Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akielezea dhamira ya kuanzishwa kwa Ikungi Half Marathon ofisini kwake. Na Mathias Canal, Singida
Ni kama vile kuwa na kiu kizito kinachohitaji maji ya kunywa na kisha maji yakakutikana kusikojulikana, ndivyo itakavyokuwa Wilayani Ikungi Mkoani Singida mara baada ya kutangazwa mashindano ya riadha yanayojulikana kama Ikungi Half Marathon 2016.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi siku ya Jumamosi Septemba 3, 2016 katika Vijiji 101 vilivyopo Wilayani Ikungi.
Akizungumzia dhamira ya kuanzishwa kwa mashindano hayo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu amesema kuwa itakuwa ni kuibua vipaji kwa vijana na kuviendeleza, Kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa vijana na kuwaandaa vijana katika Wilaya hiyo kwa ajili ya mashindano mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa.
Alisema kuwa Mashindano ya mbio ndefu yenye umbali wa kilomita 21 yatahusisha vijana wenye umri wa kuanzia miaka 17 hadi 30 waishio Wilayani Ikungi na yatafanyika kila mwaka ili kuinua hamasa ya Mchezo wa riadha huku yakiambatana na mbio fupi za mita 100, mita 200, mita 400 na mita 800.
Mashindano hayo yataanzia katika ngazi ya Vijiji Septemba 3, 2016, ngazi ya Kata itakuwa ni Octoba Mosi, Ngazi ya Tarafa ni Octoba 15, 2016 na kwa ngazi ya Wilaya itakuwa ni Octoba 29, 2016.
Dc Mtaturu alisema kuwa kuanzishwa kwa kuzinduliwa kwa mashindano hayo ni katika kuhakikisha Wilaya ya Ikungi inaibua changamoto katika sekta ya michezo nchini hivyo hiyo ni fursa muhimu kwa washiriki kujitokeza ili kuonyesha uwezo wao katika kusakata riadha.
Mtaturu alisema kuwa mwaka 2017 panapo majaaliwa wamejipanga kufanya mashindano ya Ikungi Marathon yatakayohusisha mbio ndefu za kilomita 42 ambapo jambo hili itakuwa ni kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli.
Ameeleza kuwa mashindano hayo pia yamedhamiria kuitambulisha Wilaya hiyo Kitaifa na Kimataifa kupitia shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo michezo mbalimbali hususani mashindano ya Riadha.
Aidha amewaomba vijana wote wenye umri uliofikia miaka 17 kujitokeza kwa wingi katika mashindano hayo ili kuimarisha afya zao na kuachana na mawazo ovu yakiwemo yale ya kujihusisha na wizi na ujambazi, Ngono zembe pamoja na ubakaji.
Kwa upande wake Afisa michezo Wilayani Ikungi Abubakary Kisuda alisema kuwa mashindano ya ngazi ya Vijiji yatafanyika kwa lengo la kupata vijana watakaoshindana ili kushiriki mashindano ya ngazi ya Kata, ambapo mashindano ya Kata yatafanyika kwa lengo la kupata vijana watakaoshindana ili kushiriki mashindano ya ngazi ya Tarafa.
Kisuda alisema kuwa hili ni tukio la awali kabisa kuanzishwa Wilayani humo tangu kuanzishwa kwa Halmashauri ya Wilaya hiyo miaka mitatu iliyopita hivyo litaibua hisia chanya na kuigwa na Taifa zima.
No comments:
Post a Comment