ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 7, 2016

MAULIDI YA MTUME MUHAMMAD ( SWA ) KUFANYIKA MNAMO DISEMBA 11

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akizungumza na Ujumbe wa Kamati Tendaji ya Milade Nabii iliyofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kumualika Sherehe za Maulidi ya uzawa wa Mtume Muhammad {SAW } yanayotarajiwa kufanyika Tarehe 11 Disemba.
Kushoto ya Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Kamati Tendaji hiyo ya Milade Nabii Sheikh Sheraly Shamsi na wa kwanza kutoka kulia ni Sheikh Hamad.
Wa kwanza kutoka kushoto ni Wajumbe wa Kamati hiyo Sheikh Ali na Sheikh Kassim Haidar.
Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Milade Nabii Sheikh Sheraly Shamsi akifafanua jambo wakati Kamati yake ilipofika kwa Balozi Seif kumualika ushiriki wa sherehe za Maulidi ya Uzawa wa Mtume Muhammad {SAW .
 

Picha na – OMPR – ZNZ.
Sherehe za Maulidi ya Uzawa wa Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Ulimwenguni Mtume Muhammad {SWA } Kitaifa zinatarajiwa kufanyika Mnamo Mwezi 11 Mfunguo Sita kutegemea kuandama kwa Mwezi sawa na Tarehe 11 Disemba mwaka huu wa 2016.

Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Jumuiya ya Milade Nabii Zanzibar Sheikh Sheraly Shamsi alieleza hayo wakati akiuongoza Ujumbe Wanne wa Viongozi wa Kamati hiyo kutoa mualiko wa Maulidi hayo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Seikh Sheraly Shamsi alimueleza Balozi Seif kwamba yapo mabadiliko kidogo katika maandalizi ya Maulidi kwa upande wa washiriki wa mwaka huu uliotoa fursa pana zaidi katika ushiriki wa madrasa katika kupata Qasida mchanganyiko pamoja na wasomaji wa Tajwid kutoka Wilaya zote za Unguja na Pemba.

Alisema Wajumbe wa Kamati Tendaji ya Milade Nabii walipata kazi kubwa katika kufanya mchujo wa Vijana walioandaliwa kushiriki kwenye Maulid hayo katika usomaji wa Tajwid na Qasida kazi iliyoanza tokea mwezi mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Hata hivyo Mwenyekiti huyo wa Kamati tendaji ya Milade Nabii alisema yapo malalamiko yaliyojitokeza kwa baadhi ya washiriki wa maandalizi hayo, lakini wajumbe wa Kamati yake muda wote walikuwa makini katika kufanya mchujo huo uliokwenda kwa kuzingatia haki ya kila mshiriki.

Sheikh Sheraly alimuhakikisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba maandalizi ya sherehe hizo yameanza kwa mafanikio makubwa na washiriki wa maulidi hayo katika makundi ya Madrasa na wanafunzi wa Tajwid kutoka Kisiwani Pemba wamepangiwa utaratibu maalum wa kuwasili Unguja.


Naye Mjumbe wa Kamati hiyo Sheikh Kassim Haidar Jabir aliishukuru na kuipongeza Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kupitia Idara yake ya Sherehe na Mapambo kwa msaada mkubwa inayotoa katika kufanikisha Sherehe hizo muhimu.

Sheikh Haidar alisema Idara ya Sherehe na Mapambo ni mshirika mkuu wa Kamati Tendaji ya Milade Nabii jambo ambalo uungaji wake mkono umekuwa ukiirahisishia kazi Kamtio hiyo katika maandalizi ya kufanyika kwa Maulidi hayo ifikapo Mfunguo Sita ya Kila mwaka.

Akitoa shukrani zake kwa mualiko wa Maulidi hayo ya Mwaka huu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliipongeza Kamati Tendaji hiyo pamoja na Waumini wote wa Dini ya Kiislamu Nchini kwa jitihada wanazoendelea kuchukuwa za kufanikisha sherehe hizo.

Balozi Seif alisema Jamii imekuwa ikishuhudia harakari za maandilizi ya sherehe hizo zikiendelea katika maeneo mbali mbali Nchini bila ya kutokea hitilafu zozote tokea kuanza kwake miaka mingi iliyopita.

Sherehe za Maulidi ya uzawa wa Mtume Muhammad {SAW } Kitaifa zimekuwa zikifanyika ifikapo Mwezi 11 Mfunguo Sita ya Kila mwaka hapa Nchini na kushirikisha Waumini wa Dini ya Kiislamu kutoka sehemu mbali mbali ya Visiwa hivi na nje ya Zanzibar.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
7/11/2016.

No comments: