Friday, January 8, 2016

Yanga, Mtibwa zaisubiri Simba nusu-fainali

Mshambuliaji machachari wa Azam,Farid Mussa (kulia) akimtoka beki wa Mafunzo Haji Hassan kwenye mechi ya Kundi B uliochezwa jana kwenye uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.

Vita vya panzi, furaha kwa kunguru! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya jana Azam FC kuangukia pua ilipofungwa mabao 2-1 dhidi ya Mafunzo FC na kutoa mwanya kwa Yanga na Mtibwa Sugar kutinga hatua ya nusu-fainali ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar hata kabla ya kucheza mechi yao ya usiku wa kuamkia leo.

Kipigo hicho kutoka kwa timu hiyo iliyoonekana 'kibonde' wa Kundi B la michuano hiyo mwaka huu, kiliifanya Azam FC imalize hatua ya makundi ikiwa mkiani na pointi mbili baada ya kutoka sare ya 1-1 katika mechi zote mbili za awali dhidi ya Mtibwa na Yanga.

Baada ya kupoteza mechi zote mbili za awali -- 3-0 dhidi ya Yanga na 1-0 dhidi ya Mtibwa -- Mafunzo inayonolewa na kocha msaidizi wa Taifa Stars, Hemed Morocco, imehitimisha hatua ya makundi ikiwa na mtaji wa pointi tatu katika nafasi ya tatu.

Azam ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wa kimataifa kutoka Ivory Coast, Kipre Tcheche, aliyemalizia kwa kichwa mpira wa kona iliyochongwa na beki wa pembeni kulia Shomari Kapombe katika dakika ya 20 ya mchezo.

Lilikuwa ni bao la pili katika mechi mbili mfululizo za Kombe la Mapinduzi mwaka huu kwa straika huyo mwenye magoli saba Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Robo saa baadaye, Mafunzo ambao jana walicheza bila ya kocha wao mkuu, Morocco aliyefiwa na baba yake, walisawazisha bao hilo kupitia kwa Rashid Abdallah aliyeitendea haki pasi murua ya Ali Hassan iliyotua ndani ya sita na kuzifanya timu hizo kwenda mapumzikoni zikiwa sare ya 1-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kocha Stewart Hall akilazimika kuchezesha washambuliaji watano -- Tchetche, Allan Wanga, Ame Ally 'Zungu', Khamis Mcha na Ramadhani Singano 'Messi' ili kupata matokeo, lakini ukuta wa 'maafande' hao ulisimama imara.
CHANZO: NIPASHE

No comments: