ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, January 26, 2017

Afungwa miezi sita kwa kuiba mtoto

By Mwanja Ibadi, Mwananchi

Lindi. Mkazi wa mtaa Tulieni katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Fatuma Rashidi(32) amehukumiwa kifungo cha nje miezi sita, baada ya kupatikana na hatia ya kuiba mtoto mchanga wa wifi yake mwenye umri wa wiki mbili.
Hukumu hiyo imetolewa leo na hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya hiyo, Mussa Ngaru baada ya kuridhishwa na ushahidi uliokuwa umetolewa na upande wa mashtaka.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, mshtakiwa alipewa nafasi ya kujitetea, ambapo aliiomba Mahakama imuonee huruma kwa madai ni mkosaji wa mara ya kwanza na ana wazazi wanaomtegemea.

Mwanasheria wa Serikali, Rabia Ramadhani kwa upande wake aliiomba Mahakama kupatia adhabu kali mshitakiwa huyo ili iwe fundisho kwake na wanawake wengine walio na tabia ya aina hiyo.

Hakimu Ngaru akitoa hukumu katika kesi hiyo namba 141/2016, chini ya kifungu cha 169 kifungu kidogo cha 1 (a) Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, alimuhukumu kifungo cha nje miezi sita kwa masharti ya kutotenda kosa ndani ya kipindi hicho.

No comments: