ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 27, 2017

Korti yamuachia Lissu kwa dhamana

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu
By Tausi Ally, Mwananchi

Dar es Salaam. Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amepata dhamana baada ya ombi la mawakili wa Serikali la kuomba Mahakama imnyime haki ya kudhaminiwa kutupiliwa mbali na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri ametoa uamuzi huo leo, Julai 27 akimtaka Lissu kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambapo kila mmoja atasaini bondi ya Sh10 milioni.

Pia, amemtaka asitoke nje ya Jiji la Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha Mahakama.

Hakimu ameahirisha kesi hiyo kwa muda kusubiri wadhamini. Kutokana na ulinzi kuimarishwa mahakamani hapo watu wengi walizuiwa getini.

Julai 24, jopo la mawakili wanne wa Serikali, Kishenyi Mutalemwa, Simon Wankyo, Paul Kadushi na Tulumanywa Majigo waliwasilisha hoja mahakamani hapo wakiomba Lissu anyimwe dhamana.

Jopo la mawakili 18 wanaomtetea Lissu, likiongozwa na Fatma Karume na Peter Kibatala liliomba mteja wao apewe dhamana.

Katika shauri linalomkabili, Lissu anadaiwa Julai 17 eneo la Mtaa wa Ufipa, Kinondoni, Dar es Salaam alitoa maneno ya uchochezi kuwa, 'Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ni ya kibaguzi wa kifamilia, kikabila, kikanda na kidini.'

No comments: