Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilosa Bw. Kessy Juma akitoa maoni yake katika warsha hiyo
Halmashauri ya wilaya ya Kilosa imeweka dhamira ya kuchukua hatua muhimu ya kuingiza masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika mipango na bajeti zao ikiwa ni hatua madhubuti za kkabiliana na athari za janga hilo katika maendeleo ya wilaya na taifa kwa ujumla
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa Wilaya ya Kilosa Bwana Kessy Juma wakati akifunga warsha ya wadau mbalimbali wa maendeleo ulioandaliwa na shirika la FORUMCC na kuwashirikisha maafisa kutoka Halmashauri ya Kilosa, asasi za kiraia, wakulima, wafugaji, na waandishi wa habari.
“Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakiathiri sana wilaya ya Kilosa na mkoa wa Morogoro hususani katika sekta ya kilimo japokuwa mkoa huo ni ghala la taifa” anasema Juma.
Warsha hiyo ilikuwa na lengo kutoa fursa kwa wadau kujadili namna gani wanaweza kushawishi na kujumuisha masuala ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika mipango na bajeti baada ya kupata maelezo ya utafiti uliofanywa na forumcc mwaka 2015 kutathmini kiasi cha fedha kilichotengwa na matumizi katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi
Mkurugenzi wa FORUMCC, Rebecca Muna anasema kutokana na changamoto hizo na matokeo ya utafiti walioufanya, shirika hilo liliamua kutengeza kitini ambacho kitatumika kama nyenzo kwa watendaji wa serikali na asasi za kiraia katika kujumuisha masuala ya kukabiliana na mabadiliko ya tabainchi katika mipango na bajeti. Kitini hicho kinaonesha namna mchakato huo unaweza kufanyika kwa njia rahisi na yenye ufanisi.
Kwa kuzingatia umuhimu wa suala la mabadiliko ya tabianchi halmashauri hiyo ilizindua ‘Jukwaa la Mafunzo’ kwa wadau mbalimbali likilenga kuwaleta wadau pamoja kwa ajili ya kujifunza na kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika maeneo yao husika ambalo litajumuisha wadau kutoka serikali, viongozi wa kuchaguliwa, asasi za kiraia, wakulima, wafugaji, taasisi za kidini, na vyombo vya habari.
Wadau wengine pia walieleza namna athari za mabadiliko ya tabianchi yalivyoathiri kazi zao na changamoto wanazokabiliana nazo kupambana na athari hizo ambazo ni pamoja na kuongezeka kwa joto, upungufu wa mvua, kupungua kwa uhakika wa chakula, pamoja na migogoro ya mara kwa mara ya wakulima na wafugaji.
No comments:
Post a Comment