Mvua zinazoendelea kunyesha nchini zimesababisha vifo vya watu wawili, mamia ya wananchi kukosa makazi, samani zao kusombwa na maji na shule nne kufungwa.
Morogoro
Vifo vilivyotokana na mvua hizo ni vya wanafunzi wawili wa shule za msingi Ifakara na Mbasa Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro baada ya kusombwa na maji walipokuwa wakiogelea katika mfereji unaopokea maji kutoka Mto Lumemo.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Viwanja Sitini Ifajara, Gregory Midas alisema jana kuwa wanafunzi hao; Ester Kong’oa (13) anayesoma darasa la sita Shule ya Msingi Ifakara na Rehema Lyakalyaka (12) wa darasa la nne, Shule ya Msingi Mbasa, walifariki dunia juzi tatu asubuhi.
Alisema mbali ya maafa hayo, mafuriko hayo yamesababisha shule nne kufungwa ikiwamo ya Sekondari Kwashungu na tatu za msingi Ifakara, Lumemo na Mautanga.
Midas aliwataka wazazi wanaoishi katika eneo hilo kuwa makini na watoto wao katika kipindi chote hasa cha mvua.
Dar
Katika mvua zilizonyesha jana jijini Dar es Salaam, maeneo yote yaliyobomolewa mara baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani, yalionekana kufunikwa kwa maji jambo ambalo baadhi ya wananchi walilielekezea kwamba huenda limeokoa maisha wakazi waliokuwa wakiishi maeneo hayo.
Mafuriko hayo yaliyotokana na mvua zilizonyesha kwa siku mbili mfululizo, pia yalisababisha hasara kubwa baada ya vitu na mali mbalimbali kusombwa na maji hasa maeneo ya Jangwani, Kigogo, Msimbazi, Tabata Kisiwani, Mbezi Masana na Tandale kwa Mtogole.
Tandale
Katika eneo la Tandale kwa Mtogole, zaidi ya nyumba 30 zilikuwa zimezingirwa huku wakazi wengi wakiilaumu halmashauri kwa kushindwa kutekeleza maagizo ya kukarabati miundombinu licha ya wananchi kuonyesha juhudi za kukabiliana na kero hiyo.
Mmoja wa wakazi hao, Shaban Makamba alisema eneo analoishi limekuwa likiathiriwa na mafuriko kila mvua kubwa zinaponyesha licha ya wananchi kuchanga fedha ili kutatua kero hiyo.
“Tulichanga Sh41 milioni kwa ajili ya tatizo hili, lakini kwa bahati mbaya mtaro ulijengwa lakini haukuwa na kiwango, mwishowe ukawa kero zaidi tukaamua kuufukia ili angalau mambo yawe safi. Kama unavyoona magodoro, vitanda na samani za majumbani zinaharibika,” alisema Makamba.
Tabata
Hali ilionekana kuwa mbaya zaidi eneo la Tabata Kisiwani ambalo halina mitaro ya kupitisha majitaka hivyo kutuama kutokana na mvua hizo.
Waandishi wetu walishuhudia wananchi wakipita kwenye maji hayo yaliyowafika magotini huku baadhi ya magari yakinasa kwenye madimbwi.
“Tunaingia tu hatujui wengine wamezibua vyoo mwisho wa siku tunamuomba Mungu atuepushie mbali na maradhi,” alisikika mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mama Ashura akisema.
Katika eneo la nyuma ya Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Tabata Relini, hali ilionekana kuwa tete. Daraja lililokuwa jirani na ofisi hiyo lilifurika maji na kuzuia magari kupita.
Magari kadhaa yalinasa huku bodaboda zikipita juu ya reli jambo lilikokuwa likihatarisha maisha ya abiria.
“Hali ikiendelea hivi sidhani kama kesho watu wataweza kutoka maana hata huku relini kunateleza, itafika wakati hata bodaboda zitashindwa kupita,” alisema dereva wa bodaboda, Hamis Farid.
Mbezi
Katika maeneo ya Mbezi Masana, Block C, wakazi wa maeneo hayo walilalamikia nyumba iliyopo kwenye kiwanja namba 212 kwa kuziba mkondo wa maji.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbezi Masana, Adel Alex alisema mmiliki wa nyumba hiyo alijenga eneo la wazi na hata alipoamriwa kufungua eneo hilo ili kuruhusu maji yapite ameendelea kukaidi: “Tulishapeleka malalamiko yetu halmashauri hatujui kwa nini suala hilo linakuwa gumu kutatuliwa.”
Mmoja wa wakazi hao alisema amepata hasara kwani samani zake zimeharibika pamoja na kuua vifaranga vya kuku 400.
Imeandikwa na Herieth Makwetta, Elizabeth Edward na Juma Mtanda
No comments:
Post a Comment