Advertisements

Sunday, July 23, 2017

Msigwa: Nchi inapita katika kipindi kigumu

By Elias Msuya, Mwananchi; emsuya@mwananchi.co.tz

Kumekuwa na maoni tofauti kuhusu utawala wa awamu ya tano. Wakati baadhi wakiupongeza kwa utendaji mzuri na mapambano dhidi ya ufisadi, wengine, hasa vyama vya upinzani, wanaulaumu kwa kukandamiza demokrasia.

Hivi karibuni gazeti hili lilifanya mahojiano na mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa ambaye pamoja na mambo mengine ameukosoa akisema Tanzania inapitia katika kipindi kigumu kulioko wakati mwingine wowote kutokana na jinsi utawala wa sasa unavyoendesha mambo. Endelea.

Swali: Unaonaje hali ya siasa nchini kwa sasa?

Jibu: Kwa mtazamo wangu wa kisiasa ambao pia naamini ni mtazamo wa chama (Chadema), nchi inapita katika wakati wa aina yake tangu mfumo wa vyama vingi umeanza katika nchi hii.

Tunapita mahali ambapo tumekosa uhuru wa mawazo, mtu mmoja akisema jambo linakuwa sheria.

Tunapita katika kipindi ambacho Bunge limetekwa na Serikali. Tunapita katika kipindi ambacho watawala wanatumia vyombo vya Serikali katika mapambano yao na ni waoga tu ambao hufanya hivyo.

Swali: Unamaanisha nini unaposema Bunge limetekwa na Serikali?

Jibu: Kwa mfano Mheshimiwa Rais aliamua kununua ndege kinyume kabisa na sheria ya fedha na bila Bunge kuidhinisha na haikuwepo kwenye bajeti. Ni kinyume kabisa kwa sababu inakiuka mgawanyo wa madaraka, kwamba tuna mhimili huu wa Bunge, Mahakama na Serikali.

Tunapita kipindi ambacho watawala wamejiweka wazi zaidi jinsi walivyo na inadhihirisha hata usemi wangu kwamba ufalme haubadili akili ya mtu, bali unamuweka mtu wazi jinsi alivyo.

Swali: Unadhani Serikali inakosea wapi hasa?

Jibu: Utawala wa awamu ya tano ni utawala ambao hauna vifaa vya kazi, ni kama fundi gereji ambaye hana vifaa, hauna ujuzi katika uongozi. Kwa mfano kama taa ya gari imeharibika, ni fundi wa ajabu tu atakayekwenda kuigonga kwa nyundo. Pale unahitaji tu bisibisi.

Humo kuna busara, hekima, maarifa, kuna wakati unatumia polisi na kuna wakati unahitaji mjadala, kwa sababu nchi hii inaongozwa kwa pamoja kama timu.

Swali: Unaonaje vita ya ufisadi na jinsi Serikali inavyopambana na kubana matumizi?

Jibu: Ni utawala unaojipambanua kama wapambanaji wa ufisadi, lakini wananunua viongozi wetu wadhaifu, mmeona madiwani wetu. Lakini sisi kama Chadema tunaona kama fursa, kwa sababu wamedhihirisha kuwa ni waoga.

Kwa hiyo katika hili ombwe au dhiki kama hii, viongozi wa kweli wanakwenda kuonekana. Tunakwenda kutofautisha kati ya boys and men (wavulana na wanaume). Sisi tunaimarishwa kuliko kudhoofishwa.

Swali: Mna uhakika gani kama viongozi wenu wananunuliwa?

Jibu: Nadhani umesikia katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa aliongea na vyombo vya habari. Tuna ushahidi wa kutosha kuhusu jambo hili.

Hebu tuliangalie kwa upana, kama kweli Serikali inakusanya kodi nyingi, kama kweli Serikali hii imeleta viwanda vingi na maendeleo mengi kama wanavyosema, kwa nini haruhusu watu wengine tuzungumze?

Kwa sababu angetufanya sisi tusiwe na cha kuzungumza. Uwiano wa Bunge ni 7:2:1, yaani wakiongea wabunge saba wa CCM, Chadema tunaongea wawili, CUF anaongea mmoja.

Swali: Kwa nini hujuma hizo zifanywe tu Arusha?

Jibu: Arusha, kwanza CCM inaamini ni ngome ya Chadema, hivyo wanajua wakiharibu watakuwa wamekiharibu chama. Lakini tujiulize, ina maana watu wa Arumeru tu ndiyo wanaridhika na utendaji wa Magufuli?

Pili, haiwezekani mtu unayemuunga mkono, unaacha kazi. Kwani nikimuunga mkono Rais Magufuli lazima niache ubunge au udiwani? Kwa hiyo huo unaonekana kama mchezo tu hata mtoto wa darasa la pili anaujua.

Swali: Hivi karibuni Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa alitangaza kuwa atagombea tena urais 2020. Je, mmeshampitisha au anawezaje kujitangaza mapema?

Jibu: Kila mwanasiasa ni ambitious, yaani ana matamanio. Hata mimi nitagombea ubunge jimbo la Iringa mwaka 2020, sidhani kama ile hoja ni tatizo. Haimaanishi kwamba kutangaza kugombea, kutazuia watu kuchukua fomu.

Kama mtu atashindwa kuchukua fomu kwa sababu Lowassa ametangaza, huyo hatufai. Atakuwa kama CCM inayotaka kushinda bila kushindana; yaani mmoja anafungwa mikono na kamba halafu ndiyo unapambana naye?

Swali: Ikitokea kada mwingine wa Chadema akasema atagombea, si itakuwa vurugu?

Jibu: Haitakuwa vurugu, kwanza tutapata wana-Chadema wengi wanaogombea ili tuwe na ushindani mkubwa, ili tuchuje tupate wagombea wazuri.

Hata mimi kusema nitagombea Iringa, haimaanishi kuwa nitagombea. Kuna mchakato wa chama utafanyika.

Swali: Hivi karibuni mmesikika mnataka kufungua kesi mahakamani kupinga mnaouita unyanyasaji wa Jeshi la Polisi. Unadhani ni njia mwafaka kwa sasa?

Jibu: Tunatafuta njia zozote, kama mnavyoona tumekwenda kidiplomasia kwa utawala huu ambao unavunja sheria kama nilivyoeleza. Kwanza tunataka Tanzania iwe na amani, lakini wale wanaovunja sheria tutawapeleka mahakamani.

Tunaamini kufanya mikutano ni haki yetu ya kikatiba na hatutarudishwa nyuma.

Swali: Kuna wakati mlikorofishana na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson mkakimbilia kwa Spika Job Ndugai, lakini sasa mmebadilika tena mnamlaumu Spika. Kulikoni?

Jibu: Naibu Spika Dk Tulia alikuwa hataki hata tuongee na bado anafanya mazoezi, kinyume na mfumo wa mabunge ya Jumuiya ya Madola.

Kwa hiyo Spika aliporudi aliona tatizo lile na akajaribu ku-balance kwamba tufanye kazi nzuri. Tulipongeza hatua ile kwamba anakuwa kama ni baba wa nyumba na mhimili ule kama mingine inavyofanya kazi ya nchi.

Spika anapaswa kuwa na wivu uliopitiliza kulinda mhimili wake kama ambavyo jaji anapaswa kulinda mhimili wake wa mahakama. Tunachomlaumu sasa Ndugai ni kwamba ametekwa na Serikali kiasi kwamba Bunge la Tanzania limegeuka kuwa rubber stamp (muhuri).

Kwa hiyo, kuwepo pale Bunge ni kumaliza hela za wananchi. Kwa sababu hakuna mahali ambapo Bunge linaikosoa Serikali, zaidi meno pekee ambayo Bunge linayo ni kuwatoa wapinzani nje ya Bunge.

Lakini haliwezi kuikosoa Serikali, kwamba mmenunua kinyume na Sheria ya Fedha, mmefanya kinyume. Ukijadili hayo umefanya kosa, mara kaa chini; nitakutoa nje; lete pingu. Sasa Bunge gani hilo?

Swali: Kutoonyesha Bunge moja kwa moja kwenye televisheni kumeathiri kwa kiasi gani kambi ya upinzani?

Jibu: Kutoonyesha Bunge ‘live’ hakujaathiri upinzani, bali kumeathiri Taifa. Kwanza Taifa linashindwa kuwaona viongozi wao na vipaji. Wengi wetu mlituona kwa sababu ya televisheni na tunaondoka, wengine wanakuja.

Sasa wabunge wa CCM nimesema wanaongea saba, kwa hiyo wabunge wengi walioingia Bunge hili wanalazimika kufanya siasa za ndani.

Ni hasara kwa sababu tungependa vipaji vingine viibuke, sasa haviwezi kuibuka kama wamefungiwa ndani. Kuna vipaji vingine vinakuja, sasa kuwafungia ni hatari zaidi kwa Taifa siyo kwa Chadema pekee.

Vilevile wananchi wanakosa habari za kutosha kwa sababu mle bungeni kuna habari nyingi na unapochangia unakwenda kuwasemea wengi, kwa hiyo iliwafanya wabunge wengi wasome ili usije kuongea kichekesho. Kwa hiyo ni athari kwa Taifa si kwa upinzani.

Swali: Katika awamu ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete mlimlaumu kuwa ni dhaifu, lakini sasa mnamsifu huku mkilaumu Rais Magufuli, inakuwaje?

Jibu: Kwanza lazima utambue kwamba siasa ni mchezo unaobadilika na udhaifu wa rais mmoja hauondoi udhaifu mwingine. Haimaanishi kwamba udhaifu aliokuwa nao Kikwete umekwisha, kuna maeneo alikuwa dhaifu na kuna maeneo alikuwa mwema, tutaendelea kusema.

Tulitegemea mtawala anayekuja angeacha udhaifu wa Kikwete akachukua mazuri yake akaenda nayo. Hayo ni maneno ambayo hata Baba wa Taifa alisema, mnaacha yote mnachukua mabaya?

Tulitegemea kwa mfano kwenye masuala ya uchumi, Magufuli aanzie pale ambapo Kikwete aliacha mazingira ya uwekezaji. Lakini aliyekuja sasa ame-disturb (vuruga) wawekezaji kwenye nchi yetu.

Kwenye demokrasia, Kikwete hakufanya vizuri sana lakini alisogea hatua moja, tuliamini mwingine angesogea mbele zaidi lakini yeye anaamini kwamba demokrasia ni kikwazo cha maendeleo.

Swali: Kuna taarifa kuwa Bunge lina hali mbaya kifedha kiasi kwamba wabunge hamjalipwa fedha za Juni kwa siku 50 sasa?

Jibu: Siyo kwamba Bunge lina hali mbaya bali ni Serikali, kwa sababu Bunge hatuzalishi pale, tunategemea fedha kutoka kwa Serikali, sasa kama haileti hela tutalipwaje?

Hela zimekuwa zikilipwa kwa taabu taabu, mimi ni kamishna wa Bunge ninajua kabisa kuna wakati hela zinacheleweshwa mpaka wabunge wanatusumbua jamani hela huko mbona bado hatujalipwa.

Swali: Katika Bunge lililopita ulikuwa Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii na ulikaririwa ukisema, Operesheni Tokomeza haikuwa na manufaa. Kwa nini?

Jibu: Katika Serikali iliyopita, Rais Kikwete alikuja na Matokeo Makubwa Sasa (BRN). Mimi nilikuwa miongoni mwa waliokosoa neno ‘Big Result Now’ iliyobandikwa kwenye milango lakini watendaji mle ndani hawajawa na ujuzi wala kuwezeshwa.

Tokomeza iwe matokeo ya utendaji kazi. Bado Serikali haijawa na mkakati mzuri wa kuhakikisha kuwa hawa watu wanapata ujuzi na uwezo wa kupambana na majangili. Hata hivyo kwa sasa tembo wameongezeka.

Swali: Kwa hiyo unapongeza juhudi za Rais Magufuli katika utunzaji wa rasilimali hadi idadi ya tembo imeongezeka?

Jibu: Siwezi kusema ni jitihada za Magufuli. Mimi wakati ule nilikuwa Waziri Kivuli wa Maliasili tumesafiri nchi nyingi na kukutana na balozi zote. Waziri Lazaro Nyalandu wakati ule alijitahidi sana kwa sababu alifanya ushirikishaji kama wanavyofanya Waingereza wenyewe.

Tulikutana na balozi wa Marekani aliyeondoka alitusaidia sana. Tulikutana na balozi wa Ujerumani, Uingereza, Saudi Arabia mpaka wakatoa vifaa vya kulinda. Kwa hiyo haya mambo hayakuanza awamu hii, kulikuwa na maandalizi mengi. Nyalandu alifanya mikakati kwenye masuala ya jumuiya za kimataifa zinazohusiana na uhifadhi.

Swali: Kuna wakati ilielezwa kuwa ushirikiano wako na Nyalandu ulikung’oa meno kama mpinzani?

Jibu: Mimi ninawajibika kwa yale ninayoyasema si kwa jinsi mtu watu wanavyonichukulia. Nilisema mtazamo wake ulikuwa tofauti na mawaziri wengine.

Wengine waliitafsiri vibaya, lakini mimi mikono yangu ni misafi. Kama niling’olewa meno ni sawa. Lakini wakati mimi ni waziri kivuli ndipo Wizara ya Maliasili ilikuja juu. Kwa hiyo wananchi wanavyoelewa huwezi kuwazuia.

Swali: Sasa umekuwa Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, unaona utofauti gani na awamu iliyopita?

Jibu: Nadhani mimi bado ni waziri kivuli mzuri wa mambo ya nje. Nikisimama kutoa hotuba yangu lazima Serikali ijipange. Waziri mwenyewe wa Mambo ya Nje inaonekana diplomasia inamtupa nje. Anazungumzia diplomasia ile ya nchi za mstari wa mbele za kusini mwa Afrika, nani anajali hayo mambo kwa sasa?

Bahati mbaya tuna Waziri wa Mambo ya nje aliyepitwa na wakati, sasa hivi tuna diplomasia ya uchumi.

Swali: Lakini Dk Augustine Mahiga ni msomi aliyebobea kwenye masuala ya diplomasia na amefanya kazi Umoja wa Mataifa kwa muda mrefu. Utasemaje kuwa amepitwa na wakati?

Jibu: Yule ni Mhenga. Kwa sababu kwenye hotuba zangu nazungumzia diplomasia ya uchumi, yeye anazungumzia nchi zilizo mstari wa mbele, Tanzania ina heshima kubwa, inasifiwa, nani anajali kama hakuna uchumi?

Swali: Katika Bajeti ya mwaka jana, mlilalamikia suala la Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye utalii, lakini ripoti zinaonyesha idadi ya watalii imeongezeka?

Jibu: Kuna kodi nyingi za maudhi zimeondolewa baada ya kusikia ushauri, lakini hata hivyo iliongezeka asilimia moja tu kama ulisikia ripoti ya Benki ya Dunia.

Hata kama idadi ya watalii imeongezeka, kwa nini mpaka sasa Serikali haitangazi kama ilivyokuwa imetangaza? Hata kama wametangaza hivi karibuni, ni baada ya kuwasema.

Ukifuatilia, utaona biashara nyingi zimefungwa na siyo Kariakoo tu na pengine. Kama Serikali inasema mambo yanakwenda vizuri, mimi naishi na wananchi kule chini, michicha haiuziki, mtu anakwenda na tenga anarudi na mchicha unaoza au kukauka.

Kule Iringa ni maarufu kwa ulaji wa bagia, kuna bagia zinalala halafu asubuhi inabidi atumbukize tena kwenye mafuta, halafu zinaleta matatizo.

Ukienda kwenye biashara za kati nako kuna matatizo, watu wamekimbia kwenye maeneo yao kwa sababu ya mikopo ya Pride, Finca n.k. Sasa kama hali nzuri, kwanini haya yatokee?

Swali: Unajipangaje kulitetea Jimbo la Iringa, maana kuna taarifa ya kulirejesha CCM?

Jibu: Taarifa za CCM kulichukua Jimbo la Iringa ninazo, lakini hakuna hata siku moja ambayo walipenda mimi niwe mbunge wa Iringa Mjini. Mwaka 2010 hawakutaka niwe, nikawa. Wakasema nimekuwa kwa sababu kipenzi chao Mwakalebela hakuteuliwa.

Basi nikamwomba Mungu na nilisema bungeni kwamba, mleteni huyo kipenzi cha watu wa Iringa. Mama Mbega (Monica) nilimshinda kwa kura 2,000, huyo kipenzi cha watu wa Iringa nikamshinda kwa kura 10,000.

No comments: