ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 19, 2017

WATUMUSHI OFISI YA MWANASHERIA MKUU WAZINGATIE MAADILI YA UTUMISHI

Naibu Mwanasheria wa Serikali Bw. Gerson Mdemu akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake wa kazi na watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Tabora wakati wa wiki ya Utumishi wa Umma. Katika Mkutano huo Naibu Mwanasheria Mkuu, amesisitiza watumishi wa Ofisi yake kuzingatia misingi na maadili ya Utumishi. Kushoto kwa Naibu Mwanasheria Mkuu ni Wakili wa Serikali Mfawidhi Bw. Jackson Bulashi na kulia ni Bw. Benny Kabungo Mkurugenzi wa Utumishi na Raslimali Watu.
Sehemu ya Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Tabora wakimsikiliza Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa kikao kazi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho wa wiki ya Utumishi wa Umma. Katika kuadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ( 16-23) ilitenga siku mbili za kukutana na wadau na watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu.

Image result for ofisi ya mwanasheria mkuu
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WATUMISHI OFISI YA MWANASHERIA MKUU WAASWA KUZINGATIA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA

Na Mwandishi Maalum

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Mdemu, amewataka watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiwamo Mawakili wa Serikali kuhakikisha kwamba wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia kanuni na maadili ya Utumishi wa Umma.

Ametoa wito huo mwishoni mwa wiki, mkoani Tabora, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kanda ya Tabora.

Mkutano baina ya Naibu Mwanasheria Mkuu na watumishi hao umefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhamisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma inayoadhimishwa kuanzia tarehe 16 hadi 23 mwezi huu.

Naibu Mwanasheria Mkuu, amewaambia Watumishi hao kupitia wenzao wa Tabora kwamba, anafahamu vema kuwa pamoja na kubeba dhama kubwa wanakabiliwa na mazingira magumu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Hata hivyo, amebainisha kwamba, mazingira magumu ya kazi na changamoto mbalimbali zisiwakatishe tamaa na hivyo kuwapelekea kutozingatia maadili na misingi ya kanuni za utumishi wa umma au kufanya mambo mengine yanayokwenda kinyume na taaluma zao na dhamana wanayoibeba.

“ Suala la kwamba mnafanya kazi katika mazingira magumu na yenye changamoto nyingi halina mjadala, tunajitahidi kwa kila namna kuangalia namna nzuri zaidi ya kuboresha mazingira ya kazi zetu kwa kupunguza baadhi ya changamoto”.

Na kuongeza “Ninawaomba muendelee kuwa wavumilivu, tekelezeni majukumu yanu bila woga, tembeeni kifua mbele kwani mnabeba dhamana kubwa”. Amesisitiza Naibu Mwanasheria Mkuu Bw. Mdemu.

Katika kikao kazi hicho, Naibu Mwanasheria Mkuu akatumia fursa hiyo kuwasilisha salamu za Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju na akawapongeza na kuwashukuru watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa namna wanavyovijituma na kufanya kazi kwa weledi licha ya mazigira magumu ya kazi.

Akasema anafarijika sana kuona namna Mawakili na watumishi hao wa Serikali wanavyoendelea kujituma kuisadia na kuishauri Serikali ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu.

Kupitia kikao hicho, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewaagiza Wakurugenzi wa Divisheni zote zinazounda Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, kuanda utaratibu utakaowawezesha kwenda mikoani kwa lengo la kubadilishana mawazo, kuelimishana na kufahamishana na kuhabarishan juu ya masuala mbalimbali yanayohusu utendaji na utekelezaji wa majukumu yao.

Akasema, Wakurugenzi wa Divisheni ambao wapo Makao Makuu, wakiwa na utaratibu huo licha ya ufinyu wa Bajeti utasaidia sana kutatua baadhi ya changamoto lakini kubwa zaidi kuwaweka karibu wa watendaji wa mikoani.

Kikao kazi hicho kiliwapatia fursa watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kumuelezea Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao kuishauri na kuisaidia Serikali.

Baadhi ya changamoto walizoeleza ni pamoja na ufinyu wa bajeti, uhaba na uchakavu wa vitenda kazi.

Naibu Mwanasheria Mkuu aliahidi kuzifanyia kazi changamoto hizo na nyinginezo kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi.

Naibu Mwanasheria Mkuu, alifuatana na Mkurugenzi wa Utumishi na Raslimali watu Bw. Benny Kabungo, Mkurugenzi wa Divisheni ya Katiba na Haki za Binadamu Bi. Sara Mwaipopo, Mkurugenzi wa Divisheni ya Sheria Bw. Obadia Kamea na Mkurugenzi wa Divisheni ya Mikataba Bi. Evelyne Makala.

Wengine ni Mkurugenzi Msaidizi wa Divisheni ya Mashtaka Bw. Ayub Mwenda, Mwakilishi kutoka Divisheni ya Uandishi wa Sheria Wakili Mwandamizi Bw. Shabani Kabuga na Mwakilishi wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani.

Wakurugenzi hao kwa nayakati tofauti walielezea majukumu ya Divisheni zao pamoja na kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa na watumishi.

Katika kutekeleza maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilitenga siku mbili June 16 na 17 za kukutana na wadau kutoka Taasisi za Serikali na watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu.

Miongoni mwa wadau hao ni Jeshi la Polisi lililowakilishwa Afande RCO Simon Maigwa, Mahakama ikiwakilishwa na Hakimu Mkazi,Mhe. Jactan Rweshora, Kamanda wa Takukuru Tabora Bw. Fidelis Kalungura, Magereza iliyokilishwa Assistant Inspector Afande Sudi na wawakilishi wengine kutoka Maliasili, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mawakili wa Serikali na Wanasheria.

No comments: