Waziri Mkuu, Kassim Majjaliwa akizungumza na wazee, wafanyabiashara , viongozi wa dini na wanachi wa Dodoma khusu mikakati ya seriali ya kuhamia Dodoma kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma Julai 26, 2016. Wengine kutoka kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Uledi Mussa, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,Antony Mavunde (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
-Aongoza kikao cha wadau kujadili utekelezaji wa Serikali kuhamia dodoma
-Aongoza kikao cha wadau kujadili utekelezaji wa Serikali kuhamia dodoma
-Awapa siku 14 wakamilishe
na kumkabidhi mpango kazi wao
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema uamuzi wa Serikali
kuhamia siyo siasa kama watu wanavyodhani bali ni utekelezaji wa maamuzi kamili
na kwamba Serikali inakamilisha eneo la kisheria juu ya uamuzi huo.
“Hapa tulipofika ni hatua ya utekelezaji wa
pamoja na hakuna namna nyingine kwa sababu uamuzi umeshatolewa. Nataka
niwahakikishie kwamba hii siyo siasa, tunachokamilisha ni eneo dogo tu la
kisheria juu ya uhamishaji wa makao makuu kuja Dodoma na katika Bunge la
Septemba sheria hii itapitishwa,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo jioni (Jumanne, Julai 26,
2016) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa, Serikali za mitaa, viongozi wa dini,
wajasiriamali, wazee wa mji huo, wasafirishaji, wafanyabiashara, wakuu wa
taasisi za elimu, za kifedha na watoa huduma mbalimbali katika mkutano
uliofanyika kwenye ukumbi wa Hazina ndogo mjini Dodoma.
Waziri mkuu ambaye aliitisha kikao cha kazi na
wadau hao mjini Dodoma, ameutaka uongozi wa mkoa huo pamoja na wadau wake wakae
na kuandaa mpango kazi wa jinsi ya kupokea na kutekeleza uamuzi wa Serikali
kuhamia Dodoma.
Pia ametoa siku 14 kwa uongozi wa mkoa wa
Dodoma kukamilisha mpango kazi wao na kumkabidhi mapendekezo yao ili yaweze
kuingizwa kwenye mpango mkubwa wa Serikali kuu.
“Uongozi wa Mkoa,
ukishirikiana na Ofisi yangu kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi
ya Rais TAMISEMI usimamie na kuyaratibu majukumu haya. Ndani ya siku 14 nipate proposal ya kwanza namna
mtakavyoyatekeleza. Naagiza kiundwe kikosi kazi chini yenu kitakachowajumuisha
makundi yote niliyoyataja,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu
amesema chimbuko la uamuzi wa kuhamia Dodoma kuifanya makao makuu ya Serikali lilikuwa
ni ndoto ya Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambayo imeendelea
kudumu katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ikiwemo Ilani ya
Uchaguzi ya Mwaka 2015 chini ya Ibara ya 151.
“Napenda
kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, na viongozi wengine
wote wa Chama kwa kusimamia ndoto ya Baba wa Taifa ya kuhamishia Makao Makuu hapa Dodoma. Ni imani yangu kuwa wananchi
wote mtaunga mkono uamuzi huu muhimu kwa Serikali yetu na wananchi kwa ujumla,
amesema.
Akiweka
msisitizo juu ya kazi kubwa inayowakabili viongozi hao, Waziri Mkuu amesema masuala
yanayotakiwa kufanyika kuanzia sasa ni pamoja na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kuhakikisha eneo la makazi ya Serikali Kuu litakalotumika kwa ofisi za
wizara na taasisi zake, makazi ya watumishi na huduma za biashara elimu na
taratibu zote za kisheria za kulitwaa zinakamilika kwa haraka na linakuwa
tayari kwa matumizi.
“Natambua kazi iliyopo mbele yetu ni kubwa na inahitaji
jitihada za pamoja. Hivyo kila taasisi na mtu mmoja mmoja ana jukumu la
kuhakikisha kuwa tunajipanga vizuri na kuweka mazingira ya ujio wa Serikali katika
maeneo yote muhimu,” amesema.
Amezitaka
Mamlaka za Mipango Miji na hasa CDA wahakikishe wanaweka mfumo mmoja wa
upatikanaji wa viwanja ambao utajulikana na kila mmoja, utakuwa wazi usio na
urasimu. “Mfumo huu wa viwanja uwekwe kwenye mfumo wa kompyuta na uuzaji wa
viwanja hivyo uwe wa kieletroniki kuepusha udanganyifu kutoka kwa madalali,”
amesisitiza.
Waziri
Mkuu ameonya CDA na Manispaa zisibadili ramani ya mipango miji iliyokwishawekwa
awali kama vile maeneo ya wazi kutumika tofauti na makusudio yaliyokusudiwa na akaagiza
maeneo hayo yote yarejeshwe na kufufuliwa.
“Natambua
katika makazi hapa Dodoma kulitengwa maeneo ya vituo maalum vijulikanavyo kama D Centers kwa ajili ya kutoa huduma
mbalimbali. Cha ajabu sasa kuna magenge, groceries
na sasa naagiza kwa hadhi ya Makao Makuu haya maeneo sasa yatumike kuwekeza
maduka makubwa (shopping malls) ambamo huduma zote mbalimbali hupatikana,”
amesema.
Ameitaka Manispaa iboresha usafi wa mazingira
na bustani zake kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali kuzitunza. Pia ameitaka
manispaa ya mji huo ishirikiane na TANROADS kuboresha barabara zote za mitaa na
taa za barabarani mji ukae kisasa, na usalama uwe bora zaidi.
“Eneo
jingine muhimu ni Manispaa na CDA kuhamisha makundi mbalimbali ya
wafanyabiasahra na huduma za masoko yasiyo rasmi na kuyapa maeneo yaliyo rasmi
na bora zaidi. Hii ni pamoja na maeneo
ya maegesho ya bajaji, bodaboda, taxi na daladala. Pia mazingira ya Stendi Kuu yaboreshwe,
vyoo vya kulipia pia vijengwe katikati ya mji,” amesisitiza.
Waziri Mkuu
ameuagiza uongozi wa Wakala wa majengo (TBA)
waorodheshe majengo yote ya Serikali na taasisi zake yanayotumika kwa sasa na
yasiyotumika, “Nataka muyawekee utaratibu maalum wa matumizi yake ili tupate kujua
yanayoweza kutumika kwa muda kwa baadhi ya wizara na taasisi zake. Hii ni
pamoja na jengo jipya la Mkuu wa Mkoa, linaloendelea kujengwa.”
Amewataka wakazi wa Dodoma watumie fursa hiyo kujenga
nyumba za kuishi za kutosha, nyumba za kulala wageni na mahoteli ili watu
watumishi na wageni wanapokuja wasipate taabu mahali pa kuishi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
3 comments:
Tunakubaliana na hilo. Vyema kabisa pia tunaomba kujua utakuwa umebana matumizi au umeongeza matumizi katika maandalizi hayo na kilinganisha na ofisi nyinginezo kwani majengo hayawezi kuhamiwa bila vifaa muhimu na umeme na maji. Ulinzi na usalama wa kitaalamu. Bila kushau nyumba za kuishi na familia. Pia zile za Dar es salaam zirejeshwe. Ninapita. Nitarudi tena jibu likitoka.
Kwanini imechukuwa miaka mingi
Kwanini uamuzi uwe ghafla
Uamuzi wa kuhamia Dodoma ulikuwa wakati wa chama kimoja
Serikali imeendelea kujenga kila dar pamoja na kwamba ilijuwa si makao makuu
Tunataka kura ya maoni
Kuhusu hili
Kwani itachukuwa miaka mingi Dodoma kuwa Kama dar
Bora rudusheni dar
Na feha za ujenzi zitumike kwa maendeleo mengine
Safari hii imekuwa hafla kuhamia dodoma kwa sababu mtendaji mkuu wa serikali hana siasa za blah blah ni kazi tu.
Post a Comment