ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, April 16, 2016

Bunge lakana sakata la Kampuni ya Lugumi

Wakati sakata la Kampuni ya Lugumi kudaiwa kushindwa kutekeleza mradi wa utambuzi wa vidole kwenye vituo polisi likipamba moto, Bunge limekana uwapo wa maagizo ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) kupeleka mkataba baina yake na kampuni hiyo.
Badala yake, Bunge limesema kilichoagizwa ni: ‘Maelezo ya kina kwa maandishi kuhusu utekelezaji wa mradi huo.”
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano cha Bunge, inasema Aprili 5 kamati ilikutana na Polisi kujadili taarifa ya ukaguzi wa hesabu zilizokaguliwa za bajeti ya taasisi hiyo zinazoishia Juni 2014 na kwamba, iliona haja ya kupata maelezo ya kina kuhusu mradi huo.
Kauli hiyo ya Bunge huenda ikazima kiu ya wengi iliyokuwa ikisubiri kwa hamu, kuona iwapo mkataba huo unaodaiwa kutotekelezwa ipasavyo kama ungewasilishwa kutokana na Polisi kushindwa kufanya hivyo mara mbili.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa, kamati ilimwandikia Katibu Mkuu wa Bunge kuhusu agizo hilo Aprili 12, ili kupatiwa taarifa kutoka kwa ofisa masuhuli na ofisi hiyo. Pia, lilimwandikia Katibu mkuu huyo siku hiyohiyo kuhusu maagizo hayo.
Hata hivyo, wakati Bunge likieleza hayo, moja ya kampuni zinazodaiwa kuhusika katika sakata hilo, Infosys IPS Tanzania Limited, imekana kushirikiana na Lugumi kibiashara katika ufungaji wa mfumo huo mitambo hiyo.
Kampuni hiyo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), imesema mwaka 2011 Infosys iliombwa na Kampuni ya Bio-Metrica LLC ya Marekani kupitia mdau wake wa biashara ambaye ni Kampuni ya Kompyuta ya Dell ya Marekani, kutoa huduma zinazohusiana na ufungaji na upimaji vifaa ambavyo viliuzwa kwa Polisi.

No comments: