KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa Fanja FC, Mrisho Ngassa, rasmi amesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea Mbeya City kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.
Ngassa aliyewahi kuichezea Simba, Yanga na Azam FC kwenye misimu tofauti, juzi usiku alikamilisha idadi ya wachezaji wapya kumi waliosajiliwa na timu hiyo katika usajili wa dirisha dogo.
Usajili huo umewashtua wadau wengi ambao hawakutarajia kiungo huyo wa zamani wa Yanga, Simba na Azam kusaini Mbeya City akitokea kucheza soka la kulipwa Oman.
Usajili huo ni mapendekezo ya Kocha Mkuu wa City, raia wa Malawi, Kinnah Phiri, aliyewahi kuwa naye kwenye Klabu ya Free States ya Afrika Kusini.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Phiri alisema wameingia makubaliano mazuri na kiungo huyo kusaini baada ya pande zote mbili kufikia muafaka na kusaini.
Phiri alisema ujio wa kiungo huyo utaimarisha kikosi chake kwenye mzunguko wa pili kutokana na kiwango kikubwa alichonacho.
“Ngassa tumefikia naye makubaliano mazuri ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja.
“Tofauti na Ngassa tuliyemkabidhi jezi namba 10, timu yetu imefanikiwa kuwasajili wachezaji wengine tisa wapya akiwemo Juma Seif (Kijiko) ambaye naye amesaini mkataba wa mwaka mmoja,” alisema Phiri na kuongeza:
“Wachezaji wengine wapya ni Hood Mayanja, Tito Okello, Zahor Pazzi, Hussein Salum, Otong William, Raphael Bryson, Daniel Joram, Sameer Abeid na Majaliwa Mbanga.”
Kocha huyo aliwataja wachezaji walioachwa kuwa ni Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Meshack Samwel, Peter Mwangosi, Michael Kerenge, Mackyada Franco, Issa Nelson, Salvatory Nkulula, Hemedy Murutabose na Joseph Mahundi aliyemaliza mkataba wake.
GPL
No comments:
Post a Comment