Mahakama Kuu ya Kenya imebatilisha marekebisho ya sheria yaliyompa Rais mamlaka ya kuteua Jaji Mkuu kinyume na Katiba, uamuzi ambao umeelezewa na wanasheria wa Tanzania kuwa umechelewa kufanywa hapa nchini.
Wiki iliyopita, majaji watano wa Kenya, Richard Mwongo, Joseph Onguto, George Odunga, Weldon Korir na Mumbi Ngugi walibatilisha mabadiliko ya sheria hiyo, wakisema yanaweka mwanya wa upendeleo, ukabila na hila, gazeti la Metro limeripoti.
Chama cha Wanasheria cha Kenya (LSK) kilifungua kesi hiyo kikipinga mabadiliko ya sheria sehemu ya 30 (3) yaliyofanywa na Bunge Desemba mosi mwaka jana na kusainiwa na Rais Uhuru Kenyatta kabla ya Krismasi, kwa maelezo kuwa yanapingana na Ibara ya 166 ya Katiba.
Mabadiliko hayo yalitaka Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) kuwasilisha kwa Rais majina matatu katika kila nafasi ya watu wanaopendekezwa kuteuliwa kuwa Jaji Mkuu na Naibu Jaji Mkuu.
“Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Mahakama ya 2011 ni kinyume na Katiba na ni batili,” alisema Jaji Mwongo wakati akitoa hukumu ya kesi hiyo.
Hukumu hiyo inasema Rais hawezi kuwa na nafasi ya ‘kung’ata mara mbili’ kwa kuwa tayari anawakilishwa katika JSC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wajumbe wawili wa Serikali aliowateua kwenye tume hiyo.
“Uteuzi unatakiwa kuakisi matakwa ya tume. Mchakato wa uteuzi ni mamlaka kamili ya JSC na huanza kwa kutangaza nafasi hiyo na lini majina hayo yatapelekwa kwa Rais,” inasema hukumu hiyo. Kutokana na uamuzi huo, JSC sasa itapeleka jina moja kwa kila nafasi ili Rais aidhinishe.
Muungano wa vyama vya upinzani wa Kenya, Cord pia ulizungumzia suala hilo, ukisema mabadiliko hayo yalikuwa ni mpango wa kumpa Rais Kenyatta mamlaka juu ya Mahakama Kuu, ambayo imepewa kazi ya kuamua kesi za uchaguzi.
Sheria hiyo ilipata pigo mapema mwaka huu wakati Jaji wa Mahakama Kuu, Isaack Lenaola aliposimamisha kesi ya uchaguzi akisubiri uamuzi wa kesi hiyo.
Ulivyopokewa Tanzania
Uamuzi huo umepokewa kwa hisia tofauti na wanasheria wa Tanzania, wengi wakisema umechelewa.
Jaji Ramadhan Manento, ambaye amestaafu alisema uhuru huo wa Mahakama ulitakiwa kuanza kutekelezwa mapema.
“Kwa sababu watu walipeleka mapendekezo mengi, nadhani hayakukubaliwa,” alisema Jaji Manento alipoulizwa maoni yake kuhusu hukumu hiyo.
“Ukisoma ile Katiba Inayopendekezwa na ile ya (Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Joseph) Warioba utaona. Maana hata Katiba yetu ya mwaka 1977 inasema The President may (Rais anaweza), yaani si lazima achague majaji wa Mahakama Kuu kutokana na orodha anayopewa. Anaweza kwenda nje akaweka na wengine (badala ya kulazimishwa kuteua kutoka miongoni mwa waliopendekezwa).”
Jaji Manento aliyekuwa Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu alisema Katiba ya sasa haimbani Rais kutoteua majaji anaowataka.
“Kile kifungu kinatakiwa kiseme The President shall be bound to appoint the names given to him by Service Commission (Rais atalazimika kuteua majina aliyopewa na Tume ya Huduma za Mahakama),” alisema Jaji Manento.
“Nimekuwapo mahakamani kwa miaka 35, sikupata mtu hata nikiwa mahakama za chini, aliyenielekeza au hata kuniandikia kikaratasi kumsaidia. Hayo ni maadili tunayoita ya kimahakama na ndiyo yanayoleta uhuru wa Mahakama na mahakimu na majaji,” alisema.
Jaji Manento analingana na mwenyekiti wa majaji wastaafu, John Mihayo ambaye alisema uamuzi huo umechelewa hapa nchini pamoja na kuwapo kwa majaji waliowahi kuonyesha uwezo mkubwa wa kuwa huru.
“Hoja za wengi hapa nchini ni kuwapo na utaratibu kama ilivyo kwenye mchakato wa kumpata Spika wa Bunge. Iwe hivyo katika kumpata Jaji Mkuu. Kwa sasa Rais anaweza kupelekewa majina matatu, lakini asichague hata moja kwa mujibu wa Katiba. Sasa ninadhani labda Serikali inaogopa uhuru wa Jaji Mkuu,” alisema.
Jaji Mihayo alisema mazingira ya utendaji kwa jaji hapa nchini ni magumu kutokana na mtazamo unaoathiri uhuru wake katika maamuzi.
“Anaweza kuwa mtenda haki, lakini kimfumo inakuwa vigumu kuonekana anatenda haki kwa jamii,” alisema.
Sababu nyingine aliyosema ni mazoea ya Katiba ya Tanzania. Alisema katiba hiyo imefanyiwa maboresho kadhaa lakini Taifa halijawahi kuona umuhimu wa kuboresha mamlaka hayo ya Rais.
“Lakini si kila kitu ndani ya Katiba lazima tuangalie kwa jirani zetu. Mabadiliko ya kikatiba yatokane na mahitaji ya nchi yetu. Kenya walifanya mabadiliko yao lakini yako mengine leo hii wanajutia. Jambo la msingi tufanye tafiti na kujifunza wenzetu wanafanikiwaje kwenye maboresho ya Katiba,” alisema.
Wakili Fulgence Massawe alisema mfumo huo umeshindwa kutumika Tanzania kwa sababu ya kukwama kwa mchakato wa Katiba.
“Tofauti na Katiba za wenzetu, Rais wetu ana madaraka makubwa sana. Kuna nafasi ambazo Katiba za wenzetu zinatoa nafasi kwa mamlaka nyingine kufanya uteuzi na si kuteua mtu tu, bali anafanyiwa mpaka usaili ili kuangalia kama anafaa nafasi hiyo. Kwetu sisi hatuna,” alisema Massawe.
Massawe alisema kwa sasa ni vigumu kwa Tanzania kupata fursa hiyo kwani mchakato wa Katiba ulishavurugika.
“Mchakato wa Katiba umeshaharibika, sidhani kama utarudi kama ulivyokuwa awali. Katiba inayosemwa ya ‘Chenge” ni sawa na marekebisho tu ya hii ya sasa, kwa sababu mambo mengi yaliyowekwa na Tume ya Warioba yalikataliwa, kwa hiyo mfumo huohuo utabaki,” alisema.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema Tanzania kuchelewa kuboresha Katiba kunatokana na tamaa ya kuendelea kujirundikia mamlaka na kubana uhuru wa Jaji katika kutekeleza majukumu yake.
“Serikali inaona inanufaika kupitia mazingira hayo kwa sababu majaji wengi wanashindwa kufanya uamuzi wao kwa uhuru ili kulinda fadhila ya uteuzi wake,” alisema.
1 comment:
Inadaiwa uamuzi kama huo umechelewa kufanyika hapa kwetu. Kwani Katiba ya Kenya ndiyo yetu? Uamuzi huo ni tafsiri ya Katiba ya Kenya, mbona tusiamniwe Katiba yetu inasemaje? Mbona tunapenda kuiga tu na kufuata vitu bila hoja? Hata kama ni wanasheria basi ndio wale waliosomea shahada za St Joseph!
Post a Comment