Mwajuma hana shughuli yoyote ya kumuingizia kipato, zaidi ya kulima vibarua kwa ajili ya kujipatia chakula.
Mama huyo alikuwa ameolewa na Nasoro Abdala (80), ambaye naye haoni. Hata hivyo, miaka michache iliyopita waliachana, hivyo kubaki na mzigo mkubwa wa kuilea familia hiyo, ambapo wanajipatia riziki katika mazingira magumu ya kulima, kuchoma mkaa na kushona mikeka.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini Kibaha, Mwajuma alisema licha ya kuwa na familia hiyo yenye watoto wasioona wakiwemo wajukuu wawili, hana msaada wowote kutoka serikalini, mashirika au watu binafsi.
Watoto wa mama huyo wasioona ni mume wake, Abdala Nasoro na watoto Laila Nasoro (30), Aziza Nasoro (26), Asia Nasoro (21), Kasimu Nasoro (18) na Latifa Nasoro.
Wajukuu zake ni Majidi Maulid (11), anayesoma darasa la 3 mkoani Tanga kwenye Shule ya Wasioona ya Irente; na Tariq ambaye bado ni mdogo akiwa chini ya miaka mitano; na alipopimwa alionekana hana uwezo wa kuona mbali na anahitaji matibabu ili asije kushindwa kuona.
Mwajuma alisema kuwa watoto wake wanne pamoja na wajukuu wawili, hawaoni pamoja na mume wake, ambaye hawaishi pamoja kwa sasa. Alisema anashirikiana na mwanawe mmoja ambaye anaona na mkwe wake, ambao wote hao wanategemea kufanya shughuli za kulima vibarua ili kujitafutia riziki ya kila siku.
Alisema watoto wake, wamekuwa wakipata ulemavu wa kutoona katika mazingira ya ajabu bila kujua sababu. Alisema wamekuwa wakizaliwa wazima, lakini wanapofikia umri fulani, wanapoteza uwezo wa kuona.
“Ninaishi kwenye mazingira magumu mimi na familia yangu, nafikiri kama kungekuwa na watu wanaosaidia, basi wangetupatia misaada ili nasi tuweze kujiendesha, kwani wanangu kama unavyowaona hawaoni na hatuna msaada wowote wa serikali ya mtaa au watu binafsi,” alisema Mwajuma.
Alisema hata nyumba wanayoishi, ni ya ndugu yao na mazingira ni magumu mno, kwani wanahangaika kupata mahitaji, hasa ya chakula ambacho ni muhimu.
“Kweli maisha ni magumu sana, tunashukuru wakati mwingine tunapata msaada kutoka kwenye chama cha watu wasioona wilaya ya Kibaha, wakipata chochote huwa wanatuletea, tunashukuru sana. Kwa upande wa serikali ya mtaa hatupati msaada wowote, hatujui kama kuna misaada inayokuja kwa ajili ya walemavu, hatujui, tunaona kimya tu,” alisema Mwajuma.
Aidha, alisema kuwa familia yao, licha ya kuwa ni kaya maskini, lakini haijawekwa kwenye mradi wa kusaidia kaya maskini, unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) au katika mipango mingine ya kusaidia makundi maalumu.
“Tunaomba wadau mbalimbali watuangalie namna ya kutusaidia, ikiwa ni pamoja na mashirika yanayosaidia walemavu, kwani hali ni ngumu sana ambapo moja ya watoto wangu ambaye ni binti licha ya kuwa haoni, lakini humbidi kulima, kuchoma mkaa na kushona mikeka ili kujipatia kipato lakini naye wanawe wawili hawaoni,” alisema Mwajuma.
Akihojiwa, Mzee Nassoro Abdalla alisema kuwa yeye alianza kupoteza uwezo wa kuona akiwa na miaka 40. Alisema watoto wake aliwazaa wakiwa wazima, lakini walipokuwa wakifikia umri fulani, nao wanapoteza uwezo wa kuona.
Alisema alikuwa akijaribu kuwapeleka hospitali kwa ajili ya matibabu, lakini hakuna mafanikio yaliyopatikana. Alisema licha ya yeye kutokuwa na hiyo familia, lakini maisha wanayoishi ni magumu mno, kuanzia kwenye lishe hadi kwenye masuala ya chakula.
Hivyo, alisema kuna haja ya kupatiwa misaada ya hali na mali ili kuwezesha familia hiyo, nayo kuishi kwenye mazingira mazuri, kama wenzao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa huo, Obed Njile alipoulizwa ni jinsi gani mtaa huo unawashirikisha watu wenye ulemavu, hakuwa tayari kuongelea suala hilo. Alipoulizwa kuhusu familia ya Mwajuma, alisema hawezi kuzungumzia suala la familia hiyo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Wasioona, Rajab Mgoha alisema kuwa wana taarifa na familia hiyo na wamekuwa wakisaidia pale wanapopata misaada kutoka kwa watu mbalimbali, lakini misadaa hiyo ni michache.
Mgoha alisema kuwa viongozi wengi wa serikali za mitaa, wamekuwa hawawathamini watu wenye ulemavu, kwani baadhi hawajui hata idadi ya watu wenye ulemavu, hivyo inakuwa ni vigumu kuwashirikisha kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo. Alisema chama hicho kina wanachama zaidi ya 300.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment