ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 20, 2017

JESHI LA MAGEREZA LILIVYOBEBA DHAMANA YA TANZANIA YA VIWANDA

 Na Christina R. Mwangosi, MOHA 
Jeshi la Magereza nchini ni moja kati ya Majeshi yaliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi yenye jukumu kubwa la msingi la kuwarekebishwa wafungwa wanaohukumiwa kwa makosa mbalimbali hapa nchini. 
Katika taratibu za Urekebishaji wa wafungwa zipo stadi mbalimbali za kilimo, ufundi na uzalishaji ambazo zinatumika  kuwarekebisha  wafungwa ili hata pale wanapomaliza vifungo vyao na kurudi uraiani waweze kutumia ujuzi walioupata katika shughuli za uzalishaji na hivyo kujiletea maendeleo yao binafsi lakini kuchangia pia katika maendeleo ya nchi yetu.
 Mbali na jukumu hilo la msingi la Jeshi hilo, pia Jeshi hili limekuwa likijishughulisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali ikiwemo shughuli za kilimo kwa ajili ya chakula kwa wafungwa, utengenezaji wa samani mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya ofisi na nyumbani, pamoja na utengenezaji wa viatu shughuli zinazofanyika katika Magereza yaliyopo hapa nchini.
Aidha Jeshi la Magereza nchini lina fursa nyingi ambazo zikitumika vizuri zinaweza   kuwa na mchango mkubwa sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu na hivyo kufikia malengo yetu ya kuwa na uchumi wa viwanda. Miongoni mwa fursa hizo ni pamoja na ardhi nyingi yenye rutuba inayofaa kutumika kwa kushughuli za kilimo na matumizi mengineyo ya uzalishaji vikiwemo viwanda.
Kwa muda mrefu sasa jeshi la Magereza limekuwa likitumia kiwanda chake cha Utengenezaji wa Samani mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya Ofisi na hata nyumbani kilichopo katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam.
 Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza ambaye ndiye Mkuu wa Kiwanda cha Samani cha Ukonga cha Jeshi la Magereza nchini kilichopo jijini Dar es Salaam John Itambu anasema  kwa sasa kiwanda hicho kinafanya shughuli kubwa za aina mbili  ikwemo utengenezaji  wa samani mbalimbali  kwa ajili ya matumizi ya ofisini na nyumbani ikiwemo utengenezaji wa meza, viti, makabati,  vitanda,  meza za chakula na za ofisi,  pamoja na meza za chumbani maarufu kama ‘dressing table’.
Kamishna Msaidizi Itambu anasema kiwanda hicho kinatengeneza samani hizo  kwa kutumia mbao za kawaida zile za asili zenye ubora wa kiwango cha juu na zile za henzerani yaani miti ya  minazi ambazo nazo pia zina mvuto wa hali ya juu pia ikiwemo ubora pia. 
Anasema pamoja na utengenezaji wa samani kiwanda hicho pia kimekuwa kikijishughulisha na utengenezaji wa kazi za mikono ikiwemo mazulia, vikapu, ‘table mates’ pamoja na mazulia ya milangoni.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza Itambu ambaye ndiye msimamizi wa shughuli za Kiwanda hicho anasema pamoja na kwamba Kiwanda cha Samani cha Magereza Ukonga kimekuwa kikitengeneza samani zenye ubora wa hali ya juu lakini siku zilizopita kulikuwa na changamoto ya ucheleweshaji wa ‘Oda’  ilikuwa mteja akiagiza samani za aina fulani inachukua muda mrefu kukamilishiwa mahitaji yake wakati mwingine na ubora unakuwa umepunguwa si kwa ubora aliokuwa ameuona kwenye shughuli za Maonyesho ya Sabasaba.
Anasema kwa sasa Kiwanda hicho kimeondoa changamoto hiyo ya ucheleweshwaji na sasa  mteja anapoagiza mahitaji yake ya samani ziwe kwa matumizi ya Ofisi au nyumbani mteja anapata mahitaji yake kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu hakuna tofauti tena ya ubora anaotengenezewa  na ule aliouona kwenye Maonyesho ya SabaSaba.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza John Itambu anasisitiza kuwa changamoto kubwa inayowakabili kwa sasa ni ile ya bei za mbao kwa ajili ya kutengeneza samani zao kupatikana kwa shida kwa kuwa mafundi wengi wa mitaani hununua mbao kwa kutumia fedha taslimu na bila kupewa risiti za EFD sasa pale Jeshi la Magereza linapofuata taratibu za kupewa risiti za EFD  wauzaji wa mbao hutoa kipaumbele kwa mafundi wale wa uraiani wenye fedha taslimu badala ya Magereza, hivyo ni muhimu kwa Mamlaka husika kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kutumia mashine ama risiti za EFD.
‘‘Pamoja na kwamba mara nyingi wateja wanaona bei za bidhaa za kiwanda chetu cha samani ziko juu lakini wataalamu wetu wanachokiangalia ni kuzalisha bidhaa kwa kutumia mbao zenye ubora wa hali ya juu miti hasa ile ya asili, na ndio maana samani zetu zinadumu kwa muda mrefu huwezi kulinganisha ubora wake na bidhaa za mitaani’’ anasisitiza Mkuu wa Kiwanda hicho John Itambu.
Anasema kwa sasa kiwanda kimeanzisha pia kitengo cha Masoko ndani ya Kiwanda chetu cha Samani ambacho kinahusika zaidi na utafutaji wa masoko, pamoja na kusimamia oda zinazotolewa na wateja wa kiwanda hicho ili ziweze kukamilishwa kwa wakati na ubora ule ule waliouona wakati wa Maonyesho ya SabaSaba.
Hata hivyo Kamishna Msaidizi John Itambu anatoa shukrani kubwa kwa Ofisi ya Rais Ikulu ambayo imekuwa ikiunga mkono kiwanda hicho cha samani kwa kununua samani kwa matumizi ya ofisi hiyo, ikiwemo pia ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na Mali Asili na Utalii.
‘‘Pamoja na Serikali kutoa Maelekezo kwa Taasisi zote za Serikali kununua samani kwa ajili ya matumizi ya ofisi kutoka kwenye Kiwanda cha Samani cha Gereza la Ukonga bado muitikio ni mdogo bado hatujapata tenda kubwa kutoka kwenye ofisi za Serikali’’. Anaeleza Mkuu wa Kiwanda hicho Kamishna Msadizi John Itambu.
Anasema mpaka sasa wameshatengeneza samani za Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) pamoja na Ofisi za Bunge  ambao waliotoa oda ya samani kwa ajili ya ofisi za Wabunge kwenye Majimbo yao.
Pamoja utengenezaji wa samani mbalimbali, Kiwanda chetu cha Samani Ukonga Magereza kina kitengo pia kinachojishulisha na ushonaji wa nguo mbalimbali suti na mashati ya wanawake na wanaume, ovaroli pamoja na sare mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya ofisi.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza John Itambu anasema kwa sasa  Kiwanda kina uwezo wa kuzalisha sare za wafungwa 300 kwa siku, hivyo Kiwanda kina uwezo mkubwa wa kupokea tenda kubwa kutoka kwa wateja mbalimbali hapa nchini.
Kamishna Msaidizi Itambu anasema Kiwanda hiki cha Ukonga  miaka mingi iliyopita kilianza na shughuli za ushonaji wa nguo kwa kushona sare za majeshi yaliyopo hapa nchini kwa kutumia wafungwa waliopo waliosimamiwa na Wataalamu waliopo ndani ya Jeshi la Magereza na kwamba awali wazo kuu lilikuwa ni kuwarekebisha wafungwa kwa njia ya kuwafundisha stadi za ushonaji baadae kiliamua kuanzisha na shughuli za utengenezaji wa samani.
‘‘Awali tulikuwa tukishona zaidi sare za Taasisi mbalimbali za Serikali kwa mfano sare za askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, askari wa Jeshi la Uhamiaji, kwa sasa Kitengo hiki kinachojishughulisha na ushonaji wa nguo mbalimbali  kimekuwa kikipata tenda za kushona sare za madereva na makondakta wa daladala pamoja na sare za askari wa Jiji la Dar es Salaam’’. Anasema Kamishna Msaidizi Itambu ambaye ndiye Mkuu wa Kiwanda cha Samani cha Ukonga Magereza Jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Meja Jenerali Projest Rwegasira anasema Kiwanda cha Samani cha Jeshi la Magereza kilichopo Ukonga jijini Dar es Salaam ni moja kati ya  viwanda vya hapa Tanzania vinavyotengeneza samani zenye Ubora wa hali ya juu na ndio maana bidhaa zake zimekuwa zikidumu kwa muda mrefu.
Meja Jenerali Rwegasira anasema yeye binafsi ni miongoni mwa wateja wa Kiwanda hicho cha Ukonga na amekuwa akinufaika na ubora wa samani zinazotengenezwa na Kiwanda hicho kwa kuwa si kwamba zina ubora wa hali ya juu bali pia zinavutia kutokana na wataalamu wake kuwa wabunifu na utaalamu wa kisasa katika utengenezaji wa samani hizo.
Miongoni mwa wateja ambao wamewahi kununua bidhaa hizo kwenye Kiwanda hicho cha Samani cha Ukonga, Johnson Kapeu mkazi wa Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam anasema hivi ‘‘Kwa mara ya kwanza nilihudhuria Maonyesho ya SabaSaba kati ya mwaka 2015 na 2016…nakumbuka nilihudhuria Maonyesho haya kama Mtanzania na Mtumishi wa Umma, Rais Mstaafu Kikwete alipotembelea Banda la Magereza ndipo nami nikapata nafasi ya kuona bidhaa za Magereza kweli nilivutiwa na baada ya hapo niliweka oda yangu nikabahatika kupata samani nilizohitaji kwa wakati huo ilikuwa ni Kitanda, Kabati la Nguo na Vyombo ambavyo hadi sasa ubora wake haujapungua hata kidogo. ’’ anasema Bw. Kapeu.
Kwa upande wake mmoja kati ya wananchi ambao wamewahi kushiriki Maonyesho ya SabaSaba Edson Mandira mkazi wa Ukonga jijini Dar es Salaam anasema “Ni kweli kabisa Jeshi la Magereza linatengeneza bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na ikiwa wataalamu wake watapata fursa za kutembelea Viwanda vya nje na ndani ya nchi wanaweza kujifunza ujuzi mpya hivyo kuongeza ubunifu zaidi ambao utaendana na soko la sasa ama ushindani wa soko la sasa kwa ujumla.
‘‘Mimi binafsi navutiwa sana na ubora wa samani zinazotengenezwa na jeshi letu la Magereza ila wangeongeza ubunifu kidogo tu… sasa ukichanganya na ubora wao wa hali ya juu wanaweza wakatuzidi hata sisi mafundi wa Keko kwa kweli”. anasisitiza huku akicheka Bwana  Gosbert Remanto ambaye ni fundi seremala Keko DDC.  
Kwa upande wake Ally Abdulkarim mfanyabiashara wa samani eneo la Keko DDC anasema “Binafsi naona Samani za kiwanda cha Magereza ni nzuri ila ndugu mwandishi wenzetu hawa wakiongeza ubunifu kwenye “Finishing”  na kuongeza ubunifu wa kisasa … ndugu mwandishi wakifanikiwa hapo tu wenzetu hawa watafika mbali sana na bidhaa zao zitatuacha tu … zitakimbiliwa hapa nchini kwa sababu ya ubora wa hali ya juu,  unajua hawa wenzetu kwenye mbao sio wababaishaji kama sisi huku mtaani. 
Naye Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini, Kamishna Jenerali Dk. Juma Malewa anasema kuwa “Kutokana na Serikali kuhamishia Makao Makuu ya Nchi yetu Mkoani Dodoma  ni wazi kutakuwa na uhitaji mkubwa wa samani kwa ajili ya matumizi ya ofisi na hata majumbani, hivyo Jeshi la Magereza litajenga Kiwanda  kipya kikubwa cha samani  Dodoma ili kukidhi mahitaji halisi ya samani hizo,’’ anasisitiza  Dk. Malewa.
Dr. Malewa anasema ili kukidhi mahitaji halisi  ya samani kwa ajili ya Makao Makuu ya Nchi  yetu  jeshi lina mpango wa kununua vifaa hususani mashine za kisasa  zitakazoweza kuzalisha  samani kwa wingi zaidi na hivyo kutosheleza  mahitaji  ya samani mjini Dodoma.
Hivi karibuni  Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni,  akikagua moja ya miradi ya Jeshi la Magereza mkoani Dodoma alisema miradi mingi ambayo inaendeshwa na Jeshi la Magereza nchini kikiwemo kiwanda cha samani cha Gereza  la Ukonga cha jijini Dar es Salaam, kama serikali itasaidia katika kuiwezesha, italisadia taifa kupiga hatua na kuingia katika uchumi wa viwanda. 

No comments: