ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 20, 2017

Mbaroni akipenyeza simu tano gereza la Keko Dar

RAMADHANI Nombo anashikiliwa na Jeshi la Polisi, kituo cha Chang’ombe Temeke jijini Dar es Salaam kwa kosa la kupenyeza simu tano kwenye gereza la Keko.

Mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi baada ya chakula alichopeleka gerezani, kutoa mlio wakati wa ukaguzi. Kitendo hicho kilitiliwa shaka na askari magereza ambao walikikagua. Walipochunguza zaidi, waligundua kuwa kwenye chakula hicho, kulikuwa na simu tano. Nombo aliweka simu hizo tano, zikiwa zimezungushiwa karatasi ya plastiki nyepesi kuzuia uharibifu na kuweka katikati ya chakula aina ya ndizi nyama, ambazo zilikuwa kwenye bakuli kubwa.

Lakini, zoezi hilo halikuweza kufanikiwa baada ya kubainika na kutiwa nguvuni. Akizungumza na HabariLeo jana, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, Augustine Mboje alisema mtuhumiwa anashikiliwa Kituo cha Polisi Chang’ombe na baada ya mahojiano kwa kina atapandishwa kizimbani, kwani kitendo alichofanya ni uhalifu kama ulivyo uhalifu mwingine.

“Huyu kijana alitembelea mtu gerezani, na sheria za gerezani ukileta kitu lazima kikaguliwe kubaini kwamba kiko salama, katika ukaguzi chakula alicholetea ndugu zake, askari wetu walishtuka kusikia chakula hicho kikitoa mlio. “Kilipoangaliwa ndipo ikagundulika ni simu, basi tukamchukua kwa mahojiano na kumpeleka Polisi Chang’ombe kwa hatua zaidi,” alisema Mboje Mboje alisema kuwa kwa mujibu wa sheria, kimsingi Nombo amevunja sheria, Kifungu cha 86 (1) cha Sheria za Magereza Sura ya 58 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.

“Sheria inakataza kwa mtu yeyote kuingiza kitu chochote kisichoruhusiwa gerezani, na endapo ikithibitika mtu yeyote amekamatwa kwa kuingiza kitu chochote ambacho hakiruhusiwi kuingizwa gerezani, atahukumiwa kifungo kisichozidi miezi sita gerezani au faini, au vyote kwa pamoja,” alisema.

HABARI ;LEO

No comments: