ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 15, 2016

Polisi wapekua ofisi za JamiiForums

Mkurugenzi wa mtandao wa kijamii wa\
By Muyonga Jumanne, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Siku moja baada ya kumuweka rumande mkurugenzi wa mtandao wa kijamii wa JamiiForums, Polisi jana walienda kupekua ofisi za kampuni inayoendesha mtandao huo ya Jamii Media.

Baada ya upekuzi huo, inadaiwa kuwa waliondoka na nyaraka za usajili wa Jamii Media na leseni ya biashara.

Mkurugenzi huyo, Maxence Melo alikamatwa juzi baada ya kuitwa kituo kikuu cha polisi na kwenda akiambatana na wafanyakazi wa kampuni hiyo, ambao baadaye waliambiwa waondoke huku yeye akiwekwa ndani.

Mmoja wa maofisa wa kampuni hiyo, Simon Mkina aliiambia Mwananchi kuwa polisi walifika ofisi zao zilizopo Mtaa wa Taasisi, Mikocheni jijini hapa saa tisa alasiri wakiwa na Melo na baada ya kumaliza upekuzi walienda nyumbani kwake kisha kurudi kituo kikuu cha polisi saa 12:15 jioni. “Walipofika ofisini baada ya upekuzi wameondoka na nyaraka za usajili, cheti cha Kodi ya Ongezeko la Thamani (Vat) na leseni ya biashara,” alisema Mkina.

Mkina, ambaye pia ni mwanaharakati anayetetea uhuru wa mawasiliano, alisema mbali na kuchukua nyaraka hizo, waliwahoji wafanyakazi wa kampuni kisha kuondoka na Melo na alipofika kituoni hapo walipewa taarifa kuwa atahojiwa kwa kuwa tangu ashikiliwe na polisi hakuwahi kuhojiwa.

Mmoja ya waanzilishi wa JamiiForums, Mike Mushi alisema utaratibu wa kupata dhamana leo (jana) usingewezekana kwa kuwa hakuna shtaka lililofunguliwa dhidi ya Melo hadi sasa.

“Taratibu zote zilizofanyika leo hazijafuata sheria kuanzia kumtoa kwenda ofisini na nyumbani kwake mpaka anaporudishwa. Bado tunazidi kufuatilia kujua hatima ni nini,” alisema Mushi.

Melo anadaiwa kushindwa au kukataa kutoa ushirikiano kwa polisi pale wanapohitaji kupewa taarifa za wachangiaji wa mtandao wa JamiiForums na alipokamatwa juzi alinyimwa dhamana kwa maelekezo kuwa amri ilitolewa kuwa alale kituoni hapo hadi jana.

Machi 4, Jamii Media, inayoendesha mitandao ya JamiiForums.com na Fikrapevu.com, ilitoa tamko la kupinga sheria ya zinazokandamiza haki ya Watanzania wanaotumia mtandao na ilidai kuwa ilifikia hatua hiyo baada ya kushinikizwa na polisi kutoa taarifa za wateja wanaowapa taarifa.

Baada ya kumtafuta Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi. Simon Sirro bila mafanikio, Mwananchi ilimpata Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba ambaye alisema hawezi kuzungumzia matukio bali sera tu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Suzan Kaganda alisema hana taarifa za kukamatwa kwa mkurugenzi wa JamiiForums, wala ofisi yake kupekuliwa. “Nashangaa tangu jana mnaniambia mara mkurugenzi kakamatwa mara nini, mimi sina huyo mtu hapa na wala sijui chochote,” alisema.

No comments: