ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, December 15, 2016

Saa tatu za ushahidi wa aliyetobolewa macho

By Hadija Jumanne, Mwananchi hjumanne@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kijana Said Mrisho (34) anayedaiwa kutobolewa macho na Salum Njwete (34), jana alitoa ushahidi kwa saa tatu mahakamani akieleza jinsi tukio hilo lilivyotokea hadi akapoteza uwezo wa kuona.

Mrisho alidai hayo wakati akitoa ushahidi katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala jinsi Njwete anayetuhumiwa katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha alivyomjeruhi kwa kumchoma visu mara tatu begani, mara nne tumboni na mara nne machoni.

Mrisho ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, alieleza hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Flora Haule.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Nassoro Katuga kutoa ushahidi, Mrisho alitoa ushahidi namna alivyotobolewa macho na ambavyo hakupata msaada kutoka kwa waliokuwapo katika eneo la tukio.

Shahidi huyo alidai kuwa siku ya tukio, Septemba 6, 2016 asubuhi alitoka nyumbani kwake eneo la Makuburi na kwenda katika saluni anayoisimamia iliyopo eneo la Sanene, Tabata Segerea.

“Mimi kazi yangu ni kinyozi lakini pia nasimamia saluni mbili zilizopo Tabata Segerea eneo la Sanene na saluni ninayofanyia kazi inaitwa Rodgers,” alisema Mrisho ambaye alikuwa amevalia kanzu ya njano na kibaraghashia chenye rangi nyeusi.

Mrisho alidai baada ya kufika katika saluni aliendelea na kazi zake hadi ilipofika saa nne usiku alipofunga saluni.

“Baada ya kufunga saluni nilielekea katika kituo cha daladala, lakini wakati nikiwa eneo hilo kulikuwa hakuna daladala zinazoelekea Ubungo kwa wakati huo.

“Nikiwa hapo kituo cha daladala Tabata Sanene, ilipita bajaji na kuniuliza ninapoenda na mimi nikamwambia kuwa nakwenda Ubungo,” alidai.

Aliendelea kueleza kuwa dereva wa bajaji alimwambia apande bajaji hadi Tabata Relini ili akaunganishe magari ya Ubungo kwa sababu bajaji ile ilikuwa inaeleka Buguruni Sheli kuegesha.

“Kutokana na usafiri siku ile kuwa mgumu, ilibidi nikubaliane naye anisogeze hadi Tabata Relini ili niunganishe magari ya Ubungo ambayo yanatokea Buguruni na katika bajaji ile nilikuwa peke yangu,” alidai.

Alidia kuwa wakati akiwa katika bajaji, aliona dereva anabadili uelekeo kwa kuelekea barabara ya Vingunguti badala ya Tabata Relini na ndipo alipomuuliza dereva huyo kwa nini amebadilisha njia?

“Nilimuuliza, mbona tunaacha njia ya kuelekea Tabata Relini tunapita hii ya Vingunguti? Yule dereva wa bajaji alinijibu kuwa kule Relini ni mbali na bajaji yake haikuwa na mafuta, hivyo njia ya Vingunguti ingekuwa rahisi,” aliongeza.

Kutokana na maelezo ya dereva huyo na jinsi alivyokuwa analia hali ngumu, ilibidi akubali na walipofika Buguruni Sheli alimlipa nauli ya Sh1,000.

Alidai wakati anashuka Buguruni Sheli ilikuwa saa 4: 40 usiku na eneo hilo lilikuwa limechangamka kama mchana, hali iliyomvutia kununua kuku aipelekee familia yake.

“Nilichagua kuku mmoja na kumuomba muuzaji anipunguzie bei kutoka Sh7,000 hadi Sh6,000 na wakati nasubiri kuku wangu akaushwe kwenye mafuta, alikuja mwanaume mmoja akasimama nyuma yangu upande wa kulia na akaniambia brother (kaka) nina shida naomba unisaidie,” alieleza.

Mrisho alidai kuwa baada ya kuambia hivyo na mtu huyo “ambaye alikuwa amepanda hewani akiwa na mwili wa mazoezi”, alimwambia aongee shida yake kama ataweza kumsaidia kama hataweza basi.

Shahidi huyo alisema baada ya kumwambia hivyo, alimuona mtu huyo anarudi nyuma huku akiwa ameshikilia funguo mkononi na kibegi kidogo na wakati akiendelea kuongea na muuza kuku, ghafla alimuona mtu huyo anamchoma kisu bega la kushoto.

“Kabla sijageuka niliona tena ananichoma kisu cha pili na cha tatu haraka haraka begani na hapo nilianguka chini na wakati nikiwa chini, alinikanyaga na kuanza kunikatia cheni yangu ya silva (rangi ya fedha) niliyokuwa nimevaa shingoni na mkononi,” alidai.

Mrisho aliongeza kuwa baada ya kuanguka chini, mshtakiwa huyo aliinama na kuanza kumpekua na kumchukulia pochi iliyokuwa na Sh300,000 na wakati vitendo hivyo vinafanyika yeye alikuwa anapiga kelele za kuomba msaada bila mafanikio.

“Nilishangazwa sana na kitendo cha mimi kuchomwa visu huku watu wakiangalia. Niliomba msaada watu wanisaidie lakini mshtakiwa alijibu kwa sauti kuwa hakuna mtu atakayenisaidia,” alieleza shahidi huyo huku akitumia kitambaa kufutia macho kila wakati.

Alidai wakati akiwa chini, alisikia mmoja wa wauza kuku akiwaambia mwenzake kuwa “Scorpion ameshaua mtu”.

“Nikiwa chini huku damu ikitoka, nilisikia watu waliokuwa karibu na eneo hilo wakimwambia mshtakiwa muachie hizo simu ili ndugu zake wakimtafuta wajue yupo wapi, maana hapo ameshakufa,” aliongeza.

Mrisho alidai baada ya mtu huyo kusema hivyo, aliona mshtakiwa akimfuata yule kijana aliyetoa ushauri na kumpiga na baadaye kumrudia yeye (Mrisho) na kuanza kumvuta kuelekea barabarani katika makutano ya barabara ya Mandela na Uhuru, alipomuacha kwa takriban dakika 30.

“Alinivua fulana yangu niliyokuwa nimevaa na kuniweka katikati ya barabara na kuruhusu magari yanikanyage, lakini magari kila yalipokuwa yakikaribia eneo langu yalisimama na kurudi nyuma na kisha kupita upande mwingine,” alidai.

Alidai baada ya kuona hagongwi na gari, mshtakiwa huyo alimtoa barabarani na kumuweka pembeni mwa barabara na kisha kumtoboa macho mara nne kwa kutumia kisu.

“Nilivyotobolewa macho hapo sikuweza kuona nini kinachoendelea kwa sababu nilipoteza fahamu, nilikuja kuzinduka baadaye baada ya msamaria kuniuliza kama nina namba za ndugu zangu ili awapigie,” alidai.

Alidai baada ya hapo alipelekewa Kituo cha Polisi Buguruni ambako alipewa fomu namba tatu na kupelekwa Hospitali ya Amana huko alikutana na ndugu zake akiwamo mkewe na usiku huo alihamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

“Nimefanyiwa upasuaji mara mbili na nililazwa siku sita. Daktari wangu wa macho alivyonipima alisema macho yangu yameshaharibika, siwezi kuona tena,” alidai.

Akiwa mahakamani hapo, Mrisho alivua kanzu aliyokuwa amevaa ili kuionyesha mahakama majeraha aliyoyapata baada ya kujeruhiwa kwa visu.

Mrisho aliiambia mahakama kuwa kwa sasa hawezi kuona kitu chochote wala hawezi kumtambua mshtakiwa kwa sababu ameshakuwa kipofu.

Shahidi huyo alipomaliza ilifika zamu ya upande wa utetezi ya kuhoji ambapo Wakili Juma Nassoro anayemtetea mshitakiwa Njwete, alimueleza shahidi huyo ambaye ndiye mlalamikaji kwamba siku ya tukio alikuwa amekwenda Buguruni kununua vitu vya wizi.

Nassoro aliendelea kuhoji kwamba sababu za Mrisho kutopata msaada kutoka kwa wananchi wakati akichomwa visu begani, tumboni na machoni ni kwa vile alikwenda Buguruni kununua vifaa vya simu vya wizi.

Mrisho akijibu hoja hiyo alidai yeye siyo mwizi, wala hajawahi kukamatwa kwa kosa la wizi.

“Sijawahi kununua simu yoyote mkononi mwa mtu wala mimi siyo mwizi, wala sijawahi kufanya biashara na mtu yoyote,” alifafanua huku akisisitiza safari yake ya Buguruni ilitokana na ombi la dereva wa bajaji aliyoikodi.

Hali ilivyokuwa mahakamani

Kesi hiyo ilihudhuriwa na watu wengi na chumba cha awali kilichopangwa kusikilizwa hakikutosha, hali iliyolazimu kuhamishiwa sehemu nyingine yenye nafasi.

Pia, ulinzi uliimarishwa na watu walikuwa watulivu wakifuatilia ushahidi uliokuwa ukitolewa na shahidi huyo.

Kesi hiyo itaendelea katika hatua ya ushahidi wa upande wa mashtaka Desemba 28,

No comments: