Na ASHA BANI
-DAR ES SALAAM
SIKU chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kukabidhiwa ripoti ya pili ya kuchunguza mchanga wa dhahabu wa Kampuni ya Madini ya Acacia, wananchi wa Tarime wamevamia mgodi wa North Mara kwa siku mbili mfululizo.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni mwendelezo wa kupinga uonevu unaofanywa na wawekezaji hao kupitia Kampuni ya Acacia.
Taarifa kutoka wilayani Tarime ziliambia MTANZANIA kuwa wananchi hao walivamia mgodi huo juzi saa 2.00 usiku na jana asubuhi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, wananchi hao walikwenda hadi kwenye mtambo wa kufua dhahabu na kufanya uharibifu huo.
Hata hivyo shuhuda huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema vurugu hizo zimetokana na uongozi wa Kampuni ya Acacia kushindwa kuwalipa fidia wananchi waliokuwa na maeneo yao tangu awali.
Alisema wakati madini yalipogundulika, wananchi walioondolewa walitathiminiwa mali zao yakiwamo mashamba, nyumba na kuahidiwa kulipwa fidia akini hadi sasa hawajalipwa stahiki zao.
Alisema kwa siku mbili mfululizo wanachi wenye madai yao walifika katika ofisi za kampuni na kuona baadhi ya majina ya wanaotakiwa kulipwa fidia yakiwa yamebandikwa katika ubao wa matangazo lakini majina ya wengine yakiwa hayajabandikwa.
“Wale ambao hawakuona majina yao walichukuana na kuvamia mtambo wa kfua madini na kuondoka na mawe ambayo tunahisi mengine yana dhahabu.
“Lakini polisi walifika na kuwatawanya na mabomu ya machozi,’’ kilisema chanzo cha habari hiyo.
Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga, alisema alikuwa kwenye kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya ingawa aliahidi kuzungumza na waandishi wa habari leo.
“Nimesema hivi, siwezi kuzungumza lolote, sina cha kuzungumza na siwezi kuzungumza na mwandishi hadi hapo tutakapokaa kikao kesho (leo) ndiyo nitasema,’’alisema Luoga.
MTANZANIA ilipomtafuta Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) kujua kama hatua ya wananchi hao inatokana na kauli yake aliyoitoa bungeni hivi karibuni kuwa atawaongoza wananchi kuwaondoa Acacia kwa kuwa wamekuwa wakiwaibia kama ilivyoelezwa kwenye ripoti ya Tume ya Rais Magufuli, alisema kwa sasa yupo Dodoma kwa ajili ya vikao vya Bunge .
Alisema anachojua ni kuwa wananchi hao wamekuwa wakidai malipo yao kwa muda mrefu.
“Wananchi wamekuwa na malalamiko wakidai malipo yao na tayari mgodi umeshaleta madhara mengi, hilo naweza kusema lakini mengine zaidi ya hayo siwezi kuyajua,’’ alisema Heche.
Juni 12, mwaka huu, Rais John Magufuli alipokea ripoti ya pili iliyoongozwa na wanasheria na wachumi, iliyochunguza mchanga wa madini. Kamati hiyo iliteuliwa Aprili 10 mwaka huu.
Mwenyekiti kamati hiyo alikuwa Profesa Nehemiah Osoro na ilikuwa na hadidu za rejea mbalimbali.
Profesa Osoro alisema katika ripoti hiyo kuwa Kampuni ya Madini ya ACACIA haina usajili nchini
Pamoja na mambo mengine, Kamati ilibaini kuwa makontena 44,277 ya mchanga wa madini, kwa kiwango cha chini, yalisafirishwa nje ya nchi kati ya 1998 na 2017.
Kamati hiyo pia ilieleza kuwa kampuni hiyo ilikwepa kulipa kodi ya zaidi ya Sh trilioni 100 katika kipindi hicho.
Machi mwaka huu, Serikali ilizuia makontena zaidi ya 200 kwenye Bandari ya Dar es Salaam kuchunguza mchanga wa madini ambao ulikuwa unasafirishwa nje ya nchi kuchenjuliwa.
Mchanga huo ulikuwa ni mali ya Acacia, ambayo ni kampuni mshirika wa Barrick Gold Corporation.
Baada ya zuio la mchanga huo, Rais Magufuli aliteua kamati mbili kuchunguza mchanga huo na kamati ya kwanza iliyokuwa inaundwa na wanasayansi, ilibaini kiasi kikubwa cha madini ambayo yamekuwa yakiibwa.
Kamati ya pili iliyoundwa na wachumi na wanasheria, ilibaini zaidi ya Sh trilioni 100 zimeibwa kupitia usafirishaji wa makinikia, huku sheria nyingi za madini zikikutwa na kasoro inayotoa upenyo wa wawekezaji kutorosha madini.
Baada ya ripoti ya pili kuwasilishwa, Mwenyekiti wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ambayo ina asilimia 64 katika Kampuni ya Acacia Mining Limited, , Profesa John Thornton, alikuja nchini na kukutana na Rais Magufuli.
Katika mazungumzo yao walikubaliana kuunda timu za majadiliano kubaini ukweli wa suala hilo.
Timu hizo zitahusisha Serikali ya Tanzania na wawakilishi wa Kampuni ya Barrick
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment