ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, January 9, 2016

TAJATI YAFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA VIWANDANI JIJINI MBEYA NA KUSHUHUDIA MAGOFU NA MITAMBO ILIYOTELEKEZWA

Baadhi ya mitambo iliyotelekezwa kwenye Kiwanda cha kutengenezea Zana za Kilimo ZZK
Mitambo ambayo ilikuwa ikitumika kutengenezea Zana za Kilimo katika kiwanda cha ZZK Iyunga jijini Mbeya ikiwa imetelekezwa
Niranjan Bandi, aliyejitambulisha kuwa ndiye Mkurugenzi mkuu wa shughuli zinazoendelea katika kiwanda cha ZZK  chini ya kampuni ya CMG akiwapa maelezo waandishi wa habari.
Waandishi wakitoka katika kiwanda cha ZZK huku wakijiuliza maswali mbali mbali kutokana na walichokikuta ndani ya kiwanda hicho
Baadhi ya waandishi wakichungulia ndani ya majengo ya kilichokuwa kiwanda cha kutengeneza sabuni HISOAP Kushuhudia kama kuna kilichosalia.
Huu ndiyo muonekano wa ndani ya majengo ya kilichokuwa kiwanda cha kutengenezea sabuni HISOAP kukiwa hakuna kitu licha ya kuwepo Mlinzi
Muonekano wa Jengo la kiwanda cha HISOAP lililotelekezwa ili hali serikali ya awamu ya tano ikisisitiza kuwa serikali ya Viwanda

CHAMA Cha Waandishi wa Habari za Utalii na Uwekezaji Tanzania(TAJATI) katika kutekeleza majukumu yake kimefanya ziara katika viwanda vine vilivyopo Iyunga jijini Mbeya na kushuhudia baadhi vikiwa vimetelekezwa.
Waandishi hao  15 kutoka vyombo mbali mbali ambao ni wanachama wa TAJATI, walifanya ziara hiyo iliyoanzia katika majengo yaliyokuwa ya Kiwanda cha kutengenezea sabuni kilichokuwa kikijulikana kwa jina la HISOAP kilichopo Iyunga jijini Mbeya na kukutana na majengo hayo yakiwa yametelekezwa.
Mbali na kutelekezwa kwa majengo hayo,pamoja na  kuwepo kwa mlinzi ambaye alikiri kulinda majengo ambayo ndani yake hajui kilichomo kwa kupitia matundu ya mlangoni,wanahabari hao walishuhudia ndani kukiwa hakuna hata mtambo mmoja ulichosalia na na matanki makubwa yanayoendelea kuoza nje.
“Mimi nalinda hapa kwa maagizo ya bosi wangu lakini huko ndani hakuna shughulli yoyote inayofanyika kwani hata hizo mboga zilizolimwa ni mali ya walinzi wenzetu ndiyo wamelima,sijui humo ndani kama kuna mitambo sijawahi kuona milango ikifunguliwa hata mwenye funguo simjui” alisema Mlinzi ambaye alitaka jina lake lihifadhiwe kwa usalama wake.
Aidha katika ziara hiyo timu ya waandishi ilifika katika majengo ya kilichokuwa kiwanda cha serikali, Kiwanda cha kutengenezea zana za kilimo maarufu kwa jina la ZZK ambapo timu hiyo ilipokelewa na raia mmoja wa kigeni mwenye asili ya kiasia,  Niranjan Bandi, aliyejitambulisha kuwa ndiye Mkurugenzi mkuu wa shughuli zinazoendelea hapo chini ya kampuni ya CMG.
Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari Bandi alisema ndani ya kiwanda hicho kuna shughuli za kutengeneza vipuri vya magari, uunganishaji wa matrekta madogo ya kilimo(powertiller ) kutoka China na kwamba zana za kilimo wameshindwa kutengeneza kutokana uchakavu wa mitambo iliyopo na imepitwa na teknolojia.
Aliongeza kuwa ifikapo januari 15 mwaka huu wanatarajia kuanza kutengeneza mabati baada ya kupata mtambo kutoka China ambao hivi sasa unafanyiwa marekebisho kabla ya kuanza kazi sambamba na uanzishwaji wa kiwanda cha kuzalisha bia cha Serengeti.
Wakati mwekezaji huyo akijieleza na kuonyesha mashaka makubwa ya uzalishaji kuwa ni changa la macho,Waandishi wa habari  walishuhudia mitambo iliyokuwa ya kutengenezea zana za kilimo ikiwa imetekelezwa bila kufanya kazi ndani ya majengo hayo ambapo Mkurugenzi huyo alisema hawana uwezo wa kuiendesha.
Baada ya kukamilisha mahojiano na Mkurugenzi huyo waandishi hao walielekea moja kwa moja katika kiwanda cha Malumalu cha Marmo Granito ambapo walitembelea mitambo ya kuchonga na kukata mawe na bidhaa mbali mbali zinazotokana na  miamba ya asili.
Mkurugenzi wa Marmo,Salim Jessa alisema tangu walipoanza uwekezaji katika Mkoa wa Mbeya wameanza kupata masoko nje ya nchi ikiwemo India,Italia na kutafuta masoko mengine nchini  China ambako watakuwa wakiuza malighafi zilizoongezwa thamani kwa ajili ya matumizi mengine.
Alisema changamoto kubwa ni ushindani wa soko baada ya kampuni zingine kujitokeza na kuanza kutengeneza bidhaa zinazotokana na mawe ya asili kama wao sambamba na uingizaji wa bidhaa zilizochakachuliwa kutoka nje kwa lengo la kuharibu soko.
Ziara hiyo ya TAJATI ilihitimishwa katika kiwanda cha Bia cha TBL ambapo waandishi walitembezwa kiwandani hapo na kisha kupata muda wa kuuliza maswali kutoka kwa wahusika.
Akizungumza na wanachama hao, Meneja wa Kiwanda cha Bia Mbeya, Waziri Jemedari alisema licha ya mafanikio waliyoyapata katika uzalishaji wanakabiliwa na changamoto kubwa ambazo ni miundombinu mibovu, gharama kubwa za maji na umeme sambamba na mlundikano wa vinywaji kutoka nje ya nchi vinavyoharibu bei ya vinywaji vinavyozalishwa nchini.
Jemedari alisema bia nyingi zinaingizwa nchini kutoka nje zinauzwa bei ya chini hivyo kupelekea wateja wengi kukimbilia na kuua soko la vinywaji vya ndani.

Na Mbeya yetu

No comments: