ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 14, 2016

KUMBUKUMBU YA MIAKA 17 YA MWALIMU NYERERE(1922-1999)

Tukimuelewa Nyerere katika ‘Binadamu na Maendeleo’ tutamsaidia sana Magufuli
LEO taifa linaadhimisha kifo cha muasisi wa taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere.

Katika maadhimisho haya hotuba mbalimbali hutolewa, shughuli mbalimbali hufanyika, ibada na kuweka mashada ya maua katika kaburi la muasisi huyu wa taifa. Zipo asasi na kampuni pia ambazo huandaa au kushiriki katika matembezi ya hisani ili kukusanya fedha kwa ajili ya shughuli za kijamii katika siku hiyo mfano Bank M, Rotary Club, Pepsi, Toyota na nyinginezo ili kuenzi moyo wa Baba wa Taifa kuitumikia na kuikomboa jamii kutoka katika ujinga, maradhi na umasikini.

Kiserikali, maadhimisho haya huambatana na sherehe za kuzima Mwenge na kwa mwaka huu itafanyika katika mkoa wa Simiyu. Yote haya ni heri lakini swali langu ni je, tunafuata misingi ya muasisi huyu katika kuliletea taifa maendeleo? Kama jibu ni ndiyo, mbona kila kukicha ni majipu na kutumbuliwa? Kama jibu ni hapana, kwa nini hatufuati? Kama hatuifuati misingi ile na kusababisha nyufa, kwa nini tunasema tunamuenzi au tunaadhimisha?

Hata miaka 17 baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere bado hatujamuelewa Mwalimu katika kutimiza wajibu wetu ili kuliletea taifa maendeleo. Hivyo katika maadhimisho ya mwaka huu 2016, nimeona ni vyema nishiriki kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kupitia kitabu cha Mwalimu Nyerere ‘Binadamu na Maendeleo’ kwa lengo mahsusi la kuamsha ari na nia ya kuchapa kazi, kuongeza uwajibikaji na uzalendo ili kuziunga mkono juhudi za Rais wetu wa sasa katika kuijenga upya Tanzania ya viwanda, haki, uwajibikaji, uadilifu, umoja, amani, mshikamano, uhuru na maendeleo endelevu.

Kitabu cha Binadamu na Maendeleo ni mkusanyiko wa hotuba 11 alizozitoa Mwalimu Nyerere katika muktadha tofauti, lakini akilenga nchi kujiletea maendeleo. Katika baadhi ya hotuba hizi nilizochagua nitagusia muktadha, kauli kuu na hali ilivyo sasa na wajibu wetu katika kumuenzi Mwalimu Nyerere katika kipindi cha awamu ya tano ya uongozi wa nchi yetu.

Amani ndio mambo yote

Mosi, ni ‘Mwaka mpya wa amani’ aliouzungumzia wakati akiwahutubia mabalozi wa nchi za nje walioko Tanzania, Januari mosi, 1968. Alisema: “Furaha yetu ya kibinadamu, maendeleo yetu ya kiuchumi na ya maisha kwa ujumla, yote yanategemea kuwako kwa amani.” (uk 2). Miaka 17 baada ya kifo chake, amani bado ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na ustawi wa jamii. Palipo na amani pana uzalishaji, biashara, matumizi bora ya rasilimali, uwekezaji, furaha, ubunifu, demokrasia na haki za kiraia.

Rais wetu wa sasa anahimiza amani na umuhimu wake kwa jamii. Kuna kundi lisiloona umuhimu wa amani, kila kukicha utasikia matukio ya ujambazi, uporaji, dhuluma za ardhi, madini, huduma duni za afya na matabaka baina ya matajiri na masikini. Wakati umefika wa kuilinda na kuitetea amani kwa fikra, maneno na matendo kwetu wenyewe na kwa jamii inayotuzunguka. Kumuenzi Mwalimu katika kudumisha amani, ni kusimamia haki, uwajibikaji, mgawanyo wa rasilimali, kudumisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

Kuwekeza kwenye elimu ni faida

Pili, ‘Faida ya elimu katika nchi’. Akihutubia wanajumuiya wa Chuo Kikuu cha Liberia mjini Monrovia, Februari 29, 1968, Nyerere alihimiza faida ya elimu katika nchi kwa kusema: “Tunatumia fedha kutafuta faida katika akili ya mwanadamu, kama vile tunavyotumia fedha kununua trekta.” (uk 2). Katika hili anahimiza uwajibikaji zaidi kwa watu wenye elimu kubwa kutokana na uwekezaji mkubwa wa rasilimali uliofanywa kwao.

Kwa msingi huo, mimi sikutegemea kama baadhi ya wasomi wetu wangetusaliti kwa kuingia mikataba mibovu ya uchimbaji madini, uwekezaji katika miradi ya umeme, ujenzi wa majengo ya taasisi za umma kama vile benki kuu, vyuo, madaraja, hospitali na shule. Huduma mbovu za afya, elimu, maji na chakula ni matokeo ya kutomuelewa Mwalimu na ndio maana miaka 17 baada ya kifo chake, bado tunatumbuliwa kwa kutoitumia vyema elimu yetu.

Tumeshuhudia maprofesa na madaktari wa falsafa wakitumbuliwa pia. Hii ni aibu kwao na kwa elimu waliyoipata. Yaani elimu yao imewageuza majipu! Wasomi wetu waisome upya hotuba hii ili walitendee haki taifa na jamii kwa ujumla kwa uwekezaji uliofanywa kwa ajili yao. Pia tuunge mkono kwa hatua ya Rais Magufuli kutoa elimu bure kwani anatekeleza kile alichosema Mwalimu kwamba ni lazima tutafute faida kwenye akili ya mwanadamu.

Vyama ni kwa maendeleo ya watu?

Tatu, ‘Lazima chama kiwasemee watu’. Hii ni hotuba aliyoitoa kwenye mkutano wa wanachama wa UPC nchini Uganda Juni 7, 1968. ‘Ukweli ni kwamba chama ndicho msingi wa serikali ya kidemokrasia kama kinafanya kazi yake sawasawa.’ (uk 20). Watanzania wengi ni wanachama au mashabiki katika vyama mbalimbali vya siasa hapa nchini lakini ukiviangalia vyama vya siasa nchini Tanzania kila kukicha ni migogoro na malalamiko badala ya kuwasemea watu, kuwaelekeza, kuwahimiza na kuwaongoza katika kuwajibika, kufanya kazi, kutatua changamoto zinazowakabili na kujiletea maendeleo.

Je, vyama vyetu vinawasemea watu au vinawatumia kama mradi wa kujipatia ruzuku na ada za uanachama kwa maslahi binafsi? Naamini kwamba, viongozi katika vyama vyote hawatimizi wajibu wao ipasavyo, ndio maana wanastahili kutumbuliwa ingawa wanajinadi kwamba wanamuenzi Mwalimu Nyerere.

Kama vyama hivi leo hii ndivyo vingekuwa vinapigania uhuru kutoka kwa mkoloni, hakika uhuru wetu ungechelewa sana ama usingepatikana kabisa. Nia ya dhati ya vyama hivi kuwatumikia watu haipo, ndio maana kuna migogoro isiyokwisha, kuhama hama kwa wanachama kila kukicha, kote huko ni kwa ajili ya kutafuta fursa za kujinufaisha na si kuwatumikia wananchi.

Kazi msingi wa maendeleo

Nne ni hotuba juu ya ‘Malengo ya kazi’ aliyoitoa katika ufunguzi wa kiwanda cha Urafiki, Juni 6, 1968 jijini Dar es Salaam. Mwalimu alihimiza umuhimu wa kufanya kazi ili kujiletea maendeleo kama taifa huru. Alisema: ‘Kila kikundi cha wafanyakazi katika sehemu yao nao wawe na lengo lao: La mwaka, la mwezi na la siku.’ (uk 27). Katika Tanzania ya sasa, ukitaka ukosane na wafanyakazi, pangeni malengo halafu uyasimamie utekelezaji wake. Hapo utakuwa adui na kuitwa kila aina ya majina.

Ugumu anaoupata Rais wetu kwa sasa kupitia falsafa ya Hapa Kazi Tu ni watu kutotimiza malengo ya kazi zao na wengine hawana malengo kabisa. Ndio maana kila anapofanya ziara ya kushtukiza anakuta ni uozo mtupu. Watu wanafanya kazi kimazoea, bora liende. Hatuna haja ya kuihofu serikali ya Hapa Kazi Tu iwapo tunayatambua majukumu yetu na kuyatekeleza ipasavyo. Tunapanga malengo na kuyasimamia.

Maendeleo yawe ni ya watu

Tano ni ‘Uhuru na maendeleo’ hotuba ya mwaka 1968 ambapo Mwalimu alitoa muongozo huu kusisitiza umuhimu wa maendeleo katika taifa huru. Alisema: “Maendeleo maana yake ni maendeleo ya watu. Barabara, majumba, kuongezeka mazao na vitu vingine vya namna hii, siyo maendeleo; ni vyombo vya maendeleo.” (uk. 29).

Katika hili, kuna vyombo vingi vya maendeleo kama migodi ya madini, majengo ya mifuko ya hifadhi, benki, hospitali, shule, mbuga za wanyama, ardhi yenye rutuba, misitu, vyuo vikuu, barabara za lami, umeme, mwanga wa jua, reli, bandari, bahari, anga na rasilimali watu.

Tunapoadhimisha miaka 17 tangu Nyerere kututoka, tutafakari namna ya kuvitumia vyombo hivi vya maendeleo kuinua hali ya maisha ya wananchi, viongozi na raia, tusisubiri kutumbuliwa maana dhamira ya Rais wetu ni maendeleo ya watu. Viongozi na watumishi wa umma na wale binafsi wakifikiria kujinufaisha binafsi watakuwa hawamuenzi Mwalimu Nyerere kivitendo wala kuendana na dhima ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Kujihadhari kutumia mabeberu

Sita, ‘ Amani na mapinduzi ya Afrika’ ni hotuba aliyoitoa Mwalimu katika Chuo Kikuu cha Toronto nchini Canada Oktoba 2, mwaka 1969. Alisema “Lakini serikali imara na amani kwa wananchi vilevile ni mambo muhimu kwa uhuru wetu. Maana bila ya serikali imara nchi za Kiafrika zitaendelea kuwa viwanja vya watu wengine kuchezea’ (uk. 50). Ni ukweli usiopingika kwamba serikali legelege hutoa upenyo wa kunyonywa na mataifa makubwa, kuamriwa kipi wafanye na kipi wasifanye.

Taifa lenye rasilimali nyingi kama Tanzania linapokuwa na serikali imara ni tishio kwa mabeberu. Hakuna upenyo wa kunyonya. Hivyo mabeberu watatumia kila njia ili kudhoofisha serikali ya nchi husika kwa lengo la kupata upenyo wa kunyonya kama walinzi wa amani. Vitatumika vyama vya upinzani, asasi za kiraia na watu binafsi kuzinyong’onyeza serikali imara kwa kisingizio cha ama haki za binadamu au kupingwa kwa demokrasia, tusikubali kulanguliwa.

Afrika kushikamana, kulinda uhuru

Saba ni ‘ Matatizo ya kukataa kufungamana na mataifa makubwa’. Hii ni hotuba aliyoitoa katika mkutano wa matengenezo jijini Dar es Salaam, tarehe 13 mwezi Aprili mwaka 1970. Mwalimu alisema: “Tukiwa kila mmoja na lake, hiyo ndiyo itakuwa hali yetu, na itaendelea kuwa hivyo; Tukiomba na kujipendekeza ili tupate maendeleo kidogo hapa, na rasilimali kidogo pale, na yote kwa masharti yaliyokwisha wekwa na wengine.” (uk. 89).

Umoja, mshikamano wa dhati baina ya mataifa machanga ni muhimu lakini kama taifa pia tunahitaji umoja na mshikamano wa dhati ili kuweza kusimama kama taifa imara. Kama taifa huru hatuhitaji kuchaguliwa adui wala rafiki, na ili hili tulimudu tunapaswa kuzalisha kwa wingi vya kututosha na ziada na kujitegemea, maana misaada itatusababisha kufungamana na upande fulani. Tunapoadhimisha miaka 17 tangu kifo cha Mwalimu Nyerere, tunapaswa tuwe na kauli moja kama taifa pasipokusigana. Hata mashindano yetu ya kisiasa yasitugawe kama taifa ili kuepuka kundi moja kujipendekeza kwa adui ili kujipatia msaada fulani kwa gharama ya taifa. Mfano chama kimoja kikisaidiwa na Marekani, kingine kikasaidiwa na Urusi, ni hatari maana mifungamano hiyo itahatarisha usalama wetu kama taifa kwa maslahi ya mabeberu.

Ili upate huduma lipa kodi

Nane ni ‘Juu ya umuhimu wa kodi’. Hotuba hii ilitolewa redioni kwa ajili ya kuwausia wananchi kabla ya Uchaguzi Mkuu, Oktoba 24, mwaka 1970. Mwalimu alisema: “Kama mtu anaomba sana kuongezwa kwa huduma za jumla, au ziwe nzuri zaidi, basi bila shaka anaomba vilevile kuwa nyinyi wapiga kura muwe tayari kulipa ushuru zaidi au kodi zaidi.” (uk 113). Ni kweli Watanzania tunahitaji huduma bora za jamii katika afya, elimu, usafiri, maji safi na salama, ulinzi, mawasiliano na nyinginezo.

Lakini ili kupatikana kwa huduma hizo lazima tulipe kodi. Na uongozi ni dhamana ya kuwatumikia wananchi katika kuwapatia huduma bora na sio kutumia nafasi hiyo kujinufaisha. Wagombea wa ngazi zote waliahidi kuwaboreshea huduma wapiga kura na kwa kweli hayo ndiyo mahitaji yetu. Ili kuiwezesha serikali kuboresha huduma hizo, ni wajibu wetu kama raia bora kulipa kodi itupasavyo.

Kadri tunavyofurahia huduma bora za jamii na kadri tunavyohitaji maboresho, ndivyo tunavyostahili kuzigharimia kwa njia ya kodi, ushuru au uchangiaji wa gharama. Ulinzi wa miundombinu ya reli, madaraja, maji, umeme, shule, zahanati, hospitali na alama za barabarani ni jukumu letu sote.

Tuvilinde vitu hivi tukitambua bayana kwamba ni kwa ajili yetu na vimetokana na kodi zetu. Uharibifu wowote ule siyo tu kwamba utafifisha huduma hizo bali pia utatuongezea kodi na ushuru ili kukarabati au kurekebisha. Tukilipa kodi, tukafichua wakwepa kodi na ushuru na kulinda miundombinu yetu tutakuwa tumemuenzi Mwalimu Nyerere na kuwasaidia viongozi wetu tuliowachagua katika kutimiza ahadi zao za uchaguzi.

Binadamu wote ni sawa

Tisa ni ‘Binadamu wote ni sawa’ ambapo hapa Mwalimu aliwahutubia walimu na wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Chang’ombe, Agosti 21, 1972. Mwalimu alisema: “Binadamu wote ni sawa, kama hivyo ndivyo basi lazima tukubali kwamba kunyonywa na kuonewa, mahali popote ni kuadhiriwa kwa binadamu wote. Binadamu wote wanapunguzwa utu wao kwa sababu ya uovu huo.” (Uk. 118). Watanzania tunausiwa kuwathamini wanadamu wenzetu na kuwasaidia kuondokana na unyonywaji na uonevu.

Tusikie uchungu na maumivu kwa matatizo ya wanadamu wenzetu na tuwahurumie wenzetu na kuwatatulia kero. Katika Tanzania ya leo kuna matabaka kati ya viongozi na raia, matajiri na masikini, kila mmoja anatumikia na kutetea maslahi ya kundi husika. Kujenga matabaka katika jamii ni kuigawa jamii na kuhatarisha amani yetu kama taifa.

Kwa kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwainua wanyonge, viongozi na watendaji wote wanao wajibu huo wa kumuunga Rais wetu mkono anayetetea usawa wa binadamu kwa kuiunga dhana ya usawa huo iliyoasisiwa na Hayati Mwalimu Nyerere. Kama tunamuenzi Mwalimu Nyerere, tuziunge mkono jitihada za Rais Magufuli kutetea usawa wa binadamu.

Tuepuka ukabila na upendeleo mahali pa kazi kwa kuamini kwamba binadamu wote ni sawa. Ni aibu kukuta kiongozi katika taasisi fulani ya umma, mfano BoT, Takukuru, TRA, Bandari, Tanesco, Posta, NSSF na kwingineko kwamba kwa kuwa kiongozi au mkuu wa kitengo fulani ni kabila fulani basi watu wa kabila lingine hawana fursa ya kufanya kazi katika kitengo hicho au wanafanya kwa kubaguliwa na kunyimwa baadhi ya stahiki zao. Huo sio usawa wa binadamu.

Ujamaa nguvu ya wanyonge Mwisho ni ‘Njia ni moja’, hotuba iliyotolewa katika mkutano mjini Khartoum, Januari 2, 1973. Mwalimu alisema; “Umasikini wetu wa sasa na unyonge wetu unafanya ujamaa uwe ndiyo siasa peke yake tunayoweza kuichagua.” (Uk. 125). Matatizo mengi yanayolikabili taifa kwa sasa ni Watanzania kuwa na roho za kibepari katika nchi ya kijamaa.

Kuficha pesa nchi za nje, wizi wa EPA na Escrow, mikataba tata ya IPTL, Richmond, mikataba batili ya madini, utoroshaji wa wanyama pori hai, mauaji ya tembo, dawa za kulevya, utoroshaji wa makontena bandarini, ufunguzi wa akaunti mbadala za waathirika wa tetemeko, kujilimbikizia mishahara mtu mmoja, uporaji wa ardhi, migogoro ya wafugaji na wakulima, uwepo wa watumishi hewa na vyeti feki, ni matokeo ya fikra na roho za kibepari zenye lengo la kujilimbikizia mali kwa maslahi binafsi.

Huruma kwa wananchi na raia zimetoweka, kila mtu anawaza kuchuma. Ndio maana agizo la kusitishwa kwa safari za nje, semina na warsha mahotelini vimepokewa kwa shingo upande na wanufaika wa mambo hayo. Njia ni moja tu kuepuka kutumbuliwa kwa sababu ya akili na roho za kifisadi nayo ni kuishi kijamaa, kuwahudumia wananchi na kuzisimamia vyema rasilimali za taifa kwa manufaa ya wote.

Tunamuenzi Mwalimu Nyerere lakini kama hatutamuelewa katika kitabu chake; ‘Binadamu na Maendeleo’ tutaendelea kutumbuliwa tu. Njia ni moja tu, nayo ni kubadilika. Maadhimisho ya mwaka huu, yawe chachu ya mwanzo mpya kwa mtu mmoja mmoja na kwa jamii.

Mwandishi wa Makala haya ni mchangiaji wa gazeti hili na Mwalimu wa Shule ya Sekondari Kibaha. Anapatikana kupitia Simu: 0718 495 949. Barua pepe: shageofrey@ yahoo.co.uk

HABARI LEO

No comments: