ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 15, 2016

Kilango atoa ya moyoni

Kilango, ambaye Jumatatu wiki hii uteuzi wake ulitenguliwa baada ya Machi 20, mwaka huu, kudai kuwa mkoa wa Shinyanga hauna mtumishi hewa wa serikali hata mmoja.

Hata hivyo, Ikulu ilifanya uchunguzi na kubaini kuwa katika taarifa za awali kuna watumishi hewa 45, huku kazi ya uhakiki ikiendelea katika wilaya za Ushetu na Shinyanga.

Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa mikoa wote, alipokuwa akiwaapisha kuwa wafanya uchunguzi kuhusu uwapo wa watumishi hewa katika mikoa yao na kutoa taarifa.

Kutokana na kutoa taarifa hizo zisizo za kweli, Jumatatu wiki hii, Rais Magufuli alitangaza kutengua uteuzi wake, akiwa amekaa kwenye nafasi hiyo kwa siku 27. Kilango amekuwa mkuu wa mkoa wa 19 tangu kuanzishwa kwa mkoa huo.

Mbali na Kilango, Rais Magufuli pia alimsimamisha kazi Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, Abdul Dachi, kutokana na taarifa hizo za kutokuwapo watumishi hewa katika mkoa.

ALIYOSEMA KANISANI

Akiwasalimia waumini wenzake juzi, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, mjini Shinyanga, baada ya kupewa fursa ya kusema neno, Kilango alisema anamshukuru Mungu kwa kila jambo kwa yote yaliyomtokea.

“Ndugu waumini wenzangu, hili ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu. Hata mtu unapojifungua mtoto akafariki dunia, unamshukuru Mungu kwani hayo ni mapenzi ya Mungu.

"Ukiona mzazi wako kafariki dunia pia, unamshuruku Mungu. Tunao wajibu wa kumshukuru Mungu kwa kila jambo,” alisema kwa maneno mafupi na kisha kuketi, huku akiacha simanzi miongoni mwa waumini wenzake, wakiwamo viongozi wa kanisa.

ALIVYOANZA KAZI

Mbele ya kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), muda mfupi baada ya kuanza kazi, Kilango alisema Shinyanga ni mkoa wenye changamto nyingi ambazo atazishughulikia, lakini atakuwa akilazimika kukimbia Dar es Salaam kumwona mwenzi wake, Mzee John Malecela ambaye ni mgonjwa, na pindi hali yake ikiimarika wataungana naye mjini Shinyanga.

Hayo aliyasema Machi 22, mbele ya wajumbe wa kikao cha kamati hiyo na Ijumaa Machi 25, alisali kanisani hapo.

Sambamba na hayo, aliahidi kupambana na watumishi wazembe na wale wanaoendekeza rushwa na ufisadi na kurejesha hadi ya mkoa wa Shinyanga kimaendeleo.

Kilango ambaye yuko mjini Shinyanga, akisubiri kukabidhi ofisi kwa mrithi wake kwa mujibu wa utaratibu, bado anaishi hotelini kwa vile aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Ally Rufunga, hajaondoka katika nyumba ya serikali iliyoko Ikulu ndogo, eneo la Lubaga.

ALICHOKISEMA MAGUFULI

Wakati akipokea hundi ya Sh. bilioni sita kutoa kwa Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tilia Ackson, Rais Magufuli alisema aliwapa wakuu wa mikoa siku 15 wakasimamie watumishi hewa, ambazo zilimalizika Machi 31, mwaka huu.
Alisema katika siku hizo 15, aliwaruhusu kufanya kazi hiyo kwa uhuru na kuwaahidi hakutatokea kitu chochote na kwamba walifanya kazi vizuri.

Rais Magufuli alisema watumishi hewa waliopatikana ni 5,507 ambao walikuwa wanalipwa mishahara na miongoni mwao walikuwamo wanafunzi, waliokufa na waliofungwa.

Alisema serikali imekuwa ikitenga Sh. bilioni 583 kulipa mishahara na kati ya fedha hizo hulipwa watumishi hewa.
“Ninaamini uchambuzi utaendelea kufanyika ili kuokoa mabilioni ya fedha. Wizara ya Utumishi na ya Fedha muendelee kufanya kazi hiyo,” alisema Magufuli.

Alisema zaidi ya Sh. bilioni 53 zilikuwa zinapotea kwa kuwalipa watumishi hewa 5,507.

Rais Magufuli alisema watumishi hewa hawako katika halmashauri tu, bali wako kila idara ya serikali, zikiwamo Ofisi ya Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu, vyombo vya ulinzi na usalama, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na hata Wizara ya Fedha na Mipango.

Alisema wakati akiwaapisha wakuu wa mikoa kwa kutambua tatizo hilo kuwa ni kubwa, aliwapa agizo hilo na wengi waliitikia wito na kufanya kwa ufanisi.

Rais Magufuli alisema akiwa wilayani Chato, aliona taarifa zikitolewa na wakuu wa mikoa kuhusu watumishi hewa, lakini alishangaa kusikia Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga (Kilango), akisema katika mkoa wake hakuna mtumishi hewa hata mmoja.

“Nilijiuliza ni kweli? Nikatoa maagizo nikiwa Chato kuwa watu waende 'ku-verify' (kuthibitisha) katika kila wilaya kama kweli hakuna watumishi hewa. Hadi jana usiku (Jumapili usiku) walipatikana watumishi hewa 45 na bado wilaya mbili zilikuwa hazijahakikiwa,” alisema.

“Niilijiuliza sana, nikajiuliza sana na kweli nilijuliza maswali mengi kwa masikitiko mengi kwa nini mkuu wa mkoa alizungumza vile wakati hakukuwa na adhabu yoyote, lengo lake lilikuwa nini?

“Je, kama ni mkuu wa wilaya au wasisidizi wake walimdanganya kwa nini na yeye alidanganya, ni shetani gani aliyemkumba? “Nimeamua nitengue uteuzi wa mkuu wa mkoa wa Shinyanga na atapangiwa kazi nyingine pamoja na katibu tawala wa mkoa,” alisema Magufuli.

NIPASHE

No comments: