muombaji apate leseni ndani ya siku 2 au 3 anapoomba leseni.
Mhe. Simbachawene ametoa agizo kwa Maafisa biashara wote nchini kuacha
urasimu katika kutoa leseni na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Imetolewa na:
Rebecca Kwandu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi ya Rais - TAMISEMI
30 Desemba, 2015
No comments:
Post a Comment