ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 13, 2017

DKT. MGWATU AWAAGIZA WATUMISHI KUZIBA MIANYA YA UVUJAJI MAPATO VIVUKO VYA KIGONGO-BUSISI

 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu akijibu swali la mmoja wa wafanyakazi wa vivuko vya Kigongo/ Busisi wakati alipokua akisikiliza changamoto na kero zinazowakabili wafanyakazi wa vivuko hivyo. Pembeni yake ni Meneja wa TEMESA Mkoa wa Mwanza Mhandisi Ferdinand Mishamo.
 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu akimsikiliza mtaalamu wa mifumo ya kompyuta katika kitengo cha TEHAMA (ICT) Msese Mgini alipokua katika ziara yake katika vivuko vya Kigongo / Busisi mkoani Mwanza.
  Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Dokta Mussa Mgwatu akisisitiza jambo wakati akizungumza na wafanyakazi wa vivuko vya Kigongo Busisi vinavyomilikiwa na TEMESA mkoani Mwanza wakati wa kikao chake na wafanyakazi hao. Kushoto kwake ni Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Mkoa wa Mwanza Mhandisi Ferdinand Mishamo, Mhandisi Michael Myaka na Mkuu wa vivuko Atiki Abdalah.
 Wafanyakazi wa Vivuko vya Kigongo-Busisi vinavyomilikiwa na Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Mkoa wa Mwanza wakimsikiliza Dkt. Mussa Mgwatu hayupo pichani wakati alipokua akizungumza nao kuhusiana na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika mazingira ya kazi zao kivukoni hapo.
 Mmoja wa Manahodha wa vivuko vinavyotoa huduma kati ya Kigongo na Busisi Kelvin Willy akimuuliza swali Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu (hayupo pichani) wakati alipokua akisikiliza kero za wafanyakazi hao kivukoni hapo.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Dkt. Mussa Mgwatu aliyeshika kitabu akiagana na baadhi ya watumishi wa vivuko vinavyotoa huduma kati ya Kigongo-Busisi mara baada ya kumaliza kikao na watumishi hao jijini Mwanza.Picha zote na  Alfred Mgweno - TEMESA

Na Alfred Mgweno - TEMESA, Mwanza
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu amefanya ziara katika vivuko vya Kigongo/Busisi mkoani Mwanza vinavyosimamiwa na Wakala huo na kujionea utendaji kazi wake. Akiongea na watumishi wa vivuko hivyo baada ya kutembelea na kukagua miundombinu yake, Dkt. Mgwatu aliwataka watumishi hao kuongeza bidii ya kazi na kuziba mianya ya uvujaji wa mapato ili kuhakikisha kuwa mapato yanayopatikana ni halisi.
Katika ziara hiyo Dkt. Mgwatu alitembelea pia chumba maalumu cha mifumo ya TEHAMA inayosimamia ukataji na utumiaji wa tiketi na kujionea jinsi inavyofanya kazi. Aliwataka wataalamu wa kitengo hicho kujiridhisha kama mifumo hiyo inafanya kazi ipasavyo na wala haitoi mwanya wa kuhujumu mapato. Alisema “tunafanya uhakiki wa matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika kituo hiki na ikibainika mifumo hiyo imechezewa tutachukua hatua kali”.
Awali katika kikao hicho na watumishi, Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Mkoa wa Mwanza Mhandisi Ferdinand Mishamo alimuelezea Mtendaji Mkuu changamoto mbalimbali ambazo wanakumbana nazo katika utendaji kazi kituoni hapo ikiwa ni pamoja na uchakavu wa vivuko, ukosefu wa usafiri kwa watumishi na upungufu wa wafanyakazi wa kada za unahodha na ubaharia.
Dkt. Mgwatu alikuwa mkoani Mwanza kwa ajili ya kujionea utendaji kazi wa vivuko vya MV Misungwi, MV Sengerema na MV Sabasaba ambavyo vyote vinatoa huduma kati ya Kigongo na Busisi wilayani Misungwi.

No comments: