Advertisements

Tuesday, June 20, 2017

Maalim Seif aishauri Ukawa njia mpya ya kujiimarisha

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad akizungumza na wananchi walioshiriki katika futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea nyumbani kwake Dar es Salaam juzi. Picha na Muyonga Jumanne

By Bakari Kiango, Mwananchi bkiango@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kama unajiuliza sababu za Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kutumia muda wake mwingi jijini Dar es Salaam tofauti na wakati mwingine, mwanasiasa huyo mkongwe ana jibu rahisi; anaendeleza harakati za kisiasa kwa kutumia futari.

Kwa takriban mwezi mmoja sasa, Maalim Seif ameweka kambi jijini Dar es Salaam, lakini ni mara chache amefanya shughuli zake hadharani.

“Zanzibar wametuzuia (kufanya shughuli za futari) kwa sababu ya ugonjwa wa kipindupindu,” alisema Maalim Seif wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na wanachama wa CUF wa Temeke iliyofanyika nyumbani kwa Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea.

“Lakini lengo hasa ni kumzuia Maalim Seif kwa sababu wanajua shughuli zangu za futari zinakuwa kubwa sana, nashukuru. Ila wamenipa nafasi na faraja zaidi ya kufanya shughuli zangu huku Dar es Salaam,” alisema Maalim Seif na kuibua kicheko kwa waliohudhuria hafla hiyo.

Alisema kwa kuwa Serikali imepiga marufuku shughuli za kisiasa hadi 2020 ikiwamo mikutano na maandamano wakati mtaji wa vyama vya siasa ni wananchi, hivyo ni bora wakatafuta njia mbadala ya kukutana nao kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Hata hivyo, Maalim Seif, ambaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika Serikali iliyopita ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar, alisema kitendo hicho si kizuri kwa kuwa kinaminya demokrasia na kinalenga kuwatenga wananchi na siasa.

Alisema ni jambo la ajabu kwamba vyama vya upinzani vimeridhia badala ya kubuni njia za kukutana na wananchi.

Maalim Seif, ambaye amekuwa akigombea urais wa Zanzibar tangu mwaka 1995 akiwa na CUF, alisema njia mojawapo ya kukutana na wananchi ni kujumuika nao kwenye hafla za futari zinazoandaliwa wakati huu wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

“Viongozi wenzangu wa upinzani, hasa Ukawa, tuwe wabunifu ili tuwafikie wananchi popote walipo. Vinginevyo vyama hivi vya upinzani vitatolewa roho na njia moja ni kama hivi leo nilivyojumuika nanyi kwenye futari nasikia faraja.”

Maalim Seif alisema pamoja na kuzuia mikutano ya kisiasa, Rais John Magufuli amekuwa akifanya ziara maeneo mbalimbali na kuzungumza anavyotaka, ikiwa ni pamoja na kuwaponda wapinzani.

“Rais anatushutumu wapinzani, lakini hataki kujibiwa. Tukisema demokrasia inapigwa vita nchini, tunaambiwa tumpe nafasi atekeleze ilani. Kwani miaka yote hakukuwa na ilani?” aliongeza, “Hivi tukifanya shughuli zetu za kisiasa tunamzuia nani asitekeleze ilani? Usipotekeleza ni kwa sababu huna uwezo, si kwa sababu ya mikutano. Rais ajitathmini uamuzi wake wa kuzuia mikutano wakati Sheria ya Vyama vya Siasa hairuhusu,” alisema Maalim Seif.

Sambamba na hilo, Maalim Seif aligusia mgogoro unaendelea ndani ya chama hicho na kusisitiza kuwa Profesa Ibrahim Lipumba si mwanachama wala kiongozi wa CUF na kwamba anayoyafanya yatawanyima wananchi haki yao, hasa Wazanzibari waliosusia uchaguzi wa marudio mwaka jana.

Awali, Mtolea alisema lengo la kuandaa futari hiyo ni kuwakutanisha pamoja wanachama na wakazi wa Temeke kwa ajili ya kubadilishana mawazo.

“Tukiungana na uamuzi wa Serikali ya kutofanya siasa, tutakuwa tunavunja Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba. Huu ukimya wetu wa kutofanya siasa ni sawa na kubariki mfumo wa kuviua vyama vya upinzani,” alisema Mtolea.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali ambaye alipopata nafasi ya kuzungumza alisema demokrasia ipo shakani hivyo kuna haja wapinzani kutumia njia ya mbadala ya kuwafikia wananchi.

“Kwa sasa chanzo cha habari ni kimoja tu ambacho ni Rais anayefanya kazi mbili kuwatumikia Watanzania na kazi ya uenyekiti wa CCM,” alisema Bobali.

No comments: