ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 17, 2016

MVUA NUSURA ITIBUE HARUSI YA DAKTARI WA MUHIMBILI

Zile hekaheka, nderemo na vifijo zilizotarajiwa kuwapo nyumbani kwa bwana harusi Dk Eric Mushi, zilitoweka jana na badala yake kujikuta akitumia muda mwingi kunusuru samani zake baada ya mvua kusababisha nyumba yake kujaa maji na kutibua shamrashamra za harusi hiyo.
Licha ya ndoa hiyo kufungwa baadaye jioni kwenye Kanisa la Katoliki, Parokia ya Makuburi, mafuriko hayo yalisababisha nguo za harusi za daktari huyo wa Upasuaji Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kuloa huku vyakula, magodoro na mali nyingine vikisombwa na maji.
Nyumba ya bwana harusi huyo ilikuwa imejaa maji kuanzia sebuleni hadi vyumbani huku vyombo vikionekana kuelea.
Licha ya ndoa hiyo kufungwa baadaye jioni kwenye Kanisa la Katoliki, Parokia ya Makuburi, mafuriko hayo yalisababisha nguo za harusi za daktari huyo wa Upasuaji Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kuloa huku vyakula, magodoro na mali nyingine vikisombwa na maji.
Nyumba ya bwana harusi huyo ilikuwa imejaa maji kuanzia sebuleni hadi vyumbani huku vyombo vikionekana kuelea.
“Harusi ya mwanangu, imeingiwa na mkosi gani huu!” alisikika mama mzazi wa bwana harusi aliyejitambulisha kwa jina la Mama Mushi, akilalamika.
Mwandishi wetu akiwa nyumbani kwa bwana harusi huyo alishuhudia familia ikiwa imepigwa na butwaa huku bwana harusi akishirikiana na ndugu na jamaa kutoa maji yaliyojaa ndani na kuhamisha baadhi ya vitu na kuvipeleka nyumba za jirani.
Wanafamilia hao walionekana wakikausha baadhi ya nguo na viatu vya bwana harusi ili ikifika saa nane mchana, muda wa kwenda kanisani, viwe vimekauka.
Mdogo wa bwana harusi, Rehema Mushi alisema nguo zao zote zimelowana na hawajui watavaa nini kwenye harusi ya kaka yao pia hawajui wapi watalala baada ya kutoka harusini.
“Hapa nilipo natamani harusi ingeahirishwa tu maana hakuna raha tena, kaka kachanganyikiwa mama mwenyewe unamuona hali yake, hapa nilipo mimi mwenyewe hata sielewi na mvua inaendelea kunyesha hatujui pengine itatokea kubwa zaidi” alisema Rehema.
Kaka wa bwana harusi, Frank Mushi alisema ingawa harusi lazima ifanyike lakini kwa hali ilivyo, familia nzima imechanganyikiwa.
“Harusi itafanyika ndiyo, lakini ndugu tuliowaalika kuja kwenye harusi tutawalaza wapi?” alisema.
Bwana harusi, huku akikataa kurekodiwa wala kupigwa picha kwa madai kuwa itamchafua na kumuonyesha kwamba daktari anaishi mabondeni alisema muda huo alikuwa akitakiwa kwenda saluni kujiandaa lakini alishindwa kutokana na hali ilivyokuwa nyumbani kwake.
Huku akishirikiana na majirani kufunga bomba la kuvuta maji lililoletwa na Diwani wa Makuburi, Hanifa Kiwili ili kusaidia kupunguza maji kwenye nyumba za eneo hilo Dk Mushi alisema:
“Usinipige picha ukanionyesha kwenye magazeti ni aibu watu watajua naishi mabondeni na nimepatwa na mafuriko, huu ni msala dada yangu... hapa nilipo hata sijui nifanyeje,” alisema huku akiwazuia ndugu zake wasitoe taarifa za kina juu ya harusi yake.
Diwani anena
Akizungumza kwa simu Diwani Kiwili alisema wingi wa maji hayo umesababishwa na ukuta uliojengwa na mkazi mmoja wa eneo hilo.
“Lakini tayari nimepeleka bomba la kunyonya maji wakati nikifanya utaratibu wa kutafuta mkandarasi wa kuangalia ukuta uliojengwa na mkazi wa eneo hilo ambao unasababisha maji kutuama. Tunaweza kuutoboa ili kusaidia maji kupita kirahisi,” alisema.
Hali ilivyokuwa kanisani
Baada ya kushuhudia sakata la mafuriko hayo nyumbani kwa Dk Mushi, mwandishi wetu alifika kanisani katika Kanisa Katoliki Makuburi, saa tisa alasiri ili kushuhudia ndoa hiyo.
Bwana harusi alionekana akiwa nadhifu na alifika kanisani kwa wakati tofauti na ndugu zake ambao walichelewa na kukuta maharusi wakiwa wanajiandaa kufungishwa ndoa.
Tofauti na ilivyozoeleka, ndugu wa bwana harusi hawakuonekana wakiwa wamevaa sare zao, badala yake walikuwa wamevaa nguo tofauti.
Mara baada ya ndoa kufungwa maharusi hao pamoja na ndugu wengine waliondoka kuelekea ukumbini.

No comments: