ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 20, 2017

WADAIWA KODI YA MAJENGO KUBURUZWA MAHAKAMANI

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo katika kikao kazi cha kuhamasisha ulipaji wa Kodi ya Majengo.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Arusha Ndg. Apili Mbarouk akizungumza katika kikao na wanahabari cha kuwakumbusha wananchi kuhusu ulipaji wa Kodi ya Majengo.
Baadhi ya wataalam waliohudhuria katika Kikao cha Mkuu wa Mkoa kuhamasisha uhamasishaji wa Kodi ya Majengo.


Nteghenjwa Hosseah, Arusha.
Wadaiwa sugu wa Kodi ya Majengo katika Jiji la Arusha watafikishwa Mahakamani mwanzoni mwa mwezi Julai endapo wataendelea kukaidi kutolipa Kodi hiyo katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka wa Fedha 2016/2017 unaomalizika Juni 30.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo katika kikao chake na waandishi wa habari kuwukumbusha wananchi kuhusu umuhimu wa kulipa kodi hiyo mapema kabla ya hatua kazi hazijachukuliwa wale ambao hawajalipa.
Alisema wamiliki wote wa majengo wanatakiwa kulipa Kodi hiyo kwa mujibu wa Sheria lakini hali hairidhishi kwani wengi wao hawajajitokeza kulipa wakati Serikali inategemea Fedha hizo kwa ajili ya Kutekeleza Miradi mbalimbali ya Maendeleo.
Aliongeza kuwa muda uliowekwa kwa ajili ya malipo hayo unaelekea ukikongoni:  Juni 30 itakua ni mwisho na baada ya hapo Sheria kali za Kisheria zitaanza kuchukuliwa kwa wote watakaobainika kuiibia Serikali kwa kutolipa mapato ya majengo wanayoyamiliki.
“Haiwezekani unamiliki nyumba halafu hutaki kuchangia kodi, ninatoa rai kwa wote kulipa kwa hiari kwa sababu baada ya hapo ni Faini ambayo ni mara tano ya kiasi kile ambacho ungetakiwa kulipa kwa sasa au kupelekwa Mahakami kwa mujibu wa Sheria.
Naye Meneja wa Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Arusha Ndg. Apili Mbarouk amesema mpaka Mwishoni wa Mwezi Mei walikuwa wameshafanikiwa kukusanya kiasi cha Tsh Bil.1  na kwa siku zilizobakia wanatarajia kukusanya zaidi ya kiwango walichokusanya kwa sasa.
Pia aliongeza kuwa katika maeneo yote ambayo hayajapimwa na kufanyiwa uthamini wamiliki watalipa Tsh 15,000 kwa mwaka na kwa yale maeneo ambayo yamefanyiwa uthamini wamiliki watalipa kwa kadiri ya thamani ya Majengo yao.
Aidha aliwataka wafanyabiashara na wananchi wote kutoa na kudai risiti kwa kila biashara inayofanyika ili kuhakikisha mapato ya Serikali yanakuwa salama na hayapotei kwa namna yeyote ile.
Katika hili tutaanza ukaguzi katika maeneo yote ya Mji huu kuanzia kwa wafanyabiashara kuhakikisha wanatoa stakabadhi kwa wateja wao na ambaye atabainika hajatoa atapigwa faini ta Tsh Mil 3 na kwa mwananchi ambaye atakuwa amenunua bidhaa bila kudai stakabadhi atatozwa faini ya Tsh 30,000.
Kikao hiki ni muendelezo ya vikao maalumu vya Kazi anavyovifanya Mkuu wa Mkoa wa Arusha pamoja na Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Areusha kuhakikisha mapato ya Serikali yanakusanya kwa ufanisi ili kufikia malengo waliyojiwekea. 

No comments: