Polisi wakizungumza na Meya wa Ubungo, Boniface Jacob (aliye ndani ya gari) walipokuwa wakimzuia asiendelee na ziara ya kukagua ujenzi wa miradi mbalimbali iliyopo katika Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis
Dar/mikoani. Viongozi watatu wa Chadema jana waliingia matatani katika maeneo tofauti nchini baada ya kujikuta mikononi mwa polisi, wengine wakidaiwa kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria.
Mkoani Iringa, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrick Ole Sosopi alikamatwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kufanya mkutano bila kibali chao.
Kaimu kamanda wa polisi mkoani Iringa, John Kauga ameliambia gazeti hili kuwa Sosopi alitenda kosa hilo Juni 16 mwaka huu katika vijiji vya Mlowo na Kinyika vilivypo tarafa ya Idodi.
“Ni kweli tunamshikilia hapa kituoni na tunaendelea na uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili, mtuhumiwa alifanya mikutano katika vijiji vya Mlowo na Kinyika bila kibali cha polisi,”alisema Kauga na kuongeza:
“Kwa sasa tunaendelea kumhoji na pindi tutakapokamilisha tutaendelea na hatua nyingine ila kwa sasa tunaendelea kumhoji kwanza,”alisema.
Akieleza jinsi Sosopi alivyokamatwa, Katibu wa Bavicha Mkoa wa Iringa, Jackson Mnyawami alisema juzi mwenyekiti huyo akiwa katika ziara ya siku saba katika Jimbo la Isimani alitumiwa ujumbe mfupi wa maneno na polisi ukimtaka kusitisha ziara na mikutano hiyo.
Alisema ujumbe huo pia ulimtaka jana aripoti katika ofisi ya RCO mkoani Iringa saa mbili asubuhi jambo ambalo alitekeleza.
Alisema Sosopi aliwasili katika ofisi hiyo muda huo mara baada ya hapo alipelekwa kituo kikuu cha polisi ambako alihojiwa kwa muda wa saa moja na kisha kupelekwa rumande.
“Aliwasili kituoni tukiwa wote na alipofika alihojiwa kwa muda wa saa hivi na walipomaliza kumhoji walimpeleka rumande na kutueleza kuwa kama tunataka kumwekea dhamana tukamuone RCO, tumeenda kwa RCO ametuambiwa tufike kesho (leo) asubuhi,” alisema Mnyawami.
Akizungumzia ziara ya Sosopi, Mnyawami alisema ilikuwa ni vikao vya ndani na ilianza Juni 9 mwaka huu na kwamba hadi anazuiwa kuendelea na mikutano yake alikuwa ametembelea kata sita kati ya 13 jimboni humo.
Wakati Sosopi akijikuta katika mshikemshike huo, jijini Dar es Salaam Meya wa Ubungo, Boniface Jacob naye alijikuta akiangukia mikononi mwa polisi kwa kosa ambalo halijajulikana alipokuwa akijianda kwenda na waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye kukagua miradi ya maendeleo ya Manispaa ya Ubungo.
Tukio hilo lilitokea jana saa sita mchana katika Makao Makuu ya Manispaa ya Ubungo yaliyopo Kibamba wakati Jacob akiwa katika msafara wa kuelekea kukagua miradi ya maendeleo akiwa na viongozi wenzake wa Chadema.
Askari wapatao wanne wakiwa katika gari aina ya Land Cruiser walifika katika eneo hilo kisha kuzuia msafara wa viongozi wa Chadema waliokuwa tayari kuanza ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya manispaa hiyo.
Baada ya kuzuia msafara huo, mmoja wa maofisa wa polisi alimfuata Jacob na kumweleza anamuhitaji kuambatana naye hadi Kituo cha Polisi Mbezi.
“Tunakuomba uongozane na sisi hadi kituoni, tuna maongezi na wewe yasiyozidi dakika 10 tukiridhika tunakuachia uendelee na shughuli zako,” alisema.
Ofisa huyo aliyejitambulisha kuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Mbezi alikwenda moja kwa moja hadi katika gari la Sumaye na kumweleza kuwa wanamuhitaji meya kwa dakika 10, kisha watamuachia.
Baada ya Jacob kuchukuliwa na polisi, Sumaye na viongozi wa Chadema waliendelea na ziara hiyo kwa kuanzia Shule ya Sekondari ya Matosa iliyopo Kata ya Goba.
Akiwa katika shule hiyo, Sumaye alisikitishwa na hatua hiyo na kusema huo ni mwendelezo wa uonevu dhidi ya viongozi wa upinzani na kwamba hatua hiyo inalenga kuwafanya baadhi ya watu kutojisikia huru katika nchi yao.
“Hili siyo jambo jema Serikali ivumilie, upinzani siyo uhalifu na wajue kuwa Chadema na viongozi wake ni chama halali na kinafanya kazi kama CCM. Habari ya kuwaandama watu wa Chadema kila mahali kitu hiki kinatusikitisha sana,” alisema Sumaye.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Suzan Kaganda simu yake ilipokelewa na msaidizi wake aliyejibu kamanda huyo yupo likizo na kwamba kaimu wake alikuwa zahanati.
Hayo yakitokea Iringa na Dar es Salaam kwa upande Kilimanjaro katika Wilaya ya Hai, kikao cha baraza la madiwani wa wilaya hiyo kiliendeshwa chini ya ulinzi wa polisi kutokana na amri ya kukamatwa kwa mwenyekiti na halmashauri hiyo, Helga Mchomvu (Chadema).
Kikao hicho kiliendeshwa chini ya ulinzi wa polisi baada ya polisi wa kituo cha polisi Bomang’ombe kumpelekea mwenyekiti wa halmashauri hiyo ujumbe wa kumtaka atoke nje kwa lengo la kumkata kumfikisha kituo cha polisi
Kufuatia hali hiyo, kikao hicho kiliendeshwa huku askari wa polisi wakiwa nje, wengine katika mlango wa kuingilia ukumbi wa halmashauri ambapo kikao hicho kilikuwa kikiendelea na ajenda zake za kawaida.
Kikao hicho kilichoanza saa 5:00 asubuhi na kumalizika saa 10:00 jioni kilimalizika huku polisi wakiendelea kumsubiria mwenyekiti huyo na kumtaka afike kituo cha polisi cha Bomang’ombe hali ambayo ilizua taaruki kwa madiwani na wananchi waliohudhuria kikao hicho.
Hali hiyo ilidumu kwa takribani dakika 20 kutokana na mwenyekiti huyo kutaka kujulishwa kosa la kutakiwa kufika kituo cha polisi, kitu ambacho askari hawakutaka kuweka wazi sababu ya kutakiwa kwake.
“Kama ni suala la kuharibiwa kwa miundombinu kwenye shamba la mbunge wa Hai sitanyamaza na huyo DC afanye maamuzi anayotaka lakini kama ni makosa nimefanya mtaani niko tayari kwenda polisi,”alisikika akisema.
Baada ya kikao hicho mwenyekiti huyo alichukuliwa na kupelekwa kituo cha polisi.
Imeandikwa na Geofrey Nyang’oro, Bakari Kiango na Fina Lyimo
No comments:
Post a Comment