Raundi ya Pili ya Duru la Kwanza ya Ligi Kuu ya Taifa ya Wanawake itaendela kesho Jumanne kwa mchezo mmoja tu, wa Panama ya Iringa kuwa wageni wa timu ya Marsh Academy kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Lakini, wakati mchezo huo Na. 5 wa Kundi B, ukifanyika michezo mingine mitano ya raundi ya pili ikiwamo mitatu ya Kundi A, imebidi iahirishwe na itapangiwa tarehe nyingine. Sababu kubwa ya kuahirishwa kwa michezo hiyo ni uwingi wa wachezaji kutoka timu zinazoshiriki ligi hiyo kujumuishwa kwenye timu ya taifa ya Wanawake – Twiga Stars.
Kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo, michezo ya Kundi B iliyoahirishwa ni kati ya Majengo Women ya Singida iliyokuwa icheza na Baobab ya Dodoma kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida wakati mechi nyingine ni kati ya Victoria Queens ya Kegera iliyokuwa icheze na Sisters ya Kigoma – mchezo ulipangwa kufanyika Uwanja wa Katiba mjini Bukoba.
Michezo ya Kundi A iliyoahirishwa ni kati ya Fair Play ya Tanga iliyokuwa iikaribishe Mburahati Queens ya Dar es Salaam kesho Novemba 8, 2016 kwenye Uwanja wa Mkwakwani ilihali michezo mingine iliyoahirishwa ni ya Novemba 9, ambako JKT Queens ya Dar es Salaam ilikuwa icheze na Viva Queens kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wakati Evergreen Queens na Mlandizi zilikuwa zitumie Uwanja wa Karume, Ilala kucheza mechi yao hiyo.
MECHI TATU ZA LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA BARA
Zile mechi tatu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara za raundi ya Nane Duru la Kwanza, sasa zitafanyika Jumatano.
Michezo hiyo inahusisha timu za Mwadui ya Shinyanga na Azam FC ambayo ilipewa jina la Mechi Na. 57 itachezwa Uwanja wa CCM Kambarage wakati Simba itasafiri hadi Mbeya kucheza na Tanzania Prisons katika mchezon Na. 60 Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine ilihali Young Africans ya Dar es Salaam itakuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting Uwanja wa Uhuru jijini katika mchezo Na.59.
Mechi zilipangiwa ratiba, lakini tarehe zake hazikupangwa (TBA). Tayari Bodi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), imewasiliana na wahusika kuhusu mabadiliko hayo. Sababu ya kuvuta nyuma michezo hiyo ni kutoa nafasi ya maandalizi ya kambi ya timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayotarajiwa kusafiri Ijumaa wiki hii kwenda Harare Zimbabwe kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa unaotarajiwa kufanyika Novemba 13, maka huu.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
No comments:
Post a Comment