Advertisements

Monday, June 19, 2017

VYETI VYA KUZALIWA VILIVYOANDIKWA KWA MKONO VYAANDALIWA MWONGOZO

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi ameuagiza Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) kuandaa miongozo itakayowezesha kuwaepusha Watanzania na usumbufu pindi wanapohitaji kutumia vyeti vya kuzaliwa vilivyoandikwa kwa mkono.
Akizungumza leo (Jumatatu) na wadau kuhusu usanifu mpango wa usajili wa matukio muhimu kwa binadamu na ukusanyaji wa takwimu (CRVS), Profesa Kabudi amesema amepokea malalamiko kutoka kwa watu kuhusu vyeti hivyo.
“Nimepokea malalamiko kuwa kuna baadhi ya taasisi za Serikali na sekta binafsi zinakataa kupokea vyeti vilivyoandikwa kwa mkono na badala yake wanataka vilivyoandikwa kwa mashine,” amesema.
Profesa Kabudi amesema mwongozo huo utasaidia watu kutokata tamaa kutokana na usumbufu wanaoupata baada ya vyeti hivyo kukataliwa.
‘’Wanataka vile vya kompyuta, mbona vyeti vya ndoa na vifo huwa vinaandikwa kwa mkono, mtu wa kijijini anapata wapi kompyuta? Naomba mpokee na sitaki tena kusikia malalamiko kuhusu kukataa vyeti vinavyoandikwa kwa mkono,’ ’amesema.
Waziri amesema Serikali imeamua kuboresha mfumo wa usajili uliopo na kuanzisha utakaofanya kazi vizuri wa usajili wa matukio muhimu ya binadamu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Rita, Profesa Hamis Dihengo amesema takwimu za sensa ya watu na makazi za mwaka 2012 zinaonyesha kuwa asilimia 13.4 ya wananchi ndio wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.
Profesa Dihengo amesema idadi hiyo ni ndogo na ni kiashiria kuwa Serikali haina taarifa za idadi kubwa ya wananchi.
‘’Pamoja na takwimu hizi wapo wananchi ambao huzaliwa na kufa bila hata taarifa zao kuonekana katika kumbukumbu zozote za serikali, hivyo tunaomba Watanzania wajitokeze kupatiwa vyeti vya kuzaliwa,’’ amesema.

No comments: